MAKAMU WA RAIS AZUNGUMZA KATIKA MKUTANO WA BLOOMBERG - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 17, 2021

MAKAMU WA RAIS AZUNGUMZA KATIKA MKUTANO WA BLOOMBERG

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango leo Novemba 17,2021 ameshiriki Mkutano wa Jukwaa la Majadiliano ya Kiuchumi (Bloomberg New Economy Forum 2021 ) mkutano unaojadili masuala mbalimbali ikiwemo muelekeo mpya wa Kiuchumi baada ya athari za Uviko-19 pamoja na Mabadiliko Tabia nchi. Makamu wa Rais ameshiriki kama mtoa mada katika mjadala unaohusu Juhudi za Pamoja za Kuijenga Upya Jamii Baada ya Uviko19 kwa Kuepuka Hatari ya Kuongezeka kwa Tabaka baina ya Masikini na Matajiri.

Akizungumza katika mjadala huo Makamu wa Rais amesema ipo haja ya mataifa yalioendelea kutoa msaada wa haraka katika mapambano dhidi ya Uviko19 pamoja na ufufuaji uchumi kwa mataifa yanayoendelea hasa kusini mwa janga la Sahara.

Amesema katika mapambano dhidi ya Uviko19 nchi za Afrika, Tanzania ikiwemo zimepitia changamoto kubwa ikiwamo kuelemewa kwa mfumo wa utoaji huduma za afya kutokana na kutokuwepo kwa miundombinu na vifaa vya kutosha kupambana na janga hiyo. Makamu wa Rais amesema Uviko19 umeacha madhara kwa familia kupoteza wapendwa wao waliowategemea hivyo kuingiza familia nyingi katika umasikini. Aidha amesema Tanzania hutumia sekta ya utalii katika kuchangia Pato la Taifa hivyo kufungwa kwa mipaka na kusimama kwa biashara za kimataifa wakati wa janga la Uviko19 kumepelekea ukuaji wa uchumi kushuka.

Makamu wa Rais ameongeza kwamba katika dunia ya sasa ni muhimu kuwekeza katika Tehama itayorahisisha na kuharakisha namna ya ufanyaji kazi pamoja na upatikanaji wa huduma. Hivyo, ameyaasa mashirika ya fedha ya kimataifa kuja na mpango maalum wa kuziwezesha nchi za kusini mwa jangwa la sahara kuweza kufikia mapinduzi ya Tehama pamoja na upatikanaji wa chanjo.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amesema mataifa yalioendelea ni vyema kushirikiana na mataifa ya Afrika katika tafiti za maendeleo ikiwa ni pamoja na  kuhamishia baadhi ya viwanda ikiwemo vya Chanjo katika mataifa ya Afrika ili kutoa fursa ya waafrika kujifunza na kupata maarifa katika utengenezaji wa chanjo hizo. Amesema ni muhimu elimu ikaendelea kutolewa juu ya umuhimu wa chanjo zinazotolewa kukabiliana na Uviko19 ili kuondoa dhana potovu inayosambaa katika mitandao ya kijamii juu ya madhara ya chanjo hizo.

Mkutano wa Bloomberg unawakutanisha Viongozi wakuu wa serikali, wakuu wa makampuni na taasisi, wafanyabiashara wakubwa, wasomi kutoka sehemu mbalimbali duniani kwaajili ya kujadili namna ya kujenga uchumi endelevu na stahimilivu na kuhamasisha juhudi za pamoja za kupambana na Uviko19 pamoja na Mabadiliko ya tabia nchi.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango leo Novemba 17,2021 Akizungumza katika  Mkutano wa Jukwaa la Majadiliano ya Kiuchumi (Bloomberg New Economy Forum 2021 ) Makamu wa Rais ameshiriki kama mtoa mada katika mjadala unaohusu Juhudi za Pamoja za Kuijenga Upya Jamii Baada ya Uviko19 kwa Kuepuka Hatari ya Kuongezeka kwa Tabaka baina ya Masikini na Matajiri. Novemba 17,2021


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad