WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na
Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kutekeleza dhana ya
uchumi jumuishi kwa vitendo kwa kuweka vipaumbele vitakavyowawezesha
wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
Ameyasema
hayo leo (Jumatatu, Oktoba 4, 2021) wakati wa ufunguzi wa Kongamano la
Tano la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, jijini Dodoma. Amesema kuwa
vipaumbele katika mipango ya Serikali vimekuwa katika utekelezaji wa
shughuli za kiuchumi zinazowajumuisha moja kwa moja wananchi.
Waziri
Mkuu ametaja baadhi ya vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na uimarishaji
wa huduma za afya, hifadhi ya jamii, maji, umeme na utekelezaji wa
mpango wa elimumsingi bila ada “Mtanzania mwenye afya, aliyeelimika na
miundombinu wezeshi ni chachu kwa ukuaji uchumi wa nchi yetu.”
Amesema
uwezeshaji wa uchumi jumuishi ni msingi wa kuhakikisha kunakuwa na
ustawi endelevu kwa watu wote, ambapo Serikali imeandaa Dira ya
Maendeleo ya Taifa ya 2025 ambayo pamoja na mambo mengine imeainisha
mazingira wezeshi yatakayowezesha nchi kunufaika kiuchumi, kijamii,
kisiasa na kiutamaduni.
Mheshimiwa Majaliwa amesema Dira ya
Maendeleo ya Taifa ya 2025 pia imelenga kuhakikisha kunakuwa na viwango
vya juu vya maisha, amani na umoja, utawala bora na uchumi ulioimarika
wenye ushindani katika jamii.
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali
imeandaa sera mbalimbali ambazo zimelenga kuhakikisha kunakuwa na
maendeleo endelevu na uchumi jumuishi. “Kati ya Sera hizo ni Sera ya
Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 ambayo ni Sera
kiongozi kwenye masuala ya kuwezesha wananchi kiuchumi, sera hiyo
imeweka mikakati inayolenga kuhakikisha kwamba Watanzania wanashiriki
kikamilifu katika uchumi wa nchi”.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionesha kitabu cha Taarifa ya
Utekelezaji wa Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya Mwaka 2004 kwa
Mwaka 2020/21 baada ya kuizindua katika Kongamano la Tano la Uwezeshaji
Mwananchi Kiuchumi kwenye ukumbi wa Jengo la PSSSF Makole jijini Dodoma
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa pamoja na viongozi mbalimbali wakiwa katika picha
ya pamoja na wadhamini wa Kongamano la Tano la Uwezeshaji Mwananchi
Kiuchumi baada ya kufungua kongamano hilo kwenye ukumbi wa Jengo la
PSSSF Makole jijini Dodoma, Oktoba 5, 2021. Kulia kwake ni Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwezeshaji), Geofrey Mwambe.(Picha na Ofisi
ya Waziri Mkuu)


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua Kongamano la Tano la Uwezeshaji Mwananchi Kiuchumi kwenye ukumbi wa Jengo la PSSSF Makole jijini Dodoma.

Baadhi ya washiriki wa Kongamano la Tano la Uwezeshaji Mwananchi Kiuchumi wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua kongamano hilo kwenye ukumbi wa Jengo la PSSSF Makole jijini Dodoma

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akibonyeza kitufe wakati alipozindua Kanzidata ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi baada ya kufungua Kongamano la Tano la Uwezeshaji Mwananchi Kiuchumi kwenye ukumbi wa Jengo la PSSSF Makole jijini Dodoma, Oktoba 5, 2021. Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Geofrey Mwambe na kulia ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Beng’i Issa
No comments:
Post a Comment