HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, September 12, 2021

NAIBU WAZIRI UMMY AZINDUA PROGRAMU YA ONGEA JIJINI DODOMA

SERIKALI imesema Vijana ni kundi tegemewa kwa Taifa kwani wanabeba dira ya Taifa kutokana na mchango wao mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa hivyo wanapaswa kulindwa dhidi ya changamoto zinazowakabili zikiwemo UKIMWI na vitendo vya ukatili.

 

Hayo yalisemwa Septemba 11, 2021 na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga wakati akizindua Programu ya ONGEA Kitaifa Jijini Dodoma yenye lengo kuwafikia Vijana nchi nzima kupata uelewa wa masuala ya Maambukizi virusi vya UKIMWI kupitia vyombo vya habari.

 

Katika uzinduzi wa programu hiyo TACAIDS inashirikiana na wadau wa maendeleo ikiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto (UNICEF) ambapo programu hiyo ni kampeni ambayo imetengenezewaa vipindi maalum vya redio ambavyo vina ujumbe unaowalenga vijana ili kuwezesha kundi hilo kutambua masuala VVU na Ukimwi vitakavyorushwakupitia Clouds Fm na East Africa Radio.

 

Naibu Waziri Ummy alieleza kuwa Uzinduzi wa programu ya kimataifa ya ONGEA ni fursa ya kuwafia vijana balehe nchini kupitia vyombo vya Habari ili kuwaongezea uelewa kuhusu matatizo na changamoto zinazowakabili katika Maisha yao ya kila siku ikiwemo maambukizi ya VVU ili wachukue hatua za kuandaa mikakati mbalimbali katika kukabiliana na changamoto hizo.

 

“Serikali kupitia uongozi wa Mheshimwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan tunaamini vijana ndio waliobeba taifa letu na ndiyo nguvukazi ya nchi kwa hiyo kwa pamoja lazima lazima tuhakikishe ushirikiano unakuwepo katika kulinda afya zao,” alisema Naibu Waziri Ummy

 

Aidha, Naibu Waziri Ummy alitoa wito kwa Vijana nchini wafuatilie maudhui ya programu hiyo ya ONGEA kwa kina huku akifafanua kuwa programu hiyo itakuwa ya miezi tisa lengo likiwa kuwafikia Vijana zaidi ili waweze kuondoa vikwazo kwa Vijana balehe kupitia vipindi vya redio.

 

“Kupitia programu hii tufanikiwa kuongeza uelewa pamoja na ongezeko la upimaji wa afya kutoka asilimia 43 mpaka 57 hivyo kutakuwa na manufaa makubwa, "alisema Naibu Ummy.

 

Pia aliwataka wazazi kuwajibika na kuvunja ukimya kwa kutenga muda wa kuongea na Watoto wao, kuwapa elimu ya afya na uzazi ili kuepuka mazingira hatarishi huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kulinda Vijana watimize ndoto zao.

 

"Nitoe wito kwa wazazi tuongee na watoto wetu kwa kufanya hivyo tutasikia mengi kutoka kwao na kujua mahitaji yao muhimu katika kuwasaidia waepuke vishawishi, ni matumaini yangu programu hii inakuza uhusiano baina yao na huduma za afya kuwajengea huru wa kujitokeza kupima afya zao,"alieleza.

 

Katika hatua nyingine alipongeza Mashirika mabalimbali na wadau kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania akisema Serikali itaendelea kufanya Kazi pamoja katika kusimamia ustawi wa Vijana huku akisisitiza vyombo vya habari kushiriki kikamilifu katika kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu mapambano dhidi ya virusi vya Ukimwi.

 

“Kipekee niwapongeze TACAIDS na wadau wa maendeleo ikiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto (UNICEF) kwa kuhakikisha tunashirikiana katika kutekeleza kwa pamoja programu hii ya ONGEA ili vijana waweze kuongea na kufundishana pamoja na kupeana mipango ya kujilinda na kuwa wenye afya njema na kuonyesha mchango wao katika kutambuliwa mchango wao kwenye taifa,” alisema

 

Sambamba na hayo alihimiza programu hiyo kuhakikisha Watu wenye Ulemavu wanashirikishwa kwa karibu kulingana na aina ya Ulemavu walionao

 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alibainisha Vijana wengi hushiriki ngono katika umri mdogo kwa sababu mbalimbali ikiwemo kutokuwa na elimu rika na kufanyiwa ukatili wa kingono na watu wao wa karibu vitendo vinavyochangia kuongezeka kwa maambukizi ya VVU.

 

"Kuna sababu nyingi zinazochangia maambukizi mapya zikiwemo mila potofu, tamaa za wazazi, kuruhusu watoto kulala na wageni bila kuwafahamu vizuri, watu 98,000 wenye umri kati ya miaka 10-19 wanaishi na VVU hivyo wazazi lazima tuwajibike vizuri na kutoa nafasi watoto wasikilize vipindi hivi na kutoa maoni yao maana ndiyo wahusika," alifafanua Mkuu huyo wa Wilaya.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti na Kupambana na Ukimwi, (TACAIDS), Dkt. Leonard Maboko alisema kwa katika maambukizi mapya ya Ukimwi asilimia 40 yanatoka kwa vijana kati ya miaka 15 hadi 24 ambapo kwa mwaka 2017 maambukizi yalifika 72,000 yakijumuisha Watoto, Vijana na Wazee.

 

“Kutokana na takwimu hizi TACAIDS tuliona umuhimu wa kutoa elimu kwa umma hususan vijana na tulipokea maelekezo ya Waziri Mkuu pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Mhe. Mgahama katika kufikisha elimu kwa vijana na haya ndio matokeo ya kuanzishwa kwa programu hiyo,” alisema Dkt. Maboko

 

Vile vile Kaimu Mwakilishi Mkazi kutoka UNICEF, Daniel Baheta aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali katika kuhakikisha Vijana wanakuwa na ustawi na kuwa sehemu ya maendeleo kwa Taifa lao.

 

Naye Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Uratibu Ofisi ya Waziri Mkuu Devotha Gabriel akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu alishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto Duniani, UNICEF na TACAIDS kwa kuanzisha mradi huo utakaoleta tija kwa vijana na Taifa katika kutokomeza janga hilo la ugojwa wa Ukimwi.

 

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga,akizungumza  wakati wa uzinduzi wa Program ya Ongea hafla iliyofanyika Septemba 11,2021 Jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mtendaji wa wa Tume ya Kudhibiti na Kupambana na Ukimwi (TACAIDS) Dkt. Leonard Maboko akizungumza wakati wa uzinduzi wa Programu ya ONGEA hafla iliyofanyika Septemba 11, 2021 Jijini Dodoma.

Baadhi ya washiriki wakifatilia hotuba ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa Programu ya Ongea hafla iliyofanyika Septemba 11, 2021 Jijini Dodoma katika Hotel ya Morena.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir Shekimweri, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Program ya Ongea hafla iliyofanyika Septemba 11, 2021 Jijini Dodoma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad