HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, October 18, 2021

Zaidi ya bilioni 6 kujenga miradi ya elimu na afya mkoani Njombe

 


Na Amiri Kilagalila, Njombe

Mkuu wa mkoa wa Njombe Mhandisi Marwa Rubirya amewaagiza wakurugenzi wa halmasahuri zote za mkoa huo kuhakikisha fedha za miradi ya maendeleo zinawafikia wafanyabiashara wa ndani ya mkoa kwa kununua vifaa vya ujenzi kwa mawakala waliopo ndani ya mkoa.

Ametoa agizo hilo wakati wa kikao maalum cha maelekezo ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia fedha ya mkopo wa shilingi bilioni sita na milioni mia tano na themanini katika mgao wa fedha hiyo kati ya trilioni 1.3 wa kitaifa kwa ajili ya kampeni ya maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya Uviko 19 kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya mji wa Njombe

“Vifaa vyote vya ujenzi iwe ni saruji,mabati au iwe nondo vinunuliwe kutoka kwa wafanyabiashara na mawakala tulio nao mkoani.Na kama italazimika kununua nje ya mkoa kibali hicho ni lazima tuhakikishe kinapatikana kwa katibu tawala wa mkoa kwasababu fedha hizi tunataka zionekane kwa kila mwananchi aliyeoko mkoa wa Njombe”alisema Rubirya

Awali bwana Edward Mwakipesile katibu tawala msaidizi idara ya mipango na uratibu mkoa wa Njombe,amesema wamepokea shilingi bilioni 6 na milioni 580 fedha ya mkopo wa trilioni 1.3 kwa ajili ya kampeni ya maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya Uviko 19,fedha ambayo imeelekezwa katika maeneo mbalimbali kutatua changamoto zikiwemo za afya na elimu.

“Tumepata fedha katika maeneo saba,eneo la kwanza ni kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madaras 192 katika shule za sekondari,eneo la pili ni kwa ajili ya ujenzi wa vituo shikizi 15,ujenzi wa majengo ya huduma za dharula,ujenzi wa vyumba vya wagonjwa mahututi,ununuzi wa mashine za mionzi pamoja na ujenzi wa nyumba za watumishi”alisema Edward Mwakipesile

Agnetha Mpangile ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe na Deogratius Sunday ni mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa wameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuwafikishia fedha hizo huku wakishauri kukaa pamoja na wafanyabiashara wa ndani ya mkoa ili kuzungumza nao juu ya ujenzi wa miradi ya maendeleo na kuwaeleza gharama za vifaa zinazopendekezwa ili kujenga makubaliano yatakayoondoa sababu za serikali kununua vifaa vya ujenzi nje ya mkoa.

Mkuu wa mkoa wa Njombe Mhandisi Marwa Rubirya akizungumza na watumishi wa halmashauri za mkoa huo wakati wa kikao maalum cha maelekezo ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia fedha ya mkopo wa shilingi bilioni sita na milioni mia tano na themanini katika mgao wa fedha hiyo kati ya trilioni 1.3 wa kitaifa kwa ajili ya kampeni ya maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya Uviko 19

Baadhi ya watumishi wa mkoa wa Njombe wakati wakisikiliza maelekezo ya mkuu wa mkoa juu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad