
…………………………………………………………………….
Na Dorina G. Makaya – Dar-es-salaam.
Watumishi
wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wamewatakiwa kuwa tayari kupokea
mabadiliko, kufanya kazi kwa bidii na weledi na kutoa ushirikiano mzuri
kwa uongozi wa TANESCO na bodi mpya iliyoteuliwa ili kulijenga upya
Shirika la TANESCO na kuliwezesha kufikia malengo yanayotarajiwa na
Serikali.
Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Nishati Mhe. January
Makamba leo tarehe 26 Septemba, 2021 alipokuwa anazungumza na watumishi
wa TANESCO kwenye mkutano wake na Mameneja wa TANESCO uliofanyika katika
ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar-es-salaam.
Waziri
Makamba amewaambia watumishi wa TANESCO, kuanzia sasa, hakutakuwa na
uonevu kabisa kwenye Shirika la TANESCO na kuwa, wafanyakazi wajiweke
tayari kufanya kazi kwa ushirikiano, bidii na maarifa ili kuongeza
utendaji wenye tija.
Amesema, uteuzi uliofanywa wa viongozi wa
juu wa Menejimenti ya TANESCO na Bodi, unatoa taswira na ishara namna
ambavyo Serikali inataka shirika la TANESCO liongozwe.
Aidha,
Waziri Makamba ameeleza kuwa, mkutano huo umelenga kufahamiana na
kuutambulisha uongozi mpya kwa watumishi hao wa TANESCO na kuwa, uteuzi
na utenguzi uliofanywa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Samia Suluhu Hassan na ule uliofanywa na yeye Waziri wa Nishati,
unamaanisha kuwa, Serikali inataka mapinduzi makubwa katika sekta ya
umeme.
“Tunataka shirika letu liendeshwe kwa ufanisi, kibiashara,
liwe shirika linalowajali watumishi wake, linalochangia kwenye
maendeleo na ukuaji uchumi hapa nchini na linaloheshimika zaidi Afrika
Mashariki. Tumewaletea uongozi mpya, bodi mpya na sasa tunaanza safari
yenye mwelekeo mpya.” Alisema Waziri Makamba.
Waziri Makamba
aliongeza kuwa, Serikali haitavumilia wizi, dhuluma wala hujuma na
inatarajia kiwango cha juu sana cha uadilifu na uchapa kazi na kuwa,
hiyo ni ahadi inayopeana kati ya viongozi na Serikali.
Akizungumzia
kuhusu mabadiliko yaliyofanyika hivi karibuni kwa uongozi wa TANESCO,
Waziri Makamba amesema, ni uamuzi mgumu sana kumuondoa mtu kazini hasa
mtu mwenye nafasi kubwa kama Mkurugenzi Mkuu, mtu wa manunuzi, mtu wa
sheria, lakini ni uamuzi ambao ni wa lazima ili kufikia malengo.
“Na
uamuzi huo tumeuchukua kwa sababu tunataka mambo yaende. Hawa
walioondolewa wamefanya kazi mpaka walipotufikisha, na haina doa kwamba
ni watu ambao ni wa ovyo ila tunataka mwelekeo mpya. Na tunahitaji timu
mpya ambayo itatupeleka kule tunarajia. Alisema Waziri Makamba.
Waziri
Makamba amewaambia watumishi hao wa TANESCO kuwa, Mwenendo mpya ni
kuwa, atakayefanya kazi vizuri, ataonekana na atatunukiwa. “Tunaamini
kwamba mabadiliko yaliyofanyika na mwelekeo mpya mmeupokea na
mtautekeleza” alisema Waziri Makamba.
Akizungumza kwa nyakati
tofauti katika kikao hicho, Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen
Byabato amesema, bodi iliyoteuliwa ni muhimu sana kwa maendeleo ya
shirika la TANESCO na kuwa Wizara ya Nishati inaitegemea sana bodi hiyo
katika kutoa ushauri utakaoiwezesha TANESCO kufikia malengo
yanayotarajiwa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO Bw. Maharage
Chande amewaambia watumishi hao wa TANESCO kuwa, malipo yatatokana na
utendaji. Kama mtumishi anafanya kazi vizuri apewe aneemeke na mtumishi
asiyefanya kazi vizuri afundishwe, na iwapo baada ya kufundishwa
mtumishi bado hafanyi vizuri basi mtumishi huyo atakuwa hafai.
Bw.
Chande amesema, maamuzi magumu hayawezi kufanikiwa bila kuwa na
ushirikiano wa pamoja baina ya watumishi na viongozi na kuwataka
watumishi wa TANESCO kwa pamoja washirikiane kuyatafuta yaliyo mazuri na
pia washirikiane kuyakataa mabaya.
“Malipo kutokana na utendaji,
ushirikishwaji wa wafanyakazi, motisha kwa wafanyakazi, uendelezaji wa
watumishi kitaaluma, mpango mzuri wa kurithisha vyeo watumishi, ndiyo
yatakayopewa uzito wa juu na yatafanyika kwa haraka sana.” Amesema
Chande.
Aidha, Bw. Chande amewatahadharisha watumishi hao wa
TANESCO kuwa, wakati wa kuanza safari ya kuijenga TANESCO mpya,
watakutana na changamoto na kuwataka wawe jasiri katika kusonga mbele.
Aidha,
Mkurugenzi Mkuu huyo wa TANESCO amesema, mara baada ya kikao hicho,
atakutana na Mameneja hao wa TANESCO ili kutoa dira na mwelekeo wa
shirika wenye lengo la kuifanya TANESCO kuwa shirika bora si tu kwa
Afrika Mashariki bali katika bara la Afrika.
Naye mwenyekiti wa
bodi ya TANESCO Bw. Omari Issa amesema, mabadiliko yanayotarajiwa kwa
TANESCO yatafanywa na watumishi wa TANESCO wenyewe. Na kuwa, kipaumbele
cha kwanza ni Rasilimali watu na kusisitiza kuwa kila mtumishi wa
TANESCO awe tayari kubadilika ili kuyafikia malengo yaliyowekwa na
Serikali kwa Shirika la TANESCO.
Amewaomba watumishi wa TANESCO
waiunge mkono bodi ya TANESCO na kuyakubali mabadiliko ikiwa ni pamoja
na kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
Bw. Issa amemuomba Waziri wa
Nishati kufikisha salaam zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kumuamini na kumteua kuiongoza
bodi ya TANESCO na kuahidi kufanya kazi hiyo kwa uaminifu mkubwa na kwa
kujituma.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, mameneja wa Kanda –
TANESCO wamempongeza Waziri Makamba kwa uteuzi na kwa hotuba nzuri
aliyoitoa kwa watumishi wa TANESCO yenye matumaini ya kuijenga kiupya
TANESCO kwa lengo la kuongeza ufanisi na utendaji wenye tija.
Nae
Meneja Mwandamizi wa Rasilimali watu Fransis Sangunaa, akizungumza kwa
niaba ya wafanyakazi wa TANESCO, amesema, watumishi wa TANESCO watatoa
ushirikiano mkubwa na wa kutosha ili kuyafikia malengo yale ambayo
Serikali inatarajia kuyafikia kupitia shirika la TANESCO.
Akitoa
neno la shukrani katika mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya
Nishati, Kheri Mahimbali, amewapongeza viongozi walioteuliwa na
kuwashukuru viongozi hao kwa kushiriki katika kikao hicho muhimu.
Vile
vile kwa niaba ya watumishi wote wa Wizara ya Nishati, amemshukuru
Waziri wa Nishati kwa muongozo alioutoa na kuahidi kuwa viongozi wa
Wizara ya Nishati pamoja na watumishi, wako tayari kutoa ushirikiano ili
kuwezesha mapinduzi ya Nishati kwa ajili ya maendeleo makubwa zaidi.
Mkutano
huo, umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Naibu Waziri wa
Nishati, Wakili Stephen Byabato, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mha.
Leonard Masanja, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali,
Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Felchesmi Mramba, Kamishna wa
Petrol na Gesi, Michael Mjinja, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu
wa Wizara ya Nishati, Ziana Mlawa na mameneja wa TANESCO nchini
No comments:
Post a Comment