HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, September 10, 2021

WAZIRI DKT. GWAJIMA AAGIZA KUUNDWA KAMATI KUONESHA MCHANGO WA NGOs NCHINI

Na Mwandishi Wetu Dodoma

 

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu kuunda Kamati maalum itakayofanya tathimini ya mtawanyiko na mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Maendeleo ya Taifa.

 

Dkt.Gwajima ametoa agizo hilo Leo jijini Dodoma wakati akipokea taarifa ya maazimio ya kikao cha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kilichofanyika Januari, 2021 na kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Serikali na Mashirika hayo ili kuleta Maendeleo endelevu ya Taifa kwa ujumla.

 

Agizo hili limekuja kutokana na maazimio na mapendekezo ya Mashirika hayo kwa Serikali  ya kufanya tathmini ya mchango wa Mashirika hayo katika kuleta maendeleo kwa wananchi katika maneno mbalimbali nchini ili kuwa na taarifa sahihi za Mashirika yapi yamefanya nini katika eneo gani

 

Waziri Gwajima ameongeza kuwa Wizara itahakikisha kunakuwa na usimamizi mzuri wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili yaweze kusaidiana na Serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali.

 

"Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan imejinasibu katika kushirikiana na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili kuwaletea maendeleo wananchi  katika Maeneo mbalimbali" alisema Dkt. Gwajima

 

Aidha ameyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kuzingatia uwazi na uwajibikaji kwa kuhakikisha fedha wanazozipokea kutoka chanzo mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi zitumike kwa kadri ilivyotarajiwa  ili kuleta matokeo chanja katika jamii.

 

Amesema  uwepo wa uwazi na uwajibikaji wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini utasaidia Serikali kupata taarifa ya miradi inayotekelezwa na Mashirika hayo na kwa namna gani imesaidia wananchi katika kuwaletea maendeleo.

 

Akitoa taarifa ya maazimio ya kikao cha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Naibu Mkurugenzi wa Mpango wa Uwajibikaji Tanzania  (Accountability in Tanzania Program) Rehema Tukai amesema kikao kilichofanyika kilitoka na mazimio matano ambayo yamelenga katika kuhakikisha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini yanashirikiana na Serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kuzingatia Sheria na taratibu zilizopo.

 

Kwa upande wake Katibu wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ( NaCONGO) Revocatus Soro amemwakikishia Waziri kuendelezwa ushirikiano miongoni mwa Mashirika na kati ya  Mashirika na Serikali ili kuhakikisha Sekta ya NGOs nchini inatoa mchango kwa maendeleo ya jamii.

 

Wakati huo huo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ampokea mwaliko wa Mkutano wa Mwaka wa NGOs utakaofanyika tarehe 29-30, Septemba, 2021. Jijini Dodoma.

 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akipokea maazimio ya kikao cha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kilichofanyika Januari, 2021 leo Ofisini kwake jijini Dodoma.

 

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na baadhi ya wawakilishi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali wakati akipokea maazimio ya kikao cha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali  kilichofanyika Januari, 2021 leo Ofisini kwake jijini Dodoma.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akimsikiliza mmoja wa Wawakilishi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali wakati akipokea maazimio ya kikao cha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali  kilichofanyika Januari, 2021 leo Ofisini kwake jijini Dodoma.

 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad