DKT. NCHEMBA: TUTABORESHA MASUALA YA KODI NA KUSIMAMIA MATUMIZI YA SERIKALI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, April 6, 2021

DKT. NCHEMBA: TUTABORESHA MASUALA YA KODI NA KUSIMAMIA MATUMIZI YA SERIKALI

 
Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam

WAZIRI wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amewahakikishia wafanyabiashara hapa nchini kuwa Wizara yake itahakikisha inarejesha taswira na mahusiano mazuri nao katika masuala yakodi ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na kusisimua uchumi wa nchi.

Dkt. Nchemba alitoa ahadi hiyo Ikulu Jijini Dar es Salaam alipozungumza na vyombo vya habari baada ya tukio la kuapishwa kwa Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu pamoja na viongozi wa Taasisi, tukio lililofanywa na Rais wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

“Tutatengeneza vyanzo vipya vya makusanyo ili mzigo wa kodi usibebwe na wachache kwa sababu kadri mzigo unavyobebwa na wengi ndivyo nafuu inavyopatikana, hatua itakayowafanya wafanyabiashara wengi kulipa kodi kwa hiari” alieleza Dkt. Nchemba

Aidha, Dkt. Nchemba aliyeanza kazi hivi karibuni kama Waziri wa Fedha na Mipango, alisema kuwa amekutana na wataalam wa Wizara yake na kuwaagiza wakutane na wenzao wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili kujadili namna ya kutatua changamoto za Muungano na kwamba anaamini zitapatiwa ufumbuzi.

“Shida ya watu wetu wengi wanapojadili masuala haya hawatuambii walipokwama, kwahiyo niliwaambia watubainishie wanapokwama ili tupate ufumbuzi wa jambo hilo baada ya hapo tutakaa Wizara tatu, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar na Ofisi ya Makamu wa Rais na kufanya uchambuzi wa kina” Alifafanua Dk. Nchemba

Kuhusu udhibiti wa matumizi wa Fedha za Umma, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alisema kuwa Wizara yake itatumia mifumo ya fedha iliyobuniwa kudhibiti matumizi ya Serikali na kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato ili iwe michache lakini yenye ufanisi pamoja na kuimarisha masuala ya utawala katika kukusanya mapato na matumizi yake ili fedha hizo zilete matokeo yaliyokusudiwa.

Waziri wa Fedha na Mipango alishuhudia kuapishwa kwa watendaji wake wapya, akiwemo Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Khatibu Kazungu ambao wameapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mher. Samia Suluhu Hassan, Ikulu, Jijini Dar es Salaam. 

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, akizungumza na vyombo vya habari akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kuhusu kodi, masuala ya muungano na udhibiti wa fedha za umma, mara baada ya kuapishwa kwa Makatibu wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, na Viongozi wa Taasisi mbalimbali Ikulu Jijini Dar es Salaam, tukio lililofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan. (Picha na Wizara ya Fedha na Mipango- Dar es Salaam)
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango anayesimamia Fedha za Nje Bi. Amina Khamisi Shaabani, akimpongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba, mara baada ya kula kiapo mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Ikulu Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu Mpya wa Wizara yake ambaye pia ni Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Emmanuel Tutuba (wa tatu kulia) na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Adolf Ndunguru (kushoto) pamoja na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga ambaye hapo awali alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango (Utawala).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad