SHIRIKA LA POSTA, MRISHO MPOTO WAINGIA MAKUBALIANO YA KUTANGAZA BIDHAA NA HUDUMA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, November 25, 2021

SHIRIKA LA POSTA, MRISHO MPOTO WAINGIA MAKUBALIANO YA KUTANGAZA BIDHAA NA HUDUMA

SHIRIKA la Posta Tanzania limeingia makubaliano ya pamoja na msanii wa nyimbo za asili na Mshairi Mrisho Mpoto 'Mjomba' kwa lengo la kutangaza huduma na bidhaa za shirika hilo ambalo lipo katika mabadiliko makubwa ya utoaji huduma ndani na nje ya nchi kwa teknolojia ya hali ya juu.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla iliyoambatana na utiaji saini wa makubaliano hayo Posta masta mkuu Macrice Mbodo amesema,lengo la kuingia makubaliano hayo ni kulitangaza shirika hilo ambalo lipo katika mabadiliko makubwa na limekuwa shirika la kidigitali katika utoaji huduma.
''Makubaliano haya ni kwa ajili ya kulitangaza shirika letu la Umma ambalo kwa sasa ni shirika la kidigitali na sio shirika la barua kama wengi wanavyodhaani.... Makao makuu wa Posta Afrika yapo jijini Arusha hapa Tanzania hii nafasi adhimu kwetu kujifunza kupitia Posta zote Afrika, Haya ni mageuzi ya fasta na yenye tija kwa uchumi wa taifa na tunawahimiza wananchi kutumia huduma za Posta kama nchi nyingine wanavyofanya.'' Amesema.

Mbodo amesema, shirika hilo lina fursa nyingi ambazo jamii inatakiwa kuzifahamu na kuzitumia ikiwemo huduma ya duka mtandao ambayo huwezesha kuuza na kununua bidhaa kwa njia ya mtandao kote duniani.

''Posta ina miundombinu ya usafrishaji nchini na nje ya nchi tunasafirisha hadi samaki na dagaa kupeleka nje ya nchi tutumie fursa hii, pia kuna huduma za kifedha zinazotolewa katika shirika hili, huduma za pamoja (One Stop Centre) zinapatikana katika ofisi za Posta nchi nzima hivyo ni vyema wananchi wakatumia fursa hizo kupitia shirika hilo.'' Amesema.
Aidha amesema kuwa shirika hilo linaendelea kuimarika vyema na wanategemea kupokea ujumbe kutoka shirikisho la Posta duniani ambapo Tanzania ni mwanachama hai.

''Kupitia balozi mteule Mpoto, watanzania watapata fursa ya kulifahamu shirika la Posta  na huduma zinazotolewa kwa uaminifu na gharama nafuu kama nchi nyingine wanavyotumia na kuthamini mashirika yao ya Posta kama DHL ya Ujerumani na Royal Mail ya Uingereza ambalo pia lilitushirikisha katika kusafirisha kifimbo cha Malkia hadi hapa nchini, hivyo niwaombe watanzania wenzangu tuunge mkono juhudi za Serikali kupitia shirika hili.'' Amesema.

Kwa upande wake balozi mteule Mrisho Mpoto ameshukuru kwa kupewa nafasi hiyo na kuwashauri watanzania kupenda na kuthamini vitu vya nyumbani ili waheshimwe duniani na kukuza kipato na soko.

Mpoto amesema shirika la Posta ni  la  kidigitali, salama na wanamtandao mkubwa wa usafirishaji wa bidhaa ndani na nje ya nchi na kuahidi kuwafikia watanzania wengi na kuwafahamisha juu ya huduma na bidhaa za shirika hilo zenye uhakika na viwango vya kimataifa.
Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macrice Mbodo (kulia) pamoja na Balozi mpya wa Shirika la Posta Tanzania, Mshahiri Mrisho Mpoto wakisaini hati za makubaliano mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani)  katika hafla fupi ya kumtambulisha Balozi wa Posta, iliyofanyika kwenye makao makuu ya Shirika hilo, jijini Dar es salaam leo.
Balozi mpya wa Shirika la Posta Tanzania, Mshahiri Mrisho Mpoto (kushoto), akizungumza jambo mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye makao makuu ya Shirika hilo, jijini Dar es salaam leo.
Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macrice Mbodo akifafanua jambo katika mkutano na waandishi wa habari wakati wa hafla fupi ya kumtambulisha Balozi wa Posta, Mshahiri Mrisho Mpoto (kushoto), iliyofanyika kwenye makao makuu ya Shirika hilo, jijini Dar es salaam leo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad