HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, October 27, 2021

WANAFUNZI 15, 261 WAPANGIWA MIKOPO YA TZS 37.9 BILIONI AWAMU YA TATU

 

 



BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha ya Awamu ya Tatu yenye wanafunzi 15,261 wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 37.9 bilioni kwa mwaka wa masomo 2021/2022 unaoanza wiki hii.

Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo HESLB Dkt. Veronica Nyahende amesema kuwa orodha hiyo iliyotolewa leo Jumanne (Oktoba 26, 2021) inafanya jumla ya wanafunzi wapya wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo kufikia 60,356 yenye thamani ya TZS 157.3 Bilioni.

Dkt. Nyahende ameongeza kuwa HESLB tayari imeanza kupeleka fedha za wanafunzi waliopangiwa mikopo kwa awamu zote tatu katika vyuo mbalimbali na kuwataka wanafunzi kupata taarifa za kina katika akaunti walizotumia kuomba mkopo maarufu kama SIPA (Student’s Individual Permanent Account) ili kujiandaa kwenda vyuoni kwa ajili ya kujisajili.

Kuhusu kutangazwa kwa orodha ya Awamu ya Nne, Dkt. Nyahende amesema itatolewa siku chache zijazo baada ya kukamilisha uchambuzi wa maombi unaoendelea na kuwataka waombaji mikopo kutembelea akaunti zao za SIPA kupata taarifa kuhusu maombi yao.

“Orodha hii ya tatu inajumuisha wanafunzi wenye sifa zikiwemo kuwa wahitaji, wameomba kwa usahihi na wamekamilisha taratibu za udahili wa chuo kimoja. Tunakamilisha uchambuzi wa maombi mengine na tutatoa orodha ya ya awamu ya nne siku chache zijazo,” amesema Dkt. Nyahende.

Dkt. Nyahende amesema Serikali imetenga TZS 570 Bilioni kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi 160,000. Kati yao, wanafunzi 70,000 watakuwa ni wanufaika wa mwaka wa kwanza na wanafunzi zaidi ya 90,000 ni wale wanaoendelea na masomo baada ya kufaulu mitihani yao ya mwaka.

Dkt. Nyahende amesema HESLB imeshapokea fedha na kukamilisha taratibu zote kwa ajili ya malipo ya wanafunzi na fedha za awamu zote tatu zimeanza kutumwa vyuoni.

“Serikali imeshatupatia fedha na tumeanza kuzipeleka vyuoni … lengo letu ni kuhakikisha wanafunzi wanaopangiwa wanazikuta fedha vyuoni ambako watajisajili na kupokea fedha ili watimize ndoto zao,” amesema Dkt Nyahende.

Aidha Dkt. Nyahende aliwataka waombaji wa mikopo kuwa watulivu wakati mchakato wa upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa kwa awamu inayofuata ukiendelea.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad