MIZANI WATAKIWA KUTOA ELIMU KWA WASAFIRISHAJI WAKATI WOTE - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, September 10, 2021

MIZANI WATAKIWA KUTOA ELIMU KWA WASAFIRISHAJI WAKATI WOTE

 Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, amewataka Wakala wa Barabara (TANROADS), kukutana na wadau wa usafirishaji mara kwa mara ili kuwaelimisha Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018  zinavyofanya kazi ili kuondoa malalamiko ya mara kwa mara.

Akikagua utendaji kazi wa Mizani ya Nala jijini Dodoma leo, Naibu Waziri Waitara amewataka wafanyakazi wa mizani kutoa elimu kwa kila dereva wa lori kila anapokaguliwa ili kuepusha madereva hao kuongeza mizigo njiani na kusababisha usumbufu kwa wamiliki wa malori na lawama kwa wafanyakazi wa mizani.

“Hakikisheni mnapopima magari mnawaeleza uzito uliopo na ni nini anastahili dereva kufanya ili kuepuka kuzidisha uzito na kuharibu barabara”, amesisitiza Naibu Waziri huyo.

Akiwa katika mizani hiyo Naibu Waziri Waitara ameshuhudia baadhi ya madereva wa malori kukiri kuongeza mizigo ya ziada na hivyo kukamatwa kutokana na kuzidisha uzito hali ambayo inasababisha usumbufu kwa wamiliki.

Amewataka wasimamizi wa mizani kote nchini kuhakikisha kwamba abiria wa mabasi yaliyozidisha uzito hawapati usumbufu wanapokuwa safarini kwa makosa ya madereva.

Aidha, amewasisitiza watumishi wa mizani kuhusu umuhimu wa kutenda haki kwa magari yote yanayozidisha uzito ili kuondoa malalamiko na upendeleo.

Naye, Kaimu Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Salehe Juma, amesema magari mengi yanayotozwa faini yanatokana na ukaidi wa madereva wenyewe kutotoa taarifa kwa wamiliki pindi wanapokamatwa kwa kosa la kuzidisha uzito kwani sheria inatoa fursa kwa magari kukaa siku tatu bila ya kuchajiwa kwa ajili ya kupunguza mizigo iliyozidi.

Naibu Waziri huyo alikuwa kwenye ziara ya kukagua changamoto zinazoikabili Kitengo cha Mizani ikiwa ni muendelezo wa mkakati wa Wizara kujenga taswira njema katika huduma ya usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya nchi.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akikagua moja ya kontena katika lori lililokamatwa kutokana kuzidisha uzito katika Mizani ya Nala, jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akikagua kitabu cha faini kinachotumika kwa magari yanayozidisha uzito Mizani ya Nala, jijini Dodoma. Katikati ni Dereva wa lori Bw. Abdul Hamad, akifuatilia.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akikafafanua jambo kwa Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Salehe Juma, mara baada ya kukagua Mizani ya Nala, jijini Dodoma.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Salehe Juma, akifafanua jambo kwa madereva waliokamatwa kutokana na kuzidisha uzito (hawapo pichani), katika Mizani ya Nala, jijijni Dodoma.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad