HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, June 10, 2021

Upande wa Jamuhuri wafanya mahojiano na Herbinder Seth


Mkurugenzi wa Kampuni ya Kufua Umeme (IPTL), Herbinder Seth akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo mara baada ya mahakama hiyo kuruhusu upande wa Jamhuri ufanye mazungumzo na Seth kutokana na barua alizoziandika.
Na Karama Kenyunko Michuzi TV
UPANDE wa Jamuhuri katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mkurugenzi wa Kampuni ya Kufua Umeme (IPTL), Herbinder Seth, umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ufanye mazungumzo na Seth, ili wapate ufafanuzi wa barua alizoandika kupitia wakili wake.

Hata hivyo, Mahakama imekubali ombi hilo na kuuruhusu upande wa Jamuhuri kufanya mazungumzo na mshtakiwa.

Mshtakiwa Seth peke yake ameletwa mahakamani hapo leo Juni 10, badala ya Juni 17, 2021 kama mahakama ilivyokuwa imepanga ambapo alitakiwa kuletwa pamoja na washtakiwa wenzake, James Rugemalira ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP na Wakili wa kujitegemea, Joseph Makandege, kufuatia maombi dhidi yake ya upande wa mashtaka.

Mapema wakili wa Serikali Mkuu, Martenus Marandu akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ladslaus Komanya walidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa Seth aliandika barua yeye binafsi kupitia wakili wake hivyo upande wa mashtaka umeona ni vema wakaja mbele ya Mahakama kuomba kibali cha kukutana na Seth ili waweze kuzungumza nae pamoja na wakili wake, kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa barua hizo na kile ambacho amedhamilia kwa dhati kifanyike.

Hata hivyo, upande wa utetezi haukuwa na pingamizi juu ya ombi hilo la mteja wao kufanya mazungumzo na upande wa Jamuhuri.

Aidha, Wakili Marandu ameiomba Mahakama kuipanga kesi hiyo itajwe kesho ili wapeleke mrejesho wa kile ambacho watakuwa wamezungumza.

Hakimu Shaidi ameridhia ombi hilo na kusema..., "Mtaenda kuongea kama mlivyoomba, na kesho mtaleta mrejesho, mshtakiwa utakaa mahabusu." Amesema Hakimu Shaidi.

Awali, Mahakama hiyo ilielezwaa kuwa, mazungumzo ya makubaliano ya kumaliza kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Seth yanasuburi muongozo wa Mkurugenzi mpya wa Mashtaka nchini (DPP).

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Saimon alidai, mazunguzo ya kumaliza kesi dhidi ya mshtakiwa (Seth) yanaendelea yalipoishia, ambapo wanasuburi muongozo kutoka kwa DPP mpya aliyeteuliwa hivi karibuni na rais ili waweze kuwakilisha mahakamani hapo.

"Mazungumzo yanaendelea wanasubiri mwongozo wa DPP mpya ya umaliziaji wa mazungumzo yaliyokuwa yameanza." Alidai Wankyo

Awali Seth na Wakili wa Kujitegemea Joseph Makandege waliwasilisha ombi kwa DPP wakionesha nia yao ya kutaka maliza kesi kwa kukiri makosa yao lakini, Mei 6, 2021 wakili huyo aliondoa nia yake ya kufanya makubaliano na DPP akieleza kwamba mazungumzo hayo yamechukua muda mrefu kukamilika.

Mbali na Seth na Makandegs mshtakiwa mwingine ni mfanyabiashara James Rugemalira ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP, wanadaiwa kutenda makosa hayo katika Jiji la Dar es Salaam na nchi za Afrika Kusini, Kenya na India.

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 12 yakiwemo ya utakatishaji fedha, miongoni mwa mashtaka hayo yapo ya kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu, kughushi na kutoa nyaraka za kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Washtakiwa wanadaiwa kati ya Oktoba 18 ,2011 na Machi 19, 2014 jiji Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Mwanasheria Makandege, anakabiliwa na mashtaka matano likiwemo la kuisababishia Serikali hasara ya Dola za Marekani 980,000.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad