MBUNGE JAPHARY AWATAKA WANA RORYA WA MIRERANI WASISAHAU NYUMBANI KWAO - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, October 12, 2021

MBUNGE JAPHARY AWATAKA WANA RORYA WA MIRERANI WASISAHAU NYUMBANI KWAO

Na Mwandishi wetu, Mirerani

MBUNGE wa Jimbo la Rorya Mkoani Mara, Japhary Chege Wambura amewataka wananchi wenye asili ya Jimbo la Rorya wanaoishi Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wasisahau nyumbani walipotoka kwa kufanikisha maendeleo mbalimbali.

Japhary ameyasema hayo kwenye ukumbi wa Kazamoyo Inn (Kwa Luka) Kata ya Endiamtu Mji mdogo wa Mirerani, wakati akizungumza na wananchi wenye asili ya Rorya juu ya kurudisha nyumbani kidogo wanachopata kwa kufanikisha maendeleo.

Amesema wananchi wenye asili ya Rorya wanaoishi Mirerani ni watu wenye kiu ya maendeleo na wamefanikisha mambo mengi ndiyo sababu amefika kuzungumza nao juu ya mikakati ya maendeleo.

Amesema mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya ni shilingi milioni 800 hivyo haitoshi kufanikisha maendeleo hivyo wanapaswa kushirikiana ili wapige hatua.

“Kila mwaka nitakuwa nakuja Mirerani kuzungumza na wana Rorya na mwezi wa 11 nitakuja na Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Mwenyekiti wa Halmashauri na Mkurugenzi ili tuwaeleze fursa za kiuchumi zilizopo nyumbani mje muwekeze,” amesema.

Amesema hivi sasa anakaribia kufikisha mwaka mmoja tangu achaguliwe kuwa mbunge na anapambana na changamoto tofauti ikiwemo miradi ya maji na amefanikiwa kupata greda inayochonga barabara kwenye maeneo ambayo hayana.

“Mradi wa maji wa kutoka ziwa Victoria kwenda Tarime utanufaisha baadhi ya vijiji vyetu na pia kuna mradi wa kituo cha mabasi tumeubuni utakuwa na maeneo ya kufanya biashara,” amesema Japhary.

Diwani wa kata ya Endiamtu, Lucas Chimba Zacharia, amesema kipindi akiwa Mwenyekiti wa Mara Group alifanikisha kufanya harambee na kupatikana zaidi ya shilingi milioni 70 zilizosambazwa kwenye shule zote za sekondari jimbo la Rorya.

“Fedha hizo zilitumika kujenga vyumba vya maabara za shule zote za sekondari kwenye jimbo la Rorya kipindi mbunge akiwa mheshimiwa Lameck Airo,” amesema Luka.

Amesema jamii ya wana Rorya wanaoishi Mirerani ni wana maendeleo hivyo wanamuahidi mbunge huyo Japhary kuwa wataendelea kuwa naye bega kwa bega katika kufanikisha maendeleo.

“Ndugu zangu mheshimiwa mbunge wetu Japhary amefika Mirerani kukutana na sisi hivyo tumsikilize na tuungane naye katika kuchangia maendeleo ya ndugu zetu wa Rorya,” amesema Luka.

Mkurugenzi wa shule ya awali na msingi Blue Tanzanite ya mchepuo wa kiingereza iliyopo mji mdogo wa Mirerani, Alex Raphael Ombade amesema jimbo la Rorya linapaswa kuwa na chuo cha ufundi (Veta) ili wanafunzi wasiofaulu wasome hapo.

“Ni bora hata shule moja ya sekondari igeuzwe kuwa chuo cha Veta cha serikali ili wanafunzi wanaoishia darasa la saba na kidato cha nne wapate taaluma na kujitafutia ajira,” amesema Ombade.

Amesema pia viwanda vya kuchakata samaki na zao la muhogo vinapaswa kuwepo ili ajira zipatikane na kusababisha mzunguko wa fedha kwa jamii ya eneo la Rorya.

Mkazi mwingine Lameck Ochola amesema huduma ya afya na barabara kwenye kata yao zinapaswa kuboreshwa ili wananchi waweze kupata huduma bora na mahitaji yao.

“Miundombinu ya barabara nyumbani kwetu kwenye Tarafa ya Suba ni mbovu na hakuna zahanati wala kituo cha afya na mtu akiugua anafuata huduma hiyo mbali kwa hiyo mheshimiwa Mbunge tunaomba uyafanyie kazi,” amesema Ochola.

Mkazi mwingine John amesema wazee wao wanashindwa kulala ndani usiku wakihofia wezi wa ng’ombe hivyo mbunge huyo ahakikishe anapambana kumaliza tatizo hilo.

“Pia kuna kile kiwanda cha maziwa cha Utegi, miaka iliyopita tulikuwa tunakunywa maziwa kupitia kiwanda hicho hivyo tusaidie kiwanda hicho kifanye kazi tena,” amesema John.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad