Naibu
Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu) Mhe. Ummy Nderiananga
akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya kupokea vifaa saidizi
kwa ajili ya wenye ulemavu vilivyotolewa na Taasi ya kutoa huduma ndogo
za kifedha (ASA Microfinance Company Limited) katika Ukumbi wa Ofisi
hiyo Septemba 28, 2021 Jijini Dodoma.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Kampuni ya ASA Microfinance Company Limited, Muhammad Shah
Newaj akitoa salamu za kampuni hiyo kabla ya kukabidhi vifaa saidizi
kwa watu wenye ulemavu katika Ofisi ya Waziri Mkuu enep la Mtumba Jijini
Dodoma.
Kaimu
Mkuu wa Kitengo cha Watu Wenye Ulemavu Ofisi ya Waziri Mkuu Bw.Jacob
Mwinula akizungumza katika hafla ya kupokea vifaa saidizi kwa ajili ya
wenye ulemavu vilivyotolewa na Taasisi ya kutoa huduma ndogo za
kifedha (ASA Microfinance Company Limited)..
Afisa Sheria kutoka kutoka kampuni ya ASA Microfinance Company Limited, Zephania Paul akifafanya jambo wakati wa hafla niyo.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Kampuni ya ASA Microfinance Company Limited, Muhammad Shah
Newaj ( wa tatu kulia) akikabidhi vifaa saidizi vya watu wenye ulemavu
kwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu) Mhe. Ummy
Nderiananga ( wa nne kulia ) Jijini Dodoma.
Naibu
Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu(Wenye Ulemavu) Mhe. Ummy Nderiananga na
baadhi ya viongozi wa Kampuni ya ASA Microfinance Company Limited wakiwa
katika picha ya pamoja na watu wenye ulemavu baada ya makabidhiano
hayo.
(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
…………………………………………………………………..
NA MWANDISHI WETU, DODOMA
SERIKALI
imesema inaendelea na utaratibu wa kujenga na kukarabati vyuo vya watu
wenye ulemavu kwa lengo la kuwasaidia wenye ulemavu kupata ujuzi ili
kujikomboa kiuchumi.
Akizungumza Jijini Dodoma baada ya kupokea
msaada wa vifaa visaidizi kwa ajili ya wenye ulemavu vyenye thamani ya
shilingi milioni 13.9 ambavyo ni viti mwendo 55 na fimbo nyeupe 50
za wasioona kutoka kwa Taasisi ya kutoa huduma ndogo za kifedha (ASA
Microfinance Company Limited), Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga
alisema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila mtanzania anapata haki
yake bila vikwazo.
Aliongeza kuwa ipo mikakati madhubuti ya
kuhakikisha masuala ya wenye ulemavu yanapewa kipaumbele ikiwemo
uboreshwaji wa vyuo ikiwemo Chuo cha Mwanza ambacho ujenzi wake
unatarajiwa kukamilika kuanzia mwezi Januari mwakani kuwawezesha vijana
kupata mafunzo ambayo yatawasaidia kufanya shughuli zao za uzalishaji
na kushiriki katika maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
“Kwasasa
Wizara inaratibu kwa kasi ujenzi wa vyuo vya watu wenye ulemavu na
ufufuaji wa vile ambavyo vipo.Tunaendelea kufanya hivyo katika Chuo cha
Yombo Dar es salam, tumezindua Chuo kingine Tabora ambacho kilikuwa
kimefungwa kwa miaka 10 na kumalizia ujenzi wa chuo cha kisasa Mkoa wa
Tanga,” alisema Naibu Waziri Ummy.
Pia Naibu Waziri huyo
alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia
Suluhu Hassan imeweka mkazo kuwasaidia watu wenye ulemavu kwa kuendelea
kutoa fedha ya elimu bila malipo ambapo watu wenye ulemavu nao
hunufaika na mfumo huo huku akieleza kuwa Serikali inatambua changamoto
zinazowakabili watu wenye ulemavu.
“Serikali kupitia bohari kuu
ya dawa inaendelea kuagiza mafuta ili kuwakinga dhidi ya saratani ya
Ngozi kwa watu wenye ualbino sambamba na kuzitaka Halmashauri kuendelea
kutenga fedha za mapato ya ndani kupitia asilimia 10 inayotolewa na
kila Halmashauri kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu kwa sababu hii
inawasaidia kupambana na umasikini,”alieleza.
Hata hivyo
aliishukuru kampuni hiyo kwa moyo wake wa kujitoa na kuiunga mkono
serikali katika juhudi za kuwaletea ustawi wananchi wake na kuwahimiza
wadau wengine wa maendeleo kujitokeza kuwasaidia watu wenye ulemavu
hatua itakayofanya kujiona wana thamani na kutambulika ndani ya jamii.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa ASA Microfinance Limited , Muhammad
Shah Newaj alieleza kwamba wametoa msaada huo wenye thamani ya Sh.
milion 13.9 kama sehemu ya kutambua mchango wa watu wenye ulemavu
katika maendeleo kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa akisema wana uwezo
wa kufanya kazi kama watu wengine endapo watapewa fursa na kuhudumiwa
katika mahitaji yao wataendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha
wanaisaidia jamii kuepukana na umaskini.
Naye Afisa Sheria kutoka
ASA Microfinance Limited, Zephania Paul alifafanua kwamba vifaa hivyo
ni sehemu ya kutoa huduma kwa jamii na awamu hiii ni yapili kufanyika
akisema awamu ya kwanza ilifanyika jijini Dar es salaam huku akibainisha
kuwa taasisi hiyo ipo katika Mikoa nane ya Tanzania Bara na Zanzibar
na hadi sasa wamewafikia wanawake 1,600 na kutoa ajira .
Akitoa
shukrani zake mama wa mtoto mwenye ulemavu Martha Mshama aliishukuru
serikali kwa kushirikiana na wadau kuendelea kuwajali watu wenye ulemavu
akieleza kuwa kiti alichopewa kitamsaidia kufanya kazi zake kwani
awali alikuwa akitumia muda mwingi kuwa karibu na mtoto akihofia
kuanguka na kupata madhara.
” Tunaishukuru serikali kwa kutupatia
viti mwendo ambapo ni msaada mkubwa kwangu maana nilikuwa nikihofia
usalama wa mtoto wangu kuna wakati anaweza kuanguka natakiwa kuwa naye
karibu sana lakini sasa walau nitaweza kufanya kazi zangu nawashukuru
sana Mungu awabariki,”alishukuru Martha.
Naye Selina Nigangwa
(mwenye ulemavu wa miguu) mkazi wa Swaswa aliishukuru serikali kwa
kuwapatia msaada huo na kushauri wakati mwingine kutoa viti vya
kuendesha kwa kutumia mikono.
“Tunashauri serikali wakati
mwingine watoe viti vya kuendesha kwa mikono ili tuweze kuendesha
wenyewe bila kumtegemea mtu,” alieleza Selina.
No comments:
Post a Comment