HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 28, 2021

TAKUKURU MANYARA YAONYA MATAPELI WA VIWANJA

 

Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari.

Na Mwandishi wetu, Babati
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoani Manyara, wamewataka wananchi wa eneo hilo kuepuka utapeli wa viwanja kwenye eneo la Maisaka Kati maarufu kama makatanini hivyo wakitaka viwanja wafike kwenye ofisi za halmashauri ya Mji wa Babati.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake wakati akisoma taarifa ya kipindi cha miezi mitatu ya tangu mwezi Julai hadi Septemba amesema wananchi wachukue tahadhari ili kuwaepuka matapeli hao.

Makungu amesema wamekuwa wakipokea malalamiko kadhaa ya baadhi ya kampuni zinazojiita za udalali zikilalamikiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kupitia mradi wa viwanja vilivyopimwa na halmashauriya mji vikiwemo vitalu RR na TT.

Amesema kampuni nyingi zimekuwa zikiwalaghai wananchi kuwa zimekasimiwa mamlaka ya kuuza viwanja hivyo na kwa njia hiyo kujipatia fedha nyingi kwa kuuza viwanja kuliko bei halali.

“Imebainika kuwa baada ya kulipa fedha kwa madalali hao, wananchi waliotapeliwa fedha zao huelekezwa kwenda ofisi za halmashauri ya mji kwa ajili ya kukamillisha taratibu za kupatiwa hati, lakini wanapofika kwenye ofisi hizo hugundua kuwa wametapeliwa,” amesema Makungu.

Hata hivyo, amesema kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita elimu kwa umma imetolewa kwa jumla ya semina 40 zilizoendeshwa kwa makundi tofauti ili kuhamasisha jamii kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa.

Amesema jumla ya mikutano 24 ilifanyika ikiwa na madhumuni ya kuelezea athari za rushwa na jinsi ya kupambana nayo ambapo jumla ya klabu 35 za wapinga rushwa katika shule za sekondari zilitembelewa kwa lengo la kuziimarisha na kupatiwa mafunzo na vipindi tisa vya redio vyenye maudhui ya mapambano dhidi ya rushwa na ofisi ilishiriki na kufanya onyesho moja.

“Ndugu wanahabari, katika kipindi cha miezi mitatu cha Oktoba hadi Desemba mwaka huu tutaendelea na zoezi la kudumu la ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradiya maendeleo ili kuhakikisha kuwa inaakisi thamani ya fedha iliyopangwa,” amesema Makungu.

Ametoa rai kwa wana Manyara kuendelea kutoa taarifa za rushwa kwa kupitia namba zao za dharura 113 au kwa kufika ofisi zao zilizo karibu nao kuunga mkono kauli mbiu isemayo “Kupambana na rushwa ni jukumu langu- Kazi Iendelee.”

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad