HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, November 27, 2021

TARURA, MADIWANI NA KAMATI YA ULINZI NA USALAMA ILALA KUSHIRIKIANA KUFANIKISHA MFUMO WA UKUSANYAJI USHURU WA MAEGESHO

 



Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi. Geofrey Mkinga (kushoto,) pamoja na Katibu Tawala Wilaya ya Ilala (kulia,) Charangwa Seleman wakifatilia mjadala katika kikao hicho.



*Wakubaliana ushirikiano mfumo wa kielektroniki wa ushuru wa maegesho

WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mjijini Tanzania (TARURA) imetoa elimu ya kuwajengea uwezo Madiwani na kamati ya ulinzi na usalama wa Halmashauri ya jiji la Ilala juu ya matumizi ya mfumo wa kieletroniki wa ushuru wa maegesho ambao utaanza kutumika Desemba Mosi mwaka huu katika mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Mwanza, Singida na Dodoma.

Akizungumza wakati akifungua kikao hicho Katibu Tawala wa Halmashauri ya Jiji la Ilala Charangwa Seleman amesema mfumo huo mpya wa ukusanyaji mapato ni sahihi katika kuzuia mapato yaliyokuwa yanapotea pamoja na kuziba mianya mbalimbali itakayosababisha kupotea kwa mapato hayo.

Amesema, kushirikishwa kwa Madiwani na viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama wa jiji hilo ni muhimu kwa kuwa hao ni viungo muhimu walio karibu na wananchi hivyo wanategemea matokeo chanya mara baada ya mkutano huo katika uwezeshaji wa kufanikiwa kwa mfumo huo.

Kwa upande wake Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi. Geofrey Mkinga  amesema matumizi ya mfumo huo ni katika kwenda na azma ya Serikali ya kuhama kutoka mfumo wa analojia kwenda kidigitali hasa katika ukusanyaji wa mapato na baada ya changamoto kadhaa kutokea na kusimamishwa kwa mfumo huo kwa muda marekebisho yamefanyika na elimu zaidi imetolewa kwa Umma kupitia makundi mbalimbali yakiwemo vongozi na waandishi wa habari ili wananchi waweze kufikiwa na taarifa hizo na kwenda sambamba na mfumo huo wa ukusanyaji mapato.

Kuhusiana na mabadiliko yaliyofanyiwa kazi ni pamoja na kupunguzwa kwa adhabu ya 20,000 na adhabu ya mara mbili ya kutofanya malipo baada ya siku saba na kuongezwa kwa siku 14 za malipo na ndani ya siku hizo mteja atakumbushwa mara mbili huku watumiaji wa mtandao wa simu wa VODACOM wakikumbushwa kufanya malipo na kampuni hiyo.

Mhandisi. Mkinga amesema mabadiliko hayo pia yamepunguza tozo ya siku kutoka shilingi 4500 hadi 2500 na tozo kwa saa ikibaki shilingi mia tano huku taarifa za wapi mteja alipaki zitabaki kuwa siri kwa usalama wa mfumo na watumiaji wake.

Pia Meneja wa TEHAMA kutoka TARURA Stanley Mlula amesema wamebadilisha mfumo wa ulipaji tozo zitabaki kama zilivyo na hiyo ni kwa malengo ya kuzuia kupotea kwa mapato kwa kuzuia malipo ya fedha mbichi (cash.) na kutumia mfumo wa malipo ya 'control number' ambapo wateja watalipa kwa simu na benki (NMB na CRDB.)

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Ilala Omary Kumbilamoto ameipongeza TARURA kwa kupitia changamoto hizo kwa kushirikiana na Serikali (TAMISEMI) na wanaamini mfumo huo utafanya kazi kwa mafanikio makubwa hasa katika ukusanyaji wa mapato.

Amesema ni muhimu kwa Wakala hiyo kuwashirikisha madiwani na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama katika masuala yanayohusu jamii kutokana na muunganiko muhimu na wa moja kwa moja wa viongozi hao na wananchi.


Meneja wa TEHAMA kutoka TARURA Stanley Mlula akitoa mada akati wa mkutano wa kuwajengea uwezo kamati ya ulinzi na usalama pamoja na madiwani juu ya matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji wa ushuru wa maegesho utakaoanza rasmi Desemba mosi mwaka huu.

Katibu Tawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Ilala Charangwa Selemani akifungua kikao hicho na kuwapongeza TARURA kwa kuwashirikisha viongozi hao katika mchakato huo muhimu wa ukusanyaji mapato ya Serikali.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Geofrey Mkinga akizungumza katika kikao hicho na kueleza kuwa mabadiliko yaliyofanywa na Serikali kwa kushirikiana na Wakala hiyo yana tija kwa wananchi wa hali ya chini, leo jijini Da es Salaam.




Matukio mbalimbali katika kikao hicho.





No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad