Watu 160 wamefanyiwa upimaji wa magonjwa ya moyo bila malipo Geita - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 1, 2021

Watu 160 wamefanyiwa upimaji wa magonjwa ya moyo bila malipo Geita

Na Mwandishi Maalum

Watu 160 wamefanyiwa upimaji wa magonjwa ya moyo bila malipo wakati wa upimaji ulioandaliwa na chama cha Madaktari Tanzania (MAT) uliofanyika katika viwanja vya Hospitali ya Mkoa wa Geita na kumalizika jana.

Upimaji huo wa siku tatu ulifanywa na wataalam wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kutoa rufaa kwa wagonjwa 14 Waliobainika kuwa na magonjwa mbalimbali ya moyo.

Akizungumza wakati wa upimaji huo Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Theophylly Mushi alisema upimaji uliofanyika ni wa kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi na mabadiliko ya ndani ya muundo wa kuta za moyo unaosababishwa na shinikizo la damu (Echocardioghraphy – ECHO), kuchunguza jinsi umeme wa moyo unavyofanya kazi (Electrocardiography – ECG) pamoja na shinikizo la damu (BP).

“Kati ya watu 160 tuliowaona, watu 118 (`73.5%) walikuwa na matatizo mbalimbali ya moyo, watu 105 (65.6%) walikutwa na shinikizo la damu, watu 5 (3.1%) walikuwa na shida ya valvu, watu 6 (3.7%) walikutwa kuta zao za moyo zikiwa zimetanuka (dilated cardiomyopathy), watu 2 walikuwa na tundu kwenye moyo na watu 2 walihitaji upasuaji mkubwa wa moyo kuziba matundu ya moyo”,

“Hata hivyo walio kuwa na shida ya umeme wa moyo walikuwa watu 3, ambao kati yao wawili wanahitaji kuwekewa betri ya moyo huduma inayotolewa katika taasisi yetu. Wagonjwa tuliowaona wengi wao hawakuwa wanajijua kama wanamatatizo mbalimbali katika mioyo yao”, alisema Dkt. Mushi

Aidha Dkt. Mushi alisema kuwa sambamba na upimaji huo, Taasisi ilitoa elimu ya afya ya moyo, namna ya kuzuia magonjwa ya moyo pamoja na Lishe bora jambo ambalo lilifurahiwa na wananchi wengi kwani elimu hiyo hawakuwahi kuipata.

Kwa upande wake mwananchi aliyepata huduma katika banda la JKCI Zalphia Mzinga amewashukuru wataalam wa JKCI kwa kugundua tatizo alilokua nalo kwa muda mrefu kwani alikua akizimia mara kwa mara bila ya kujua kama anasumbuliwa na tatizo la moyo.

“Nimekua nikidondoka mara kwa mara bila kujua kama mapigo yangu ya moyo yapo chini, leo hii nimefika katika banda la JKCI na kufanyiwa uchunguzi ambao ulionyesha mapigo yangu yanapiga 28 kwa dakika nikapewa dawa, ushauri na kutakiwa kufika Taasisi ya Moyo kwa ajili ya kuwekewa kifaa ambacho kitaongeza mapigo yangu ya moyo”,

“Kwa bahati mbaya wakati naendelea na huduma za matibabu katika mabanda mengine ile hali ya kudondoka na kupoteza fahamu ikanitokea tana na kupata huduma ya kwanza, sasa nimelazwa hapa Hospitali nasubiria rufaa ili niweze kupelekwa JKCI kwa ajili ya kuwekewa pacemaker” alisema Zalphia

Naye mwananchi kutoa mkoa wa Kagera Helena Christofa aliyetumia fursa ya kupata huduma za matibabu baada ya kusikia kuwa kuna madaktari mabingwa wanatoa huduma katika mkoa wa Geita, amewapongeza madaktari wa JKCI kwa kutumia muda mrefu kuwafanyia wananchi uchunguzi wa kina ili kuweza kupata majibu yanayoridhisha.

“Kwakweli nimekua nikienda hospitali kufanyiwa vipimo mbalimbali lakini sijawai ona madaktari kama hawa wa JKCI wanaotumia muda wao mwingi kuhakikisha kuwa majibu wanayoyatoa ni ya uhakika, nimeridhika na majibu niliyopewa, sasa naenda kuwa balozi mzuri wa namna ya kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza”,

Katika upimaji huo kampuni za uagizaji na usambazaji wa dawa za binadamu za Menarine, Kasmedics, SunPharma na Emcure zilitoa dawa bila malipo kwa wananchi waliokuta na matatizo ya moyo, kisukari na shinikizo la damu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad