HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 15, 2021

SHIRIKA LA WATERAID WATOA VITUO 12 VYA KUNAWIA MIKONO DAR


Mganga Mkuu Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume akiwakabidhi maafisa afya wa mkoa wa Dar es Salaam vituo vya kunawia mikono 12 ikiwa ni kuadhimisha siku ya unawaji mikono duniani.MGANGA Mkuu Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume amesema kunawa mikono kwa usahihi kutasaidia kuepusha vifo vinavyotokana na magonjwa ya milipuko kama kuhara na kipindipundu  kwa asilimia 35 huku pia ukipunguza vifo vitokanavyo na maambukizi ya magonjwa ya mfumo wa hewa kwa asilimia 32.

Dk. Mfaume ameyasema hayo leo Oktoba 15, 2021  jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya siku ya kunawa mikoni yaliyoandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la WaterAid kwa kushirikiana na The Foreign, Commonwealth & Development Office (FCDO) na Unileve.

Katika maadhimisho hayo, WaterAid  wamekabidhi vituo 12 vya kunawia mikono vyenye thamani ya Sh.milioni 144 kwa hospitali ya Mwananyamala, Mnazi Mmoja, Temeke, Kituo cha Magufuli, shule ya Msingi Malamba mawili na Msasani, ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Kituo cha Mabasi cha Simu 200 kama sehemu ya kuadhimisha siku ya unawaji mikono duniani ambayo ufanyika Oktoba 15, ya kila mwaka.

Amesema katika kuhakikisha watu wanakuwa salama,  serikali itaendelea kuongeza nguvu katika unawaji sahihi wa mikono haki ambayo ikizingatiwa itasaidia kuepuka vifo vya magonjwa yanayoambukiza kwa zaidi ya asilimia 67.

"Tunawaasa watu kuzingatia umuhimu wa kunawa mikono pindi tu wanapotoka chooni, ama kufanya kitu chochote kinachoashiria uchafu,  kwani tukifanikiwa katika suala hili la kunawa mokoni tutaweza kushinda vita hii ya magonjwa ya mlipuko na yanayoambukiza," amesema Dk. Mfaume 

Pia Dkt,  Mfaume amesema kwa mujibu wa Shirika la afya duniani (WHO) katika gramu moja ya kinyesi kunauwezano wa kubeba zaidi ya virusi milioni kumi, hivyo kama mtu hata nawa mikono kwa usahihi basi kun uwezekano mkubwa wa vijidudu kusambaa mwilini na hata kumuambukiza mtu mwingine maradhi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkaazi wa WaterAid Tanzania,  Anna Mzinga amesema wametoa msaada wa vituo hivyo ikiwa ni jitihada za kuunga mkono juhudi za Serikali kusaidia watanzania kunawa mikono ili kupambana na magonjwa ya mbali mbali ya kuambukiza ikiwemo UVIKO 19.

Mzinga amesema, pasipo huduma sahihi za maji, usafi wa mazingira na vifaa vya kunawia mikono katika makazi yetu, mashule, vituo vya kutolea huduma za Afya na taasisi nyingine basi mazingira yetu yatakuwa ni vyanzo vya magonjwa na kuacha jamii ikiwa katika hatari ya kupata milipuko ya magonjwa ya kuambukiza na kuingia gharama kubwa za matibabu na kupoteza nguvu ya uzalishaji.

“Ukiondoa afua nyingine, wote ni mashahidi namna unawaji wa mikono umeongezeka nchini kwa kila sehemu ya biashara, taasisi na makazi kuweka vifaa vya kunawia maji na sabuni. Hivi sasa tunaona kama taifa jinsi ambavyo tulivyofanikiwa kupambana na ugonjwa wa UVIKO 19 kupitia unawaji wa mikono.” Amesema Mzinga.

Aidha, Mzinga ametoa wito kwa Serikali kutoa kipaumbele kwenye miundombinu ya usafi wa mikono katika vituo 
vya huduma za afya, shuleni na kwenye maeneo ya umma, halikadhalika, miradi ya kampeni ya tabia ya usafi huku pia akiomba  mashirika yasiyo ya kiserikali kuendelea 
na kuongeza uwekezaji katika usafi wa mikono kama jambo muhimu na linaloendelea ili  kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

“Serikali, wadau wa maendeleo, na wafanyabiashara watenge fedha ya kutosha kwenye masuala ya usafi wa mikono kuwalinda watanzania mbali na magonjwa ya 
kuambukiza na yale ya mlipuko.” Amesisitiza Mzinga

Nae Enezael Ayo, Afisa Afya wa mkoa wa Dar es Salaam, amesema kumekuwa na ongezeko la unawaji mikono katika ngazi zote za kijamii na maeneo ya utoaji wa huduma za jamii jambo ambalo linaonesha elimu ya unawaji mikono imekuwa ikizidi kueleweka na kuongezeka siku hadi siku

Amesema awali ni watoa huduma pekee ndio walikuwa wakinawa mikono baada ya kumaliza kutoa huduma lakini sasa hata hata wateja wamekuwa wakinawa mikono pindi tu wamalizapo kupewa huduma jambao ambali litasaidia kupunguza maambukizi.

Katika maeneo mengi ya biashara asilimia 79.5 yameonekana kuwa na vifaa vya unawaji mikono kwa maji tiririka  na sabuni

"Kumekuwa na ongezeko la unawaji mikono katika ngazi zote za kijamii na maeneo ya utoaji wa huduma za jamii jambo ambalo linaonesha elimu ya unawaji mikono imekuwa ikizidi kueleweka na kuongezeka siku hadi siku." amesema

Aidha ameongeza kuwa, bado kuna muamko mdogo wa unawaji  mikono katika jamii, jamii bado inahitaji elimu endelevu ili kujua umuhimu wa kunawa mikono na kuongeza kuwa pia kumekuwa na uharibifu wa miundombinu ya unawaji mikono katika maeneo ya Umma kama vile sokoni, mashuleni na maeneo ya burudani kwa vile vifaa vinavyowekwa kwa ajili ya kinawia mikono kuibiwa ama kuaribiwa.
Mganga Mkuu Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume akifungua kituo kimojawapo ya 12 vya kunawia mikono vilivyotolewa na Shirika la Water Aid katika Mkoa wa Dar es Salaam. Ikiwa ni kuadhimisha siku ya Kunawa mikono ambayo hufanyika kila mwaka ifikapo Oktoba 15.


Viongozi mbalimbali wakinawa mikono wakati wa kuadhimisha siku ya kunawa mikono ambayo hufanyika kila mwaka ifikapo Oktoba 15.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Rashid Mfaume akizungumz wakati wa kuadhimisha siku ya kunawa mikono ambayo hufanyika kila mwaka ifikapo Oktoba 15. Maadhimisho hayo yameadhimishwa na shirika la Water Aid katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam leo pia wametoa msaada vituo 12 vya kunawia mikono vyenye thamani ya Sh.milioni 144.

Watoto wakiwa katika maadhimisho ya siku ya kunawa Mikono katika hospitali ya Mwanananyamala leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika Water Aid Tanzania, Anna Mzinga akizungumza wakati wa kuadhimisha siku ya Kunawa mikono duniani ikiwa Shirika la Water Aid wameadhimisha siku hiyo kwa katika hospitali ya Mwananyamala pia kutoa msaada katika vituo 12 vya kunawia mikono katika mkoa wa Dar es Salaam.
Mkufunzi akitoa maelekezo na hatua za kunawa mikono ili kujikinga na magonjwa ya Mlipuko.
Wanafunzi wakiigiza mbele ya hadhara wakati wa maadhimisho ya siku ya kunawa mikono duniani ambayo hufanyika kila mwaka ifikapo Oktoba 15.
Baadhi ya wadau wa afya na Water Aid wakiwa katika Maadhimisho ya siku ya kunawa mikono duniani ambayo hufanyika kila mwaka ifikapo Oktoba 15.

Wanafunzi wakitumbuiza ngonjera kuhusu siku ya kunawa mikono.
Picha ya pamoja.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad