UWEPO WA MTANDAO WA KUPINGA UDHALILISHAJI PEMBA WASAIDIA JAMII KUFUATILIA HAKI ZAO - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, November 22, 2021

UWEPO WA MTANDAO WA KUPINGA UDHALILISHAJI PEMBA WASAIDIA JAMII KUFUATILIA HAKI ZAO

 


WANAMTANDAO wa kupinga udhalilishaji Pemba wamesema uwepo wa mtandao huo katika jamii umefanikiwa kuisaidia jamii kutambua namna ya kufuatilia haki zao ili kukabiliana na vitendo hivyo katika jamii.

Hayo yamebainishwa na wanamtandao hao wakati wa mkutano wa kuwasilisha ripoti ya mwaka ya utekelezaji wa majukumu ya mtandao huo ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa kutumia jukwaa la habari kumaliza vitendo vya udhalilishaji unaotekelezwa na TAMWA ZNZ kwa ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Denmark -DANIDA. 

Haji Shoka kutoka wilaya ya Mkoani alisema kupitia utoaji wa elimu kwa jamii ya namna ya kupambana na vitendo hivyo wamewafikia wanajamii wengi katika shehia na kuwaelimisha mbinu za kuibua na kufuatilia kesi hizo katika ngazi mbaimbali.

“Kwa mwaka 2021 katika utoaji wa elimu kupitia mikutano, tuliwafikia watu 8,043 katika makundi mbalimbali kwenye shehia za wilaya ya Mkoani ambapo mikutano hiyo tuliifanya katika maeneo tofauti ikiwemo mashuLeni na kwenye madrasa.

Alibainisha kupitia mikutano hiyo imesaidia kuimarisha ukaribu wa mtandao na wanajamii hasa wahanga wa matukio hayo na kurahisisha jamii kutoa mashirikiano ya kuripoti kesi hizo pale zinapotokea.

Alisema, “kutokana na shughuli hizi ambazo tumekuwa tukizifanya imetusogeza karibu zaidi na wanajamii hasa wahanga wa udhalilishaji kwani wamezidi kutuamini na kutoa mashirikiano ya karibu pale linapotokezea tukio la udhalilishaji kwenye jamii.”

Aidha alieleza ucheleweshaji wa upelelezi kwa matukio ya udhalilishaji bado ni kikwazo kinachozikabili kesi hizo na kupelekea wahanga kukosa haki zao kwa wakati.

Alisema “upelelezi kuchelewa kwa matukio ya udhalilishaji yanaporipotiwa bado ni changamoto na hili linapelekea wahanga na wanajamii wengi kukata tamaa ya kuendelea kufuatilia kesi hizo.”

Kuhusu ufuatiliaji wa kesi alisema, “katika ufuatiliaji wa kesi, tulifuatilia jumla ya kesi 32 na kati ya hizo kesi za utelekezaji ni 4, ubakaji 17, ulawiti 6 na mimba za umri mdogo zilikuwa 5.”

Nae Siti Faki ali kutoka Wilaya ya Wete alisema mtandao huo kwa wilaya hiyo umefuatilia na kuibua kesi 48 za aina mbalimbali huku kati ya kesi hizo, 6 tayari zimeshatolewa hukumu zake.

“Kwa mwaka huu sisi kama mtandao Wilaya ya Wete tumefuatilia kesi 48 kati ya hizo, kubaka zilikuwa 23, shambulio la aibu 10, mimba kesi 2, kunajisi mvulana 7, na kutorosha kesi 4,” alisema.

Alieleza kwamba licha ya juhudi kubwa ambazo mtandao huo umekuwa ukizichukua kukabiliana na udhalilishaji lakini walibaini kuwepo kwa changamoto ya uhaba wa wakalimani kwa kesi zinazohusu wenye mahitaji maalum.

Alisema, “ katika utekelezaji wa majukumu yetu wanamtandao wilaya ya Wete tulibaini bado kuna tatizo la ukalimani kwa kesi za wenye mahitaji maalum jambo linalopelekea kuchelewa kesi zao.”

Mratibu wa TAMWA Pemba, Fat-hiya Mussa Said aliwataka wanamtandao kuongeza nguvu katika utoaji wa elimu ya ushahidi ili kujenga jamii yenye uelewa wa taratibu za kutoa ushahidi kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa haki.

Alisema, “kwasasa tuendelee kujikita zaidi kuwaimarisha mashahidi wawe na uwezo wa kwenda kutoa  kutoa ushahidi mahakamani ili tupunguze hili suala la kesi nyingi kufutwa kwa kukosa ushahidi unaojitosheleza.”

Mradi wa tumia jukwaa la habari kumaliza vitendo vya udhalilishaji Zanzibar ni mradi  ambao unatekelezwa katika Wilaya Tano za Zanzibar, Unguja Wilaya tatu na Pemba wilaya mbili za Mkoani na Wete kupitia ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Denmark -DANIDA. 

Mratibu wa TAMWA ofisi ya Pemba Fat-hiya Mussa akifungua mkutano wa wanamtandao wa kupinga udhalilishaji Pemba 
Mjumbe wa mtandao kutoka Wilaya ya Mkoani, Haji Shoka akiwasilisha ripoti ya utekelezaji wa majukumu ya mtandao huo kwa mwaka 2020.
 Mshiriki wa mkutano akichangia wakati wa uwasilishaji wa ripoti ya mwaka kwa wanamtandao huo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad