HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, September 17, 2021

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar afanya mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini Tanzania


MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othaman Masoud Othman, amesema ili Zanzibar iweze kupiga hatua inahitaji kufanya mageuzi makubwa na kuweka  mfumo bora wa kusimamia nchi yakiwemo masuala ya uchaguzi na ukuzaji wa Demokrasia.

Mhe. Othman ameyasema hayo leo ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar alipozungumza na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Bw. Donald Wright.

Mhe. Makamu amesema kwamba  hatua hiyo ni muhimu kwani kutaiwezesha Zanzibar kuwa na mazingira mazuri  zaidi ya utoaji huduma na kuwavutia wawekezaji na kuifanya nchi kupiga hatua kubwa na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Amefahamisha kwamba mfumo uliopo sasa unahitaji kufanyiwa mageuzi  makubwa kwa kuwa unaifanya Zanzibar kutumia gharama kubwa katika shughuli mbali mbali likiwemo suala la usimamizi wa uchaguzi.

Amesema suhali hilo linasihusisha taasisi nyingi wakiwemo masheha na wengine ambao kisheria wamepewa mamlaka kubwa  katika mchakato wa aina hiyo jambo linahitaji kufanyiwa mapitio kwa dhamira ya ukuzaji wa demokrasia na ustawi wa serikali ya umoja wa kitaifa.

Amesema  ni muhimu Zanzibar kuwa na mfumo wenye mtazamo bora na sahihi  zaidi unaofaa kwa  mazingira sasa na baadae katika kuzingatia matakwa ya mifumo mbali mbali ya kidemokrasia iliyopo duniani.

Hata hivyo, amesema kwamba hivi sasa yapo matumaini makubwa kwamba Zanzibar itaweza kusonga mbele kiuchumi na Kidemokrasia  kutokana na kuonekana dhamira njema ya kisiasa kwa viongozi mbali mbaili wa ngazi za juu nchini.

Naye Balozi wa Marekani nchini Tanzania Bw. Dolnad Wright, amesema  nchi yake imeamua kuendelea kuiunga mkono na kuisaidia Zanzibar katika masuala mbali mbali ya kimaendeleo kutokana na kuwepo hatua kadhaa zinazochukuliwa na Serikali katika kukuza Demokrasia.

Amesema kwamba nchi yake inaunga mkono juhudi za Viongozi na Serikali kwa jumla zinazochukuliwa katika kujenga Serikali ya Umoja wa kitaifa na kwa ipo tayari kusaidia kuifanya ipige hatua.

“ Kwa kweli marekani  imevutika sana na juhudi za kujenga maridhiano ya Serikali ya umoja wa kitaifa yanayoendelea na ndio maana imeamua kurudia kuisaidia Zanzibar kuendeleza juhudi hizo” , alisema Balozi huyo. 

Balozi Dolnad amesema kwamba nchi yake ingependelea kuwepo maridhiano ya kweli ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kwamba jambo hilo ndilo linaloivutia nchi yake kurudi tena kuisaidia Zanzibar.

Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar  Mhe. Othman Masoud Othman( kulia), akizungumza na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Bw. Donald Wright. Balozi huyo alifika ofisini kwa Makamu wa Rais  kwa Mazungumzo  yaliyohusu masuala ya Maendeleo ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa na Demokrasia Zanzibar . Picha  kwa Hisani ya  Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar.
Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar  Mhe. Othman Masoud Othman( kulia) ,akisalimiana na  Balozi wa Marekani nchini Tanzania Bw. Donald Wright alipowasili ofisini kwa Makamu Migombani leo kwa Mazungumzo  yaliyohusu masuala ya Maendeleo ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa na Demokrasia Zanzibar . Picha  kwa Hisani ya  Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad