HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, May 23, 2021

Wanahisa wa Benki ya CRDB waidhinisha Gawio la Shilingi 22 kwa hisa kufuatia ongezeko la faida kwa 37.5% mwaka 2020

Wanahisa wa Benki ya CRDB wameidhinisha gawio la shilingi 22 kwa hisa lililopendekezwa na Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo katika Mkutano Mkuu wa 26 wa Wanahisa uliofanyika kidijitali siku ya jumamosi tarehe 22 Mei, 2021. Gawio ambalo ni ongezeko la asilimi 29.4 ya gawio liloidhinishwa mwaka jana, linatokana na matokeo mazuri ya kifedha ya benki hiyo katika mwaka wa fedha 2020 ambapo ilitangaza faida baada ya kodi ya Shilingi bilioni 165.2 licha ya changamoto zilizoletwa na COVID19.

Akiwasilisha taaarifa yake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay alielezea kuwa utendaji endelevu na mabadiliko ya kimkakati yanayoendelea ndani ya benki hiyo yamesaidia kufungua uwezo wa Benki, katika kuwahudumia wateja na kusaidia kuweka mazingira mazuri ya biashara. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, utendaji wa Benki ya CRDB umeendelea kuimarika na kufanya uwekezaji wa wanahisa wake kuwa watija zaidi."Licha ya changamoto ambazo tulikutana nazo 2020, tulijidhatiti katika kuhakikisha wanahisa wetu wanapata faida kutokana na uwekezaji wao kama inavyojionyesha katika mapato kwa kila hisa. Tulipendekeza gawio la Shilingi 22 kwa kila hisa na ninafurahi kuwa julisha kuwa wanahisa wameliidhinisha, ”alisema Dk Laay.

Aliongeza: “jumla ya gawio lililopendekezwa ni Shilingi bilioni 58, ambalo linaashiria ukuaji wenye nguvu na maendeleo katika mapato kwa kila hisa na gawio kwa kila hisa. Ninapenda kuwajulisha kuwa Wanahisa wa Benki pia waliidhinisha Kampuni ya Ukaguzi wa Hesabu Ernst & Young kuwa Wakaguzi wetu wa nje wa mwaka fedha 2021, ikiashiria imani yetu katika utekelezwaji wao na kuendelea kwa Benki kufuata misingi ya utawala bora ”, alisema Dkt. Laay.

Dkt. Laay pia alibainisha kuwa katika kipindi cha mwaka jana, Benki ilipata mjumbe mpya wa Bodi, Bi. Ellen Gervas Rwijage, ambaye alijiunga na Bodi kama mwakilishi wa Mfuko wa Uwekezaji wa DANIDA (DIF), ambao una miliki hisa 21% ndani ya Benki.

Aliwaarifu pia Wanahisa kwamba Bi. Esther Kitoka, ambaye alikuwa Afisa Mkuu wa Uendeshaji aliondoka Benki na Bruce Mwile alichaguliwa kuziba nafasi hiyo. Kabla ya kuchaguliwa kwake, Bwana Mwile alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa tanzu ya Benki ya CRDB Burundi.

Wakati huo huo wanahisa wa Benki waliidhinisha mabadiliko ya katiba yaliyopendekezwa na Bodi ya Wakurugezi, na pia walipiga kura kuchagua wajumbe wawili wa bodi ambapo Prof Faustine Bee ilichaguliwa kwa mara ya pili kuwakilisha wanahisa wenye umiliki chini ya 1% na Gerald Kasatualichaguliwa kuwakilisha wanahisa wenye hisa kati ya 1% na 10%. Prof. Bee ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), wakati Gerald Kasatu ni Afisa Mkuu wa Uwekezaji katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF, Uganda.Katika taarifa yake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alibainisha kuwa mapato ya Benki ya CRDB na kampuni zake yaliongezeka sana licha ya kushuka kwa uchumi kwa sababu ya Janga la COVID-19. Mapato ya uendeshaji yalisajili ukuaji wa asilimia 10.4 kufikia Shilingi bilioni 854 kulinganisha na Shilingi 774 zilizoripotiwa mwaka uliopita.

"Mkakati wetu wa kusaidia wateja wakati wa janga hilo kwa kiasi kikubwa ulitusaidia kuboresha mipango yetu ya biashara ili kuendana na mabadiliko," alisema Nsekela. 

Nsekela pia alisema kuwa mabadiliko ambayo benki hiyo imekuwa ikiyafanya yameendelea kuleta matokeo chanya, huku akibainisha kuwa katika kipindi cha mwaka jana Benki ya CRDB iliwekeza kwa kiasi kikubwa katika mfiumo ya kidijitali. Uwekezaji huu ulipelekea kukua kwa idadi ya wateja wanaotumia njia za kidijitali, ambapo asilimia 87 ya miamala yote ilifanyika kidijitali.Kukua kwa faida ya Benki ya CRDB, kulichangiwa pia na matokeo mazuri ya kifedha ya kampuni zake tanzu, ambazo zilichangia asilimia 7 ya faida baada ya kodi kwa jumla. Kampuni tanzu ya Benki ya CRDB Burundi ilirekodi ongezeko la faida kwa asilimia 75 kutoka Shilingi bilioni 6.4 hadi Shilingi bilioni 11.2. Kwa upande wake, Kampuni tanzu ya bima, CRDB Insurance Broker Limited, ilipata faida ya Shilingi bilioni 3.6 ikiwa ni ukuaji wa asilimia 140.

Akizungumzia mipango ya baadae ya Benki ya CRDB, Nsekela alisema malengo ya muda mrefu ya Benki ya CRDB ni kujenga benki iliyo tayari siku zijazo ambayo itaongoza kwa uvumbuzi na ubunifu wa huduma bora za kifedha. Mkakati wa Benki hiyo wa mwaka 2021 unakusudia kufungua uwezo kamili wa Benki ya CRDB na kampuni zake tanzu kwa kuimarisha ufanisi wa huduma kwa wateja.

Nsekela pia alifunua kuwa Benki hiyo inaagazia kupanua wigo wa huduma zake katika masoko mapya na kwa sasa ipo katika hatua za mwisho za kufungua tawi katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema kampuni tanzu ya Benki ya CRDB DRC Congo itasaidia kuimarisha biashara kati ya ya Tanzania na nchi hiyo jirani. "Lengo letu ni kuimarisha ushiriki wa benki yetu katika kuunganisha nchi zilizopo katika Ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati na kufungua fursa za kiuchumi," aliongeza Nsekela.Akizungumza wakati wa Mkutano huo Mkuu wa Wanahisa, Mkurugenzi Mtendaji mstaafu wa Benki ya CRDB ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Vunjo na Mwanahisa wa Benki hiyo, Dkt. Charles Kimei aliipongeza menejimenti na wafanyakazi kwa kazi nzuri wanayoifanya ambayo imepelekea ukuaji mzuri katika viashiria vyote muhimu vya utendaji katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020. Aliihakikishia Bodi na Menejimenti kuwa wanahisa wana imani nao na wataendelea kushirikiana nao kikamilifu.

"Kipekee kabisa nimpongeze Mkurugenzi Mtendaji wetu Abdulmajidi Nsekela kwa kuonyesha uongozi imara, kwa kawaida ni ngumu kupata mafanikio ambayo ameyapata katikati ya janga COVID19, lakini kwa uongozi wake thabiti leo hii tunaurahia ongezeko la gawio, ”aliongeza Nsekela.

Mkutano Mkuu wa 26 wa Benki ya CRDB ulikuwa wa kihistoria ambapo kwa mara ya kwanza wanahisa walishiriki kwa njia ya mseto, ambapo wengine walihudhuria katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC). Zaidi ya wanahisa 1,400 walishiriki Mkutano Mkuu huo wa mseto baada ya mafanikio ya Mkutano Mkuu wa 25 mwaka jana.




















No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad