HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, December 14, 2021

BALOZI SHIYO AWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO AU

  BALOZI wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Afrika, Mhe. Innocent Eugene Shiyo amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Mhe. Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa tarehe 13 Desemba 2021.


Wakati wa hafla hiyo, Mhe. Mahamat amempongeza Balozi Shiyo kwa kuteuliwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Afrika. Amemkarabisha na kumtakia kheri katika utekelezaji wa majukumu yake.

Mhe. Mahamat na Balozi Shiyo wamekubaliana kushirikiana katika kusimamia utekelezaji wa masuala ya kipaumbele ya Umoja wa Afrika hususan juhudi za kupambana na UVIKO-19 ikiwemo upatikanaji na utengenezaji wa chanjo za ugonjwa huo barani Afrika pamoja na mikakati ya kunasua uchumi wa Afrika dhidi ya athari za UVIKO-19.

Wamekubaliana kushirikiana katika kutekeleza miradi ya kipaumbele ya Umoja wa Afrika yenye lengo la kuimarisha na kukuza Mtangamano wa Afrika hususan ujenzi wa miundombinu ya uchukuzi, kuboresha mazingira ya biashara kupitia Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) na juhudi za uimarishaji wa hali ya amani, usalama na utulivu barani Afrika.

Vilevile, wamekubaliana kuhusu umuhimu wa utekelezaji wa mchakato mabadiliko ya kitaasisi ndani ya Umoja wa Afrika ili kuboresha utendaji wa umoja huo.

Aidha, Mhe. Balozi Shiyo alizungumzia kwa undani umuhimu wa kutekeleza maazimio mbalimbali ya Wakuu wa Nchi na Serikali ya kuwezesha lugha ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha za kikazi za umoja wa Afrika. Mhe. Mahamat alimhakikishia Mhe. Balozi Shiyo kuwa ataunga mkono ombi la Tanzania kutaka lugha ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha za Kazi za Umoja wa Afrika.

Mhe. Mahamat alitumia fursa hiyo kutoa salamu za shukurani kwa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumwalika kushiriki Maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara tarehe 09 Desemba 2021 na zaidi kwa kukubali kuonana naye tarehe 10 Desemba, 2021 ambapo alipata fursa ya kumwelezea Mhe. Rais kuhusu maeneo mbalimbali ya kipaombele ndani ya Umoja wa Afrika na Afrika kwa ujumla.
Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Afrika, Mhe. Innocent Eugene Shiyo amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Mhe. Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika.

Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Afrika Mhe. Innocent Eugene Shiyo akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika baada ya kuwasilisha Hati za Utambulisho.

Picha ya pamoja

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad