Benki ya CRDB yaahidi kuendeleza ubunifu wa huduma bora kwa wateja - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, October 4, 2021

Benki ya CRDB yaahidi kuendeleza ubunifu wa huduma bora kwa wateja

Benki ya CRDB imewaahidi wateja wake kuendelea kutoa huduma na bidhaa bunifu zitakazowawezesha kufikia malengo yao ya kifedha. Ahadi hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja 2021 uliofanyika katika tawi la benki hiyo la Mlimani City Jijini Dar es Salaam.

Akitoa ahadi hiyo, Nsekela alisema Benki ya CRDB ikiwa kinara katika soko inaamini katika utoaji wa huduma bora kwa wateja wake na Watanzania kama njia ya kusaidia wateja kufikia malengo yao. “Tunapoadhimisha wiki hii tumejipanga kuendelea kutoa huduma bora na kuziboresha kadri ya matakwa ya wateja wetu ili tuendelee kuwaridhisha na kufanya huduma zetu kuwa na viwango zaidi,” alisema Nsekela.
Nsekela alisema Benki hiyo sasa hivi imetilia mkazo katika uwekezaji wa mifumo ya kidijitali ili kurahisisha upatikanaji kwa wateja. Mapema mwaka huu, Benki ya CRDB ilizindua huduma ya Simbanking iliyoboreshwa ambayo kwa sasa inamuwezesha mteja kufungua akaunti mwenyewe popote alipo, pia inamuwezesha kupata taarifa za akaunti yake na mengine mengi. 

Benki hiyo pia imeendelea kutanua wigo wa huduma kupitia mawakala “CRDB Wakala” ambapo katika kipindi cha nusu mwaka ya kwanza imefanikiwa kuongeza idadi ya mawakala kwa asilimia 22.8. Benki ya CRDB sasa hivi inatoa huduma kupitia mawakala zaidi ya 20,000 ambao wamerahisha kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma hususan katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa na huduma za kifedha.
“Malengo yetu ni kuona tunamuhudumia mteja kwa ukaribu na unafuu zaidi kupitia mifumo hii ya kidijitali. Lakini pia, kuwezesha huduma zetu kuweza kupatikana kidijitali kama ambavyo tumefanikiwa kupitia mikopo ya kidijitali kama Salary Advance, Pension Advance na Mikopo ya Jiwezeshe maalum kwa ajili Wamachinga,” alisema Nsekela huku akisisitiza kuwa Benki hiyo pia imewekeza vyakutosha katika mafunzo kwa wafanyakazi ili kuwajengea weledi na kuwawezesha kutoa huduma bora kwa wateja.
 
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja, Yolanda Uriyo alisema Wiki ya Huduma kwa Wateja ni fursa kwa Benki hiyo kuwashukuru  wateja wake kwa kuichagua Benki ya CRDB na hivyo kuifanya kuendelea kuwa Benki bora na inayoongoza hapa nchini. Aliwakaribisha wateja kutembelea matawi ya Benki ili kupata huduma bora, na kutoa maoni au ushauri ili kuiwezesha Benki hiyo kutoa huduma na bidhaa bora zaidi zitakazo fikia na kuzidi matarajio ya wateja. 
“Niwakaribishe wateja na Watanzania wote katika matawi yetu katika kipindi hiki kushuhudia ‘Nguvu ya Huduma’ kama ilivyo kauli mbiu ya mwaka huu kwani tumeboresha kwa kiasi kikubwa huduma zetu na naamini watafurahia,” aliongezea Yolanda.

Aidha, Yolanda alisema katika Wiki hii ya Huduma kwa Wateja Benki ya CRDB pia imejipanga kutembelea wateja wake katika maeneo yao kuwashukuru, kusikililiza mahitaji yao na kutoa elimu juu ya huduma na bidhaa mbalimbali zinazotolewa na Benki ya CRDB.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Heri James akizungumza katika hafla fupi ya uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wajeta ya Benki ya CRDB, iliyofanyika kwenye tawi la Mlimani City, jijini Dar es salaam.
 
Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na Wakati wa Benki ya CRDB, Boma Raballa akizungumza katika hafla fupi ya uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wajeta ya Benki ya CRDB, iliyofanyika kwenye tawi la Mlimani City, jijini Dar es salaam 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad