RC Mwanza: Watumishi zingatieni uadilifu na uzalendo mnapotekeleza shughuli za ununuzi kwenye taasisi zenu - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, May 12, 2021

RC Mwanza: Watumishi zingatieni uadilifu na uzalendo mnapotekeleza shughuli za ununuzi kwenye taasisi zenu

 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mheshimiwa John Mongela, amewataka watumishi wa Umma mkoani humo kuzingatia misingi ya uadilifu na uzalendo wakati wanaopojishughulisha kwenye michakato ya ununuzi kwenye taasisi zao ili kuwezesha kupatikana kwa thamani ya fedha kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.


Mkuu huyo wa Mkoa ametoa wito huo wakati akifungua mafunzo ya Sheria, Kanuni, Miongozo na Mifumo ya Ununuzi wa Umma kwa watendaji na watumishi wa umma kutoka taasisi zilizopo mkoani humo. Mafunzo hayo yana lengo la kuwajengea uwezo watumishi hao katika kutekeleza majukumu yao ya Ununuzi kwenye taasisi zao kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Ununuzi wa Umma.

Mhe. Mongela amesema maendeleo ya Halmashauri za mkoa huo yanategemea sana ufanisi wa watumishi hao katika kutekeleza shughuli za Ununuzi kwa kufuata Sheria na Kanuni za Ununuzi wa Umma ambazo, pamoja na mambo mengine, zinataka wadau wote wanaohusika kwenye michakato ya ununuzi kuzingatia misingi ya uadilifu na uzalendo.

“Lazima tuzingatie misingi ya uadilifu na uzalendo kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu na kuunga mkono azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Niseme tu kwamba hata kwenye Mkoa wa Mwanza, ikithibitika ukosefu wa uadilifu na uzembe wa wazi kabisa kwa watumishi wetu lazima hatua zichukuliwe dhidi yao,” alisema Mhe. Mongela.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kujenga Uwezo na Huduma za Ushauri wa PPRA, Mhandisi Mary Swai, alisema kupitia mafunzo hayo washiriki watafundishwa kuhusu matumizi sahihi ya utaratibu wa “force account” ambao taasisi nyingi za umma huutumia sana wakati huu.

“Tunafahamu kwamba utaratibu wa ‘Force Account’ umekuwa na changamoto kadhaa katika utekelezaji wake, ingawa njia hii ilianza kutumika kwa lengo zuri la kupunguza gharama. Baadhi ya changamoto ni usimamizi hafifu wa miradi unaotokana na wasimamizi kukosa ujuzi wa masuala ya ujenzi. Pia, kutowezeshwa gharama za usimamizi pamoja na kukosa uadilifu kwa baadhi ya wasimamizi,” alisema Mhandisi Swai.

Mafunzo hayo ya siku tatu yamehudhuriwa na takribani washiriki 100 wakiwemo Wajumbe wa Bodi za Zabuni, Wakuu wa Idara Tumizi (user departments, watumishi kutoka vitengo vya Usimamizi wa ununuzi, Wanasheria, na Wakaguzi wa Ndani kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Mwanza na taasisi mbalimbali za mkoa huo.

PPRA imeshaendesha mafunzo kama hayo kwenye mikoa 15 nchini, Ruvuma, Njombe, Iringa, Kagera, Shinyanga, Kigoma, Geita, Rukwa, Katavi, Tabora, Mbeya, Dodoma, Songwe, Mara na Simiyu, ambapo huu wa Mwanza ni wa 16.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongela akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya sheria na kanuni za ununuzi wa umma kwa watendaji na watumishi wa Taasisi za Umma zilizopo mkoani humo. Mafunzo hayo ya siku tatu yameendeshwa na Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA).

Picha ya pamoja kati ya Mgeni Rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongela pamoja na Wakurugenzi wa baadhi ya Halmashauri za Wilaya zilizopo ndani ya Mkoa wa Mwanza


Bw. Bernard Costantine, ambaye ni Mtaalam wa Mifumo ya Habari wa PPRA akiwasilisha mada kuhusu matumizi fasaha ya Mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Mtandao (TANePS) kwa washiriki


Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw. Emil Kasagara akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo

Picha ya pamoja kati ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongela (katikati waliokaa) pamoja na Kaimu Katibu Tawala wa mkoa huo Bw. Emil Kasagara (kushoto waliokaa), Mkurugenzi wa Kujenga Uwezo na Huduma za Ushauri wa PPRA, Mhandisi Mary Swai. Mstari wa nyuma waliosimama ni wawezeshaji wa mafunzo hayo kutoka PPRA
 Mkurugenzi wa Kujenga Uwezo na Huduma za Ushauri wa PPRA, Mhandisi Mary Swai, akifundisha washiriki wa mafunzo hayo .

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad