RAIS
wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni amefanya ziara
kutembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR katika Stesheni ya
SGR jijini, Novemba 28, 2021.
Rais
wa Jamhuri ya Uganda yuko nchini Tanzania katika ziara ya kikazi ya
siku tatu kuanzia Novemba 27 – 28 Novemba 2021. Lengo la ziara hiyo ni
kuona maendeleo ya mradi huo wa kimkakati ambapo alipata fursa ya
kukagua jengo la Stesheni ya Dar es Salaam ambalo limejengwa kwa mfano
ya Madini ya Tanzania, madini ambayo yanapatika Tanzania pekee.
Akihutubia
katika ziara hiyo Mhe. Rais Museveni amesema kuwa amefurahishwa na
namna nchi ya Tanzania inavyosonga mbele kiuchumi katika kuboresha
miundombinu na kuongeza fursa za biashara na uwekezaji, jambo ambalo
limechangiwa na mwamko mkubwa ambao watanzania wameupata kwa kufanya
kazi na kukuza uchumi wa nchi.
Rais
Museveni ameongeza kuwa "Usafirishaji wa mizigo kwa njia ya treni ni
bora, rahisi na unaokoa muda zaidi kwa sababu treni ina uwezo wa
kusafirisha mzigo mkubwa kwa safari moja na hii itasaidia kukuza uchumi
wa nchi zetu za Afrika Mashariki."
Waziri
wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Makame Mbarawa amesema kuwa utekelezaji wa
mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa unakwenda kuziunganisha bandari ya Dar
es Salaam nchini Tanzania na bandari ya Port Bell nchini Uganda ambazo
ni muhimu katika uchumi wa nchi hizo mbili na Afrika Mashariki kupitia
Ziwa Victoria, kwa kufanya hivyo kutaharakisha zoezi la kupakia na
kupakua mizigo na kupunguza msongamano wa mizigo katika bandari hizo.
Waziri
Mbarawa amesema kuwa Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya reli
kwa kujenga reli mpya ya kisasa ili kuliongezea Shirika la Reli ufanisi
katika kubeba mizigo.
“Serikali
ya Tanzania inawekeza katika uboreshaji miundombinu ya zamani na
kujenga miundombinu mipya ya kisasa ili kuendana na uchumi mzuri kwa
nchi za Afrika Mashariki" ameongeza Waziri Makame Mbarawa.
Mkurugenzi
Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kadogosa wakati akitoa
taarifa ya maendeleo ya mradi wa SGR ameeleza kuwa kwa sasa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatekeleza mradi huo kwa awamu ya
kwanza Dar es Salaam – Mwanza yenye urefu wa Kilometa 1219 kwa njia kuu.
Pia
Ndugu Kadogosa ameongeza kuwa ujenzi wa reli ya kisasa utasaidia
kukuza uchumi na utaunganisha kibiashara nchi za Afrika Mashariki
kupitia bandari na ziwa Victoria kwa kuokoa muda wa safari na gharama za
usafirishaji hadi 40%.
“Usafirishaji
wa mizigo kwa njia ya Treni kwa kutumia treni za kisasa utarahisisha
zaidi na kuokoa muda, safari moja ya treni itakua na uwezo wa
kusafirisha Tani 10,000 kwa safari moja" amesema Ndugu Masanja Kadogosa.
Aidha,
Kadogosa amesema kuwa TRC imeweza kurejesha huduma ya usafirishaji wa
shehena ya mafuta kutoka Dar es Salaam hadi Kampala nchini Uganda
kupitia reli, pia TRC inaendelea na jitihada za kuboresha huduma za
usafiri wa reli kati ya Tanzania na Uganda kwa kushirikiana na Shirika
la Reli Uganda kwa lengo la kuzifaidhisha nchi ya Uganda na Tanzania
kupitia Bandari.
“Hivi
karibuni miezi miwili iliyopita tumeanza biashara ya mafuta, yanatoka
bandari ya Dar es Salaam yanapita ziwa Victoria na kufika Port Bell
nchini Uganda, na mpaka sasa tumeshapeleka matenki 72 ambayo ni sawa na
Lita Milioni 3,240,000, kwahiyo ni huduma ambayo ilipotea na
tumerudisha”
Kadogosa
amesema kuwa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kipande cha Dar es
Salaam – Morogoro umefika zaidi ya 95% , Morogoro – Makutupora ambao
umefika 75% pamoja na Isaka Mwanza ambao umefika 3.87%, huku vipande vya
Makutupora – Tabora na Tabora – Isaka vikiwa kwenye maandalizi kwa
ajili ya kuanza utekelezaji wake.
Rais
wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni (kulia) akipata
maelezo kuhusu maendeleo ya mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR
kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja
Kadogosa katika Stesheni ya SGR jijini Dar es Salaam, Novemba 28, 2021.
Rais
wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni (wa pili kulia)
akipata maelezo kuhusu jengo la stesheni ya SGR jijini Dar es Salaam
alipokuwa akikagua jengo hilo jijini Dar es Salaam, Novemba 28, 2021.
Rais
wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni (kulia) akipata
maelezo kuhusu eneo ambalo litatumika na abiria wakati wa kupanda na
kushuka katika treni za kisasa za SGR katika Stesheni ya SGR jijini Dar
es Salaam, Novemba 28, 2021.
No comments:
Post a Comment