WAZIRI SIMBACHAWENE AINGILIA KATI MGOGORO WA WAKULIMA, WAFUGAJI MALOLO, RAIS SAMIA ATOA MILIONI 250 UJENZI KITUO CHA AFYA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, September 23, 2021

WAZIRI SIMBACHAWENE AINGILIA KATI MGOGORO WA WAKULIMA, WAFUGAJI MALOLO, RAIS SAMIA ATOA MILIONI 250 UJENZI KITUO CHA AFYA

 Na Felix Mwagara, MoHA, Kibakwe.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amewataka viongozi wa Kata ya Malolo, Jimbo la Kibakwe, Wilayani Mpwapwa, kusuluhisha mgogoro wa wakulima na wafugaji haraka iwezekanavyo.

Amesema kitendo cha mgogoro huo kuendelea kuwa sugu mpaka sasa na kutokupatikana kwa suluhu ni kuonyesha kushindwa kwa viongozi wa Kata hiyo ambayo inaongozwa na Afisa Mtendaji wa Kata.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa Wananchi wa Kata hiyo, uliofanyika katika Kijiji cha Idodoma, Simbachawene amemtaka Afisa Mtendaji huyo kuhakikisha anafanya kikao cha mapatano kwa haraka kwa kukutana na Katibu wa Chama cha Wafugaji pamoja na wawakilishi wa wakulima na wafugaji ili kuzungumza na kumaliza mgogoro huo.

“Ukiona mfugaji anamchukia mkulima huyo hajitambui, hatambui umuhimu wa mkulima kwa mifugo, na ukiona mkulima anamchukia mfugaji hatambui umuhimu wa mfugaji kwa kilimo, nyie watu kwa asili mnategemeana, mnatakiwa kupanga utaratibu nyie wenyewe, sio kuacha mtu anafanya anavyotaka, lazima kuweka usawa maslahi ya watu hawa, na hii ndiyo kazi ya viongozi,” alisema Simbachawene

Aliongeza kuwa, “..huku vijijini tukisikia mahala wafugaji wanawanyanasa wakulima au wakulima wanawanyanyasa wafugaji tunajua kuwa kiongozi wa mahali hapo kazi imemshinda, kwahiyo viongozi mna  kazi kubwa, mtendaji wa kata ni mtu mkubwa sana, watumishi wote kwenye kata hii wapo chini yako, wananchi wote wapo chini yako, ili uweze kufanikisha maendekelo lazima uweze kuongoza vizuri, kiongozi lazima usimame na wanyonge, ukiona kiongozi hausimami upande wa wanyonge unatetea walichonacho, hiyo kazi imekushinda. ”

 Aidha, Waziri Simbachawene amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Ipera, jimboni humo ambacho kikikamilika kitakuwa kinahudumia idadi kubwa ya wananchi kutoka katika kata mbalimbali zilizopo Jirani na kata hiyo.

“Gharama ya ujenzi wa Kituo hiki ni shilingi milioni 500, lakini tayari Rais Samia ametoa milioni 250 ili ujenzi uweze kuanza, na pia nimejisikia na furaha baada ya kuwaona wananchi mkijituma kusafisha eneo hili litakalojengwa kitu cha afya, hakika mnaonyesha umoja wa hali ya juu, hongereni sana,” alisema Simbachawene.

Simbachawene aliongeza kuwa, Kituo hicho kikikamilika kitaweza kuhudumia pia wananchi wa Kata ya Malolo, Galigali, Mbuga, Masa, Nang’aliza, pamoja na Kata yenyewe ya Ipera ambapo kitakua na jengo la wagonjwa wa nje (OPD) ambao watakuja kupata matibabu na kuondoka, pia kutakua na wodi, sehemu ya kuhifadhia maiti, na operesheni mbalimbali zitafanyika.

Hata hivyo, Waziri Simbachawene alisema Rais Samia kwa kipindi cha miezi mitano ametoa bilioni mbili ambazo zimetolewa kwa ajili ya kurekebisha barabara za Jimbo hilo, ambapo kati ya fedha hizo, milion 500 zimetengwa kwa ajili ya kujenga barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 1.3 Kibakwe mjini.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akizungumza na wananchi wa Kata ya Ipera, Jimboni kwake Kibakwe, Mkoani Dodoma, leo, baada ya kuwakuta wananchi hao wakilisafisha eneo ambalo kitajengwa Kituo cha kisasa cha Afya cha Ipera, jimboni humo baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho kitakapokamilika kitakuwa kimegharimu shilingi milioni 500.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akipokea zawadi ya mbuzi kutoka kwa wananchi wa Kijiji cha Kinusi ikiwa ni kumshukuru Waziri huyo kwa kuwezesha kupatikana kwa fedha ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Ipera jimboni humo. Waziri amewaambia wananchi hao kuwa, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.
Wananchi wa Kijiji cha Kinusi, Kata ya Ipera, Jimbo la Kibakwe wakisafisha eneo lililopitishwa na wataalamu wa Halmshauri ya Wilaya ya Mpwapwa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Ipera jimboni humo, Mkoani Dodoma, leo. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo hilo, George Simbachawene aliwasili katika eneo hilo na kuwakuta wananchi hao wakisafisha eneo hilo. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Idodoma, Kata ya Malolo, Jimboni kwake Kibakwe, Mkoani Dodoma, leo, amemtaka Afisa Mtendaji wa Kata ya Malolo jimboni humo kusuluhisha mgogoro wa wakulima na wafugaji kwa kuwakutanisha ili waweze kupatana na kuishi kwa amani na kushirikiana. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad