HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 28, 2021

WAFUGAJI WAKEMEWA KUWASHAWISHI WATOTO WAO WAFELI ILI WAOLEWE AU WAKACHUNGE

 


Na Joseph Lyimo
MIONGONI mwa haki za mtoto ni kupatiwa elimu, ila bado kuna changamoto ya baadhi ya wazazi na walezi wa jamii ya kifugaji hawakubaliani na jambo hilo.

Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za dini, watu binafsi na jamii kwa ujumla wamekuwa wakipaza sauti katika kusisistiza watoto wapare elimu bila kubagua ni wakike au wakiume.

Miongoni mwa wazazi na walezi wa jamii ya kifugaji bado baadhi yao wana mtazamo hasi katika kuhakikisha watoto wa jamii hiyo wanapata elimu hivyo kusababisha kuweka vikwazo mbalimbali.

Baadhi ya wazazi na walezi wa jamii ya kifugaji wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, bado wana tabia ya kuwashawishi watoto wao wafanye vibaya katika mitihani ili wapate nafasi ya kuolewa wakiwa wadogo au kuchunga mifugo.

Mkazi wa Kata ya Naberera, Yohana Yamat amesema kitendo cha mzazi au mlezi kumfundisha mtoto wake mbinu chafu ili asifaulu masomo yake ni jambo baya.

"Unapomwambia mtoto wako achore nyoka au aandike madudu kwenye karatasi ya mtihani ili asifaulu ni kitendo kibaya mno," amesema.

Amesema wataalamu mbalimbali wa miaka inayo ikiwemo walimu, madaktari na wengineo watakuwa wachache miaka ijayo kutokana na jamii kutosomesha watoto wao hivyo wanapaswa kubadilika.

Mkazi wa Kata ya Terrat, Njani John anasema bado wazazi wachache wanamtazamo wa kudharau elimu kutokana na wao kutoipata kwani walikuwa wanachunga mifugo nakukosa fursa hiyo.

"Kutokana na wao kuikosa elimu bado hawaoni umuhimu wake zaidi yakutaka watoto wao nao wakose hivyo wantamani wawaozeshe wakiwa wadogo wapate mifugo au wakiume wakachunge ng'ombe," amesema.

Amesema hawatarajii kuona suala hilo linatokea mwaka huu wanafunzi watakapofanya mtihani wa darasa la nne na kuhitimu darasa la saba.

Mmoja kati ya viongozi wa kimila wa jamii hiyo Isack Saibul anasema japokuwa serikali na mashirika binafsi yanakemea kitendo hicho bado wazazi wanaendelea kuwafundisha watoto wao tabia hiyo mbaya.

Ameeleza kuwa jamii ya kifugaji hivi sasa imeelimika tofauti na awali hivyo wanawaunga mkono watoto wao wasome ila wapo baadhi yao wachache wanaokwamisha hilo.

"Tunaendelea kuwashawishi wazazi waachane na mtindo huo kwani mtoto akisoma na kuhitimu masomo yake ataolewa tuu na mzazi atapata ng'ombe wengi zaidi ya hizo 10 anazopewa akimuozesha akiwa bado mdogo," amesema.

Kaimu mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Mbaraka Alhaji Batenga, anakemea kitendo hicho kwa kuwataka wazazi na walezi kusomesha watoto wao na kuachana na mtindo huo wa kuwafelisha masomo yao.

Batenga amesema bado wapo wazazi hadi leo wanawashawishi watoto wao wafanye vibaya kwenye mitihani ili wasifaulu jambo ambalo siyo zuri.

"Mzazi unadiriki kumshawishi mtoto wako afanye vibaya kwenye mitihani ulimpeleka shuleni ya nini? kwa kuogopa kuwa utakamatwa kwakuwa hukumpeleka mtoto shuleni ili asome?" amehoji Batenga.

Amesema jambo hilo linasikitisha  na lipo kwenye jamii za kifugaji, hivyo amewataka kulifanyia kazi na kuchukua hatua kwa wazazi na walezi ambao wanawashawishi watoto wao wafanye vibaya kwenye mitihani na akifanya vizuri kwenye mitihani mtoto huyo anaenda kuadhibiwa.

"Serikali ya awamu ya sita haitavumilia vitendo vya namna hiyo kwa sababu inafanya kila juhudi inayowezekana kuboresha mazingira na miundombinu ya shule ili watoto wasome vizuri lakini baadhi ya wazazi wanawapotosha watoto wafanye vibaya darasani," anasema.

Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amesema ni kosa kwa jamii kufanya hivyo ila serikali, wawakilishi wa wananchi na jamii kwa ujumla wataungana kuendelea kutoa hamasa kwa wananchi ili kuhakikisha kwamba watoto wote wakike na wakiume watapewa fursa sawa ya kupelekwa shuleni.

Amesema matukio ya kuwarudisha nyuma wanafunzi ni kupoteza ndoto zao hivyo watoto wanapaswa kulindwa ili mtoto wa kike apate elimu, siyo ya msingi pekee ila kuendelea sekondari hadi vyuo vikuu.

"Nia yetu ni kuwa na wasichana wa jamii ya kifugaji ambao watakuwa na shahada zao moja au mbili na wao waweze kutoa mchango kwa Taifa letu hata kwa familia wanazotoka hiyo ndiyo dhamira na lengo tulilonalo kwa jamii ya wafugaji," amesema Ole Sendeka.

Amesema kuwa wazazi wanaofanya hivyo wabadilike kifkra na kimtazamo waelewe dunia inaelekea wapi na mahitaji halali ya watoto wakike na wakiume.

Ofisa elimu ya msingi wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Silvanus Tairo amesema kila mara wamekuwa wakikemea kitendo hicho kinachofanywa na baadhi ya wazazi wa jamii hiyo.

Tairo amesema wamekuwa wanakutana na jamii kwa ujumla, viongozi wa mila, viongozi wa vijiji na vitongoji ili kusaidiana kukomesha tabia hiyo mbaya.

Katibu mkuu wa shirika la Elimisha Simanjiro Organization (ESO) Lowassa Edward Lekor anasema kuanzishwa kwa kampeni niache nisome ni ili kupambana na mimba za utotoni kwa mtoto wa kike katika kuhakikisha wanawake wawe katika mazingira wezeshi ya kusoma pasipo na changamoto wala vikwazo na kutimiza ndoto zao .

Lowassa amesema watoto wakike wa jamij ya wafugaji wanapswa kwenda shuleni hivyo kampeni ya niache nisome ni sauti ambayo itawafanya mabinti hao watamani kusoma ili waweze kusimama na kufanikisha ndoto zao.

Amesema shirika limelenga kuelimisha jamii ili kuwasomesha, kuwafuatilia na kuwasaidia watoto wa jinsia zote waweze kufikia ndoto zao kwa ustawi wa elimu ya Tanzania.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara, Merrisone Mwakyoma hivi karibuni ameeleza kuwa wanaendelea kutoa elimu kwa jamii ya eneo hilo kuwapa watoto wao haki zao za msingi.

Kamanda Mwakyoma amesema sheria zipo na zitatumika kwa wale wote ambao kwa namna moja au nyingine itathibitika kuwa wanakwamisha watoto wasisome ipasavyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad