WANAFUNZI ENDIAMTU WAKATIWA MAJI KWA MIAKA MITANO - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, September 22, 2021

WANAFUNZI ENDIAMTU WAKATIWA MAJI KWA MIAKA MITANO

Na Joseph Lyimo
WANAFUNZI wa msingi Endiamtu, Kata ya Endiamtu, Mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro, Mkoani Manyara, wanakabiliwa na ukosefu wa maji baada ya bomba lililokuwepo kukatwa kwa zaidi ya miaka mitano iliyopita.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Evetha Kyara, amesema shule hiyo yenye wanafunzi 894 wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa maji baada ya maji ya bomba yaliyokuwepo awali kukatwa.

Mwalimu Kyara amesema Diwani wa kata ya Endiamtu, Lucas Zacharia alifanikisha upatikanaji wa maji kwenye eneo hilo miaka saba iliyopita ila baada ya miaka miwili maji hayo yalikatwa.

Amesema kutokana na hali hiyo ya ukosefu wa maji inawalazimu wanafunzi wa shule hiyo wawe wanabeba maji na madumu kutoka majumbani mwao na kufika nayo shuleni hapo.

Diwani wa kata ya Endiamtu Lucas Zacharia amesema alifanikisha kuvuta maji ya bomba shuleni hapo kwenye kipindi chake cha mwaka 2010-2015 ila baada ya kura za udiwani kutokutosha Octoba mwaka 2015 maji yakakatwa.

Zacharia amesema alitumia gharama zake kwa zaidi ya shilingi milioni 2 ili kufanikisha upatikanaji wa maji hayo ya bomba shuleni hapo ila yakakatwa baada ya yeye kuondoka madarakani.

“Hivi sasa nimerudi nitahakikisha maji yanapatikana kwani siyo vyema wanafunzi wa shule hii kwenda shuleni wakiwa na madumu ya maji suala ambalo lingepatiwa ufumbuzi,” amesema Zacharia.

Katibu wa CCM kata ya Endiamtu, Anthony Mavili akiwa na kamati ya siasa ya CCM ya kata hiyo, baada ya kufika shuleni hapo amesema wamelichukua suala hilo na watalifikisha mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani.

“Siyo sawa kama baadhi ya viongozi wa vitongoji waliagiza kwa watu wa idara ya maji kuwa maji yakatwe shuleni na kupelekwa eneo jingine, tutafuatilia hilo,” amesema Mavili.

Mmoja kati ya viongozi wa eneo hilo, ambaye hakutaka kutaja jina lake, amesema baadhi ya wenyeviti wa vitongoji wa eneo hilo walishirikiana na kuagiza maji yakatwe kwenye shule hiyo.

“Wenyewe waliona wapiga kura wao ndiyo bora kuliko wanafunzi hivyo wakaagiza kuwa maji yakatwe kwenye shule hiyo na kusambazwa kwa wapiga kura wao mitaani,” amesema.

Amesema suala la maji ni sawa na nishati ya umeme na huwezi kununua nguzo ya umeme na kuihodhi hivyo hata kama ni Diwani alinunua mabomba ili maji yaende shuleni lakini wakayakata yaende kwa wananchi.

Mmoja kati ya wanafunzi wa shule hiyo, Elias John aliwaomba viongozi wa eneo hilo kuhakikisha wanafanikiwa kupatiwa maji kwani wanapata wakati mgumu kwa kukosa maji.

Amesema inawalazimu kuchota maji na madumu kutoka majumbani mwao na kwenda nayo mashuleni, ilihali awali kulikuwa na maji yaliyofanikishwa na Diwani wao.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Adam Kobelo amesema hana taarifa ya maji kukatwa kwenye shule hiyo ya msingi Endiamtu.

"Suala la mtu kudai kuwa kuna wenyeviti wa vitongoji waliwaagiza wataalamu wa idara ya maji wakate maji shuleni hapo ili wapiga kura wao wapate siyo ukweli," amesema Kobelo.

Amesema mara nyingi uongozi wa serikali hauwezi kukubali kukata maji kwenye taasisi ya serikali na kupeleka kwa wananchi kwani wote wanahitaji huduma hiyo ya maji.

Amesema miaka mitano iliyopita walinikiwa kufikisha maji kwenye taasisi mbalimbali ikiwemo shule ya msingi Jitegemee, Tanzanite na Mirerani na shule za sekondari.

"Tungepatiwa taarifa tungefanikisha hilo kwani kuunganisha bomba haizidi kiasi cha shilingi laki 2 tungefanikisha kutengeneza bomba na kurejesha bila tatizo," amesema Kobelo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad