HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, April 12, 2021

WALIMU MWANGA WAPONGEZWA KWA KUFANYA KAZI KWA NIDHAMU NA WELEDI



Na Adili Mhina

Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) imewapongeza walimu wa Wilaya ya Mwanga kwa kuendelea kufanya kazi kwa weledi na nidhamu licha ya changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Pongezi hizo zimetolewa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi wa Idara ya Ajira, Maadili na Maendeleo ya walimu kutoka TSC, Christina Hape alipofanya ziara wilayani hapo kwa lengo la kukutana na kuzungumza na walimu juu ya masuala mbalimbali ya kiutumishi.

Hape alieleza kuwa TSC inatambua changamoto mbalimbali za wilaya hiyo ikiwemo upungufu wa walimu pamoja na shule nyingi kuwa maeneo ya mbali ambapo miundombinu na huduma mbalimbali bado hazijafika.

Aliongeza kuwa, licha ya changamoto hizo, walimu wa wilaya hiyo wamekuwa mfano wa kuigwa kutokana moyo wa kufanya kazi kwa bidii na kwa nidhamu, kitu kinachofanya Mkoa wa Kilimanjaro kuendelea kuwa miongoni mwa mikoa inayofanya vizuri kitaaluma.

“Kwa kweli Mwanga mnajitahidi kufanya vizuri, tunatambua kuwa yapo maeneo ya milimani ambayo hata kufikika kwake ni changamoto. Nimeelezwa kuwa hata kufika hapa kwenye mkutano huu wapo baadhi yenu mliolala kwenye magari ili muweze kuwahi”, alisema Hape.

Aliongeza kuwa, “pamoja na changamoto hizo mmeendelea kufanya kazi kwa kujituma na kwakweli hata kule makao makuu hatujapokea rufaa nyingi zinazohusu utovu wa nidhamu kwa walimu wa mwanga, naomba niwapongeze sana kwa hilo.”

Mkurugenzi Hape alifafanua kuwa, suala la upungufu wa walimu sio la wilaya hiyo peke yake bali maeneo mengi ya nchi kuna upungufu wa walimu na tayari serikali imeamua kuchukua hatua za haraka ili kukabiliana na tatizo hilo.

 “Mtakumbuka kuwa hivi karibuni Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan alizungumzia suala la upungufu wa walimu na kuagiza suala hilo tulishughulikie kwa haraka. Vilevile, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu naye amesisitiza kuwa hataki kuona shule yenye walimu wawili au watatu,” alisema Hape.

Aliongeza kuwa maagizo ya viongozi hao kuhusu kutatua changamoto ya upungufu wa walimu inaifanya TSC pamoja na mamlaka nyingine zinazohusika kuchukua hatua za haraka kuhakikisha walimu wanaajiriwa ili kujaza maeneo yenye upungufu.

Pamoja na hayo, Mkurugenzi huyo alipongeza ushirikiano uliopo kati ya ofisi ya TSC wilaya pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mwanga na kusema kuwa ushirikiano huo ndiyo unaofanya walimu wafanye kazi kwa moyo, nidhamu na weledi.

“Nishukuru ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji pamoja na ofisi ya TSC wilaya kwa kuwa mnafanya kazi kama timu moja, hakuna mivutano. Kaimu Katibu wa TSC, Maafisa Elimu pamoja na Maafisa Utumishi mnazungumza lugha moja katika kutatua kero za walimu. Hii imefanya hata katika masuala ya kupandisha madaraja sijasikia malalamiko kuwa kuna mwalimu amesahaukika,” alisema Hape.

 Akitoa taarifa fupi ya utendaji wa TSC wilayani hapo, Kaimu Katibu Msaidizi wa TSC wilaya ya Mwanga, Catherine Kimaro alisema kuwa, wilaya hiyo ina jumla ya walimu 1120 wanaofundisha shule za Serikali. Katika idadi hiyo, walimu 558 ni wa shule za msingi na 562 ni wa shule za sekondari.

Kimaro alieleza kuwa, wilaya hiyo kwa sasa haina shauri lolote la nidhamu kutokana juhudi za ofisi yake za kutoa elimu kwa walimu mara kwa mara  kuhusu  miiko na maadili ya utendaji wa kazi.

Mmoja wa walimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga akitoa maoni ya masuala ya utumishi wa walimu wakati wa kikao.
Mmoja wa walimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga akiuliza swali wakati wa kikao.
Baadhi ya walimu na wathibiti ubora wa shule wa Wilaya ya Mwanga wakiendelea kufuatilia hotuba ya Mkurugenzi wa Idara ya Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC makao makuu, Christina Hape (hayupo pichani).
Mwakilishi wa Afisa Elimu Wilaya ya Mwanga, Hilda Sindato akitoa salam wakati wa kikao kilichowakutanisha Walimu wa wilaya hiyo na Mkurugenzi wa Idara ya Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC makao makuu.
Kaimu Katibu Msaidizi wa TSC Wilaya ya Mwanga, Catherine Kimaro akitoa taarifa fupi ya utendaji kazi wa ofisi yake wakati wa kikao cha walimu na Mkurugenzi wa Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC kilichofanyika mwishoni mwa wiki wilayani Mwanga.
Mkurugenzi wa Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Christina Hape akitoa hotuba yake kwenye kikao cha walimu wa shule za msingi na sekondari wa Wilaya ya Mwanga. Kikao hicho lichofanyika mwishoni mwa wiki katika shuke ya sekondari Mwanga.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad