HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, November 2, 2021

PUMA, AMEND WAMWAGA ZAWADI KWA WANAFUNZI JIJINI DODOMA

 



Mkuu wa Wilaya Dodoma Mjini, Jabir Shekimweri (kulia) akikabidhi kikombe cha ushindi mshindi wa wa kwanza kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chidachi, Veronica Suya baada ya mwanafunzi wa shule hiyo Joseph Thadei (kushoto) kuibuka mshindi wa mashindano ya kuchora picha zinaoonesha mambo ya usalama barabarani. Mashindano hayo yaliyoshirikisha wanafunzi shule mbalimbali za jiji hilo yaliendeshwa na Taasisi ya Amend kwa udhamini wa Kampuni ya Mafuta ya Puma. Mwanafunzi huyo amezawadiwa sh 500,000 na shule sh. mil. 4. Hafla hiyo imefanyika katika shule ya Msingi Kisasa jijini Dodoma Novemba 2,2021. Wa pili kulia ni Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Leonce Kaimukirwa Mwakilishi wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma.




Na Charles James, Michuzi TV-Dodoma

KATIKA kuhakikisha ajali za barabarani zinapungua, zaidi ya Wanafunzi 120,000 nchi nzima wamepatiwa mafunzo ya usalama barabarani Ili kuweza kutokomeza ajali hizo.

Mafunzo hayo ambayo yameendeshwa na Kampuni ya Mafuta ya Puma kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la AMEND yamewafikia wanafunzi hao katika Mikoa Mitano ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Geita, Ruvuma na Kilimanjaro pamoja na visiwani Zanzibar.

Akifunga mafunzo hayo jijini Dodoma leo, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri ameipongeza Kampuni ya Puma na AMEND kwa kuendesha mafunzo hayo ambayo anaamini yatachangia kupunguza ajali za barabarani ambazo wahanga wakubwa pia wamekuwa ni Wanafunzi.

DC Shekimweri amesema kuwa anatambua mbali ya kutolewa elimu ya barabarani, wameendesha shindano la mchoro wa usalama barabarani, na hivyo ameamua kuongeza zawadi kwa mshindi wa shindano hilo."Nitatoa Sh.100,000 na wengine naomba mchangie,walimu hawa ambao wanafundisha elimu ya usalama barabarani na kuwafundisha kuchora nao wapate motisha.

Katika mashindano hayo ya michoro, Mwanafunzi kutoka Shule ya Msingi Chidachi, Joseph Chidachi amejinyakulia kiasi cha Sh Laki Tano huku Shule yake ikipata Sh Milioni Nne huku Shule ya Kisasa ikishika nafasi ya pili na ya tatu.

" Niwapongeze sana Puma na AMEND jambo hili mlilolifanya ni kubwa na lenye manufaa makubwa kwa Taifa letu, elimu hii itawajengea uelewa vijana wetu juu ya usalama barabarani na hivyo kupunguza ajali nyingi ambazo zimekua zikileta vifo kwa wanafunzi wetu, walemavu na hata watembea kwa miguu wengine.

Nitumie fursa hii kuliagiza Jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani jijini Dodoma kushirikiana na Shule zetu kuendesha mafunzo kwa wanafunzi wetu na kuwapatia vifaa kwa ajili ya wanafunzi wanaosimama barabarani kuzuia magari wenzao wapite," Amesema DC Shekimweri.

Ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Samia kwa miundombinu ya barabara katika Jiji la Dodoma na hivi karibuni Sh.bilioni 300 zimetengwa kwa ajili ya miundombinu na wamepanga kujenga pia barabara za pande mbili ambazo zote zitazingatia watembea kwa miguu pamoja na alama za barabarani.

"Takwimu za watu wanaopata ajali za barabarani bado ni kubwa, nafikiri kuna haja ya kuongeza elimu ili kupunguza au kuondoa kabisa vifo vya watoto, wazee na wenye ulemavu.Nawaagiza Jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani jijini Dodoma kuongeza mafunzo kwa wanafunzi ambao wamekua wakisimama barabarani kuzuia magari ili wanafunzi kuvuka sambamba na kuwapatia vifaa.

" Tutaendelea kusimamia sheria ya usalama barabarani, nitoe rai kwa Jeshi la Polisi kuwa wakali kwa wanaovunja sheria za barabarani, haiwezekani mtu anatembea mwendo kasi sehemu ambayo kibao kinamuonesha kutembea mwendo mdogo, na Polisi mkimkamata mtu mara nyingi zaidi basi ikiwezwkana anyang'anywe leseni yake," amesema Shekimweri.

Ofisa Uhusiano wa Puma, Godluck Shirima akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Puma, Dominic Dhanah ameishukuru Serikali kwa namna ambavyo wametoa ushirikiano kwao wakati wa utekelezaji wa mafunzo hayo huku akiahidi kuwa wataendelea kutoa mafunzo hayo kwa wanafunzi lengo likiwa ni kutokomeza kabisa ajali za barabarani.

Amesema utoaji wa zawadi hizo unahitimisha mradi uliotekelezwa na Puma na Amend ambao ulihusisha mafunzo kuhusu usalama barabarani na uchoraji wa picha kwa shule za Kisasa, Ipagala B, Chidachi, Makole na Dodoma Mlimani ambapo wanafunzi wasiopungua 20,000 walipata mafunzo hayo.

“Huu mpango huu wa usalama barabarani ni mwendelezo wa kampeni ambayo ilizinduliwa rasmi miaka tisa iliyopita ambapo zaidi ya shule 100 zimefikiwana na wanafunzi zaidi ya 120,000 mikoa mbalimbali wamepata mafunzo hayo,”alisema.

Amesema kwa njia hiyo Puma Energy inaamini kuwa watoto watakuwa salama na kutakuwa na taifa lenye watu imara na wenye nguvu za kulitumikia taifa lao.

" Lengo letu kama kampuni ni kuongeza wigo ili kufikia shule nyingi zaidi nchi nzima kwa mwaka 2022, sisi kampuni ya Puma Energy tunaahidi kuendelea kuwekeza katika kampeni ya usalama barabarani kwa kushirikiana na serikali kupitia jeshi la Polisi ili kuokoa maisha ya watanzania,” Amesema Shirima.

Pia Mkaguzi Msaidizi wa Polisi ambaye amemwakilisha Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Leonce Kaimukirwa amesema wamefurahishwa na mafunzo ambayo yamekuwa yakitolewa na Amend kwa kushirikina na Kampuni ya Puma Energy Tanzania na kwamba Jeshi la Polisi limekuwa likitoa mafunzo ya usalama barabarani.

"Tumekuwa tukitoa elimu katika shule za msingi,shule za sekondari ,vyuoni pamoja na watumiaji vyombo vya moto wakiwemo waendesha bodaboda, tumekuwa tukielimisha wazazi kutopakia watoto wao kwenye bodaboda,tunawashauri wazazi wasikubali watoto kubebeshwa zaidi katika bodaboda,"amesema.

Amefafanua mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka na kuongeza kauli ya Jeshi la Polisi katika kuelekea Wiki ya Usalama Barabarani inasema Jali maisha yako,jali maisha ya wengine."Hivyo kwetu mafunzo haya ni muhimu sana , ni muhimu tukashirikiana kwa ajili kupunguza ajali."

Simon Kalolo ambaye ni Meneja Mkuu wa Shirika lisilo la kiserikali la Amend Tanzania, amesema wamekuwa wakitekeleza miradi mingi katika nchi zaidi ya 10 barani Afrika ikiwemo Tanzania.

"Moja ya mradi ambao tunautekeleza ni mradi wa elimu ya usalama barabarani, ajal bado ni changamoto, duniani watu zaidi ya 350,000 wanapoteza maisha na wengine zaidi ya milioni tatu wanabakiwa na ulemavu wa hivyo jitihada zinahitajika, mbali ya elimu pia kumefanyika mashindano ya michoroya usalama barabarani.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri akimkabidhi cheti na fedha Sh.500,000 Mwanafunzi Joseph Mtei wa Shule ya Msingi Chidachi ambaye ameshinda shindano la michoro ya usalama barabarani lililoendeshwa na Kampuni ya Puma na Shirika la AMEND.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri (wa kwanza kushoto) akiwa na Mwakilishi wa Kampuni ya Puma, Godluck Shirima (katikati) na Meneja wa Shirika la AMEND, Simon Kalolo(kulia) wakichagua picha za washindi wa shindano la picha za michoro ya usalama barabarani lililoendeshwa kwa wanafunzi wa Shule za Jiji la Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri akimkabidhi zawadi ya Sh 20,000 Mwanafunzi wa Shule ya Msingi kisasa ambaye alijibu swali ambalo aliuliza kwa wanafunzi hao.
Meneja Mkuu wa AMEND, Simon Kalolo akionesha Moja ya michoro iliyochorwa na wanafunzi wa Shule ya Msingi Kisasa katika shindano la michoro ya usalama barabarani.
Meneja Mkuu wa AMEND, Simon Kalolo akizungumza katika tukio la ufungaji mafunzo ya usalama barabarani kwa Shule za Msingi Dodoma. Mafunzo hayo yameendeshwa na AMEND na Kampuni ya Mafuta ya Puma.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi walioshinda shindano la michoro ya usalama barabarani pamoja na Walimu wao na viongozi wa Kampuni ya Puma na Shirika la AMEND.
Wawakilishi wa wanafunzi wa Shule mbalimbali za Jiji za Dodoma wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri wakati wa kufunga kwa mafunzo ya usalama barabarani yaliyoendeshwa na Kampuni ya Puma na Shirika la AMEND.
Mwanasheria na Mahusiano wa Puma, Goodluck Shirima akimkabidhi zawadi mshindi wa pili kutoka Shule ya Msingi Kisasa baada ya kushika nafasi hiyo kwenye shindano la michoro ya usalama barabarani Nchini.






















Matukio mbalimbali katika picha wakati wa utoaji wa zawadi kwa wanafunzi walioshinda shindano la michoro ya usalama barabarani lililoandaliwa na Kampuni ya Mafuta ya Puma na kwa kushirikiana na AMEND kwa shule za Mkoa wa Dodoma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad