HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, November 11, 2021

JIJI LA DODOMA LATOA MIKOPO YA VIKUNDI

 


Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais-Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kutekeleza takwa la kisheria kuvikopesha vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu shilingi 1,039,050,000 kutoka mapato ya ndani ya halmashauri.

Waziri Mwalimu alisema hayo alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi wa Jiji la Dodoma waliojitokeza katika bustani ya Nyerere square kabla ya tukio la kukabidhi mfano wa hundi ya shilingi 1,039,050,000 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

“Niwashukuru na kuwapongeza sana Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma chini ya Mstahiki Meya, Prof. Davis Mwamfupe. Pongezi hizi ziende hadi kwa watendaji wake chini ya Mkurugenzi, Joseph Mafuru kwa kutekeleza kikamilifu maelekezo ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mama Samia Suluhu Hassan. Si kikopo kiduchu, Jiji la Dodoma mpo juu, hongereni Dodoma!” alisema Waziri Ummy kwa furaha kubwa.

Aidha, Waziri huyo alilitaka jiji hilo kuendelea kutoa mikopo mikubwa wa vikundi vya kiuchumi. “Ni matumaini yangu kuwa Jiji la Dodoma haitakuwa mara ya mwisho kutoa mikopo mikubwa. Tunataka kuona mikopo mikubwa, wakopaji wenye mawazo mazuri yanayotekelezeka wapewe mikopo hata milioni 100 na kuendelea. Lakini pia msiache kutoa mikopo midogo kwa vikundi. Najua kuna vikundi ambavyo mnatakiwa kuanza navyo kidogo kidogo kisha vinaenda vinakuwa” alisema Waziri Mwalimu.

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe alisema kuwa Halmashauri hiyo haijawahi kuwa na upungufu wa fedha. Alisema kuwa upungufu unaoikabili halmashauri hiyo ni vikundi kwenda kukopa.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alisema kuwa kwa kipindi cha robo ya kwanza 2021/2022 jumla ya shilingi 1,039,050,000 zimekopeshwa kwa vikundi 48. Alisema vikundi vya wanawake 19, vijana 19 na watu wenye ulemavu 10. Kati ya fedha hizo shilingi 238,514,365 ni mgao wa robo ya kwanza na shilingi 800,535,635 ni fedha zilizovuka mwaka, aliongeza.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad