Na Said Mwishehe,Michuzi TV - Dodoma
NI Wiki ya AZAKI! Hivyo ndivyo unavyowezea kuelezea wiki hiyo ambayo imeanza leo Oktoba 23 hadi Oktoba 28 mwaka huu Mjini Dodoma ambapo viongozi kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za umma na binafsi wamekutana kujadili na kuweka mikakati ya namna Bora kuhakikisha AZAKI zinashiriki kikamilifu kuchagiza uchumi wa Taifa la Tanzania.
Katika Wiki ya AZAKI inayokwenda na kauli mbiu inayosema AZAKI na Maendeleo imeanza mapema leo kwa wadau mbalimbali kushiriki matembezi yaliyoanzia Shule ya Sekondari Dodoma na kumalizikia viwanja vya Ukumbi wa Jakaya Kikwete.
Wadau hao kutoka kwenye AZAKI baadhi yao walikuwa wamebeba mabango yenye jumbe mbalimbali na mengi kati yao yalikuwa yakielezea namna mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ambavyo yamejipanga kushiriki Katika kuleta maendeleo ikiwa ni sehemu ya kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan aliyedhamiria kuboresha hali ya uchumi wa watanzania.
Kwa kukumbusha tu Wiki ya AZAKI ni jukwaa pekee nchini linaloleta kwa pamoja wadau wakuu wa maendeleo ikiwemo serikali, sekta binafsi na Asasi za kiraia pamoja na wananchi kwa lengo la kujadili masuala yanayohusu ustawi wa nchi na Maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Wakati wa matembezi hayo baadhi ya washiriki wameiambia Michuzi TV na Michuzi Blog kwamba wameshiriki kwenye Wiki ya AZAKI mwaka huu kwa kutambua mchango wao Katika kuleta maendeleo kwa kutoa elimu inayowesesha kufahamu shughuli wanazofanya ambazo kimsingi ni kusaidia kupaza sauti na kuibua changamoto zikitatuliwa nchi inaendelea kupiga hatua.
No comments:
Post a Comment