NICOL yazidi kufanya maajabu kwenye soko - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, September 22, 2021

NICOL yazidi kufanya maajabu kwenye soko

 

*Yaendelea kupata faida hisa zake zikipaaa
Na Mwandishi Wetu
HISA za Kampuni ya NICOL (National Investments PLC) zimeendelea kufanya vizuri katika Soko la Hisa la Dar es Salaam kutokana na kazi nzuri inayofanywa na bodi ya kampuni hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake Dk. Gideon Kaunda.

Thamani ya hisa moja ya kampuni hiyo imepanda kutoka Sh 170 hadi Sh 250 sawa na ongezeko la asilimia 47 huku NICOL ikiwahamasisha wananchi na wawekezaji kutumia fursa hii kuwekeza kwenye kampuni hiyo kwa kuwa thamani ya uwekezaji inaendelea kukua.

Kwa mujibu wa taarifa za mahesabu ya NICOL yaliyotolewa na kusambazwa katika vyombo vya habari, inaonyesha kuwa faida ya nusu mwaka imekua kwa asilimia 68 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2020 na wakati huo huo gharama za uendeshaji za kampuni ya NICOL zimepungua kwa zaidi ya asilimia 37 ikilinganishwa na msimu uliopita.

Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya NICOL, Erasto Ngamilaga, amesema kuwa faida hiyo imetokana na ongezeko la mapato ya msimu wa nusu mwaka wa 2021 yaliyotokana na faida ya uwekezaji katika makampuni mbalimbali pamoja na riba za hati fungani.

Ngamilaga amesema kutokana na mafanikio hayo, Bodi na Menejimenti ya kampuni ya NICOL zinaendelea kuchukua hatua kuongeza mapato, na kupunguza matumizi hatua ambazo zitawezesha kuendelea kuimalisha uwekezaji na kuongeza malipo ya gawio kwa wanahisa wake.

“Tunafanya vizuri na tunaahidi kuendelea kufanya vizuri zaidi na wanahisa wetu watarajie kuona bei ya hisa za kampuni katika soko la hisa DSE zinaendelea kuimarika, sambamba na kuongezeka kwa malipo ya gawio kwa wanahisa wetu,” alisema

Amesema mpango mkakati wa Kampuni hiyo ni kutawanya uwekezaji katika maeneo yenye kuleta tija kwa wanahisa, ambapo mpaka tarehe ya mahesabu ya kampuni hiyo wamewekeza kwenye dhamana za serikali zaidi ya Sh bilioni 7.6 na matarajio ni kuongeza uwekezaji kwenye dhamana za serikali hadi kufikia Sh bilioni 15 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2021.

Amesema uwekezaji huo utasaidia kuboresha mapato kwa wanahisa kwa kuongeza gawio na kuongeza thamani ya kampuni na pia kuimalisha bei ya hisa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam.

“Bodi inawashukuru wanahisa na taasisi mbalimbali zinazotoa ushrikiano katika kuliendeleza shirika hilo na wananchi wachukue fursa kuwekeza kwenye shirika linaloendelea kuimarika siku hadi siku,” amesema

Amesema mbali na mkakati wa kuwekeza kwenye dhamana za serikali zinazotoa faida ya asilimia 15 kwa mwaka, NICOL iko kwenye mpango wa kuboresha mpango mkakati wa uwekezaji wa miaka mitano.

Ameogeza kuwa, mpango mkakati huo 2022-2025 unatarajiwa kukamilika na kuanza kazi mwakani na kusema kuwa kuhusu gawio na mkutano wa Mwaka 2020, Bodi ya Wakurugenzi itawatangazia wanahisa hivi karibuni.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad