HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, April 27, 2021

WAZIRI CHAMURIHO ATOA MAAGIZO KIWANJA CHA NDEGE IRINGA

 

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho, ameitaka Kampuni ya kikandarasi ya SinoHydro Corporation kutoka China kuhakikisha kuwa wanakamilisha kazi ya ukarabati wa Kiwanja cha ndege cha Iringa kwa muda uliopangwa ili kuruhusu ndege kubwa kuweza kutua katika kiwanja hicho.

“Kama mnavyoona, sasa hivi huduma ya ndege ya ATC imesimama kwa sababu ya ukarabati huu, hakikisha Mkandarasi unatekeleza kazi hii kwa haraka kama mkataba unavyosema, wananchi wa hapa wanasubiria kwa hamu Kiwanja hiki”, amesema Chamuriho.

Aidha, amemtaka Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Iringa, Mhandisi, Kindole Daniel, kukaa na Mkandarasi huyo kuona namna ya kuunganisha awamu mbili za ukarabati kama zilivyoainishwa na Mkandarasi ili kukamilisha mapema kazi hiyo.

Amesisitiza kwa Meneja huyo kuhakikisha kuwa, wananchi wa maeneo jirani ya mradi huo wanapata ajira ili waweze kunufaika na mradi huo, pia kuweka matangazo kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuhusu ajira za kitaalamu ambazo zinatolewa na Mkandarasi huyo ili wataalamu wazawa nao kuweza kuomba nafasi hizo.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Iringa, Mhandisi, Kindole Daniel, amesema kuwa mradi wa ukarabati wa Kiwanja cha ndege cha Iringa unahusisha matengenezo makubwa ya njia ya kuruka na kutua ndege ya sasa yenye kiwango cha lami nyepesi, ujenzi wa eneo la usalama, njia ya michepuo ya ndege, maegesho mapya ya ndege, jengo la muda la abiria na mnara wa muda wa kuongozea ndege.

Ameongeza kuwa, mradi huu pia unahusisha ujenzi wa jengo la zimamoto, ujenzi wa jengo la kituo cha nishati na kuweka taa za ardhini kwenye njia ya kuruka na kutua ndege.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Iringa ameomba ujenzi huo ufanyike kwa awamu moja ili uishe haraka kwani wananchi wa Mkoa huo wanapata tabu kwa sasa kutokana na Kiwanja hicho kupokea ndege ndogo pekee.

Mradi wa Ukarabati wa Kiwanja cha ndege cha Iringa, ulisainiwa mwezi Mei mwaka jana, ambapo Ukarabati wake unahusisha kazi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa njia ya kuruka na kutua ndege kutoka urefu wa kilometa 1.6 hadi kufikia kilometa 2.1 na hivyo kupelekea hata ndege za masafa ya kati kuweza kutua kwa urahisi pindi ukarabati huo utakapokamilika.



Kazi ya Ukarabati wa Kiwanja cha ndege cha Iringa ikiendelea. Ukarabati huu unahusisha matengenezo makubwa ya njia ya kuruka na kutua ndege ya sasa yenye kiwango cha lami nyepesi, ujenzi wa eneo la usalama, njia ya michepuo ya ndege, maegesho mapya ya ndege, jengo la muda la abiria na mnara wa muda wa kuongozea ndege.



Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho, akitoa maelekezo kwa wakandarasi wa Kampuni ya SinoHydro Corporation Limited kutoka China wakati Waziri huyo alipotembelea mradi wa Ukarabati wa Kiwanja cha ndege cha Iringa kujionea maendeleo yake.



Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Iringa, Kindole Daniel akielezea jambo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho (WaTatu kushoto mbele) wakati Waziri huyo alipotembelea mradi wa Ukarabati wa Kiwanja cha ndege cha Iringa kujionea maendeleo yake.



Msimamizi wa mradi wa Ukarabati wa Kiwanja cha ndege cha Iringa, kutoka Kampuni ya SinoHydro Corporation Limited ya China, Yuan Rui, akionesha mchoro wa picha ya mradi huo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho (WaPili kushoto) wakati Waziri huyo alipotembelea mradi huo kujionea maendeleo yake.PICHA NA WUU


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad