HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 28, 2021

Ayalagaya wakataa Maji kwenda kwingine, serikali yachukua maamuzi magumu

 

Na John Walter-Manyara
Mkuu wa mkoa wa Manyara Makongoro Nyerere amechukua uamuzi mgumu wa kupeleka maji maeneo mengine baada ya wananchi wa kata ya Ayalagaya wilayani Babati kuigomea Serikali kutumia chanzo cha maji kilichopo katika kata hiyo wakidai kuwa maji hayo hayatoshelezi hivyo hawataki yasambazwe maeneo mengine.
Akizungumza na wananchi hao katika mkutano wa hadhara uliofanyikia Dareda Kati oktoba 27 mwaka huu, Nyerere amemwagiza mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange kuanzia jumatatu Novemba 1,2021 kuanza utekelezwaji wa mradi huo uanze mara moja ili wananchi wenye shida ya maji waanze kupata huduma hiyo muhimu.
Kwa agizo la mkuu wa mkoa ni wazi kwamba sasa badala ya Mradi huo kuwa na kata nne sasa zimebaki tatu baada ya Ayalagaya kususia hivyo kata zilizobaki ni Bagara,Sigino na Arri.
Ameitaka mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira mjini Babati (BAWASA) kuacha shughuli za usambazaji wa maji katika maeneo ya Ayalagaya kwa kuwa wameikataa huduma hiyo mpaka pale ambapo watamwambia kuwa wanahitaji.
"Ninaagiza watu wa maji acheni shughuli za maendeleo ya maji kwenye kata ya Ayalagaya mpaka siku wakiniambia, siku watakayoniambia mimi nipo tayari" alisisitiza Nyerere
Mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange alishafika kijijini hapo akiambatana na mkuu wa mkoa Makongoro Nyerere kuzungumza na wananchi na viongozi ili kupata suluhuhisho ambapo awali walishakubaliana kuwa mradi uendelee.
Wazee wa Kimila la Kiiraq wa eneo hilo waliwapiga faini ya Ng'ombe watatu (Dume, Awuu kwa lugha ya Kiiraq) BAWASA kwa kosa la  kufika katika chanzo hicho ambacho kipo kijiji cha Bacho bila kuwasiliana nao, faini ambayo BAWASA walikubali kuilipa.
Uongozi wa kijiji uliwapeleka viongozi wa wilaya na mkoa kukagua chanzo hicho cha maji ambapo wataalamu wa maji walijiridhisha kuwa maji hayo yanatosha kwa ajili ya matumizi ya binadamu katika kata nne.
Wananchi wa eneo hilo la Ayalagaya na vijiji jirani wanasema kuwa  huyatumia maji hayo katika shughuli za kilimo cha Umwagiliaji,mifugo na matumzi mengine ya nyumbani.
Wakati mkuu wa mkoa akizungumza na wananchi wa eneo hilo, wakina mama wakiwa na fimbo mkononi walisimama na kuanza kupiga yowe ishara kuwa hawakubaliani na maagizo ya serikali kutoa maji kutoka katika chanzo hicho.
Kwa Mujibu wa mkurugenzi wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira mjini Babati (BAWASA) serikali imetoa shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuwafikishia wananchi wa kata nne huduma ya maji ambapo mradi ulitakiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2021.
Maji na Dira ya Taifa ya Mwaka 2025 inalenga kuinua hali ya maisha ya wananchi na kuwa na utawala bora unaozingatia Sheria na uchumi imara.
Pamoja na mambo mengine, Dira ina malengo makuu ya kuwa na (i) Maisha bora yaliyo endelevu katika mazingira huru, yasiyokuwa na kukithiri kwa umaskini, (ii) Utawala bora unaozingatia Sheria, (iii) Uchumi imara, endelevu na wenye manufaa kwa wote ambapo ili kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya 2025 ya kufuta umaskini, kuwa na chakula cha kutosha na cha uhakika, afya bora na kuwa na bayoanuai endelevu, maji ni moja ya nyenzo muhimu katika kufikia malengo haya.
Sera ya Maji na mapitio ya mifumo ya kisheria na ya kitaasisi inalengo la kufanikisha Dira hii.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad