MAMLAKA ya maji safi na usafi wa mazingira Manispaa ya
Songea(Souwasa),imekamilisha ujenzi wa miradi miwili ya maji kwa
mafanikio makubwa katika vijiji vya Mhilo na Kipapa katika Halmashauri
ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.
Kukamilika kwa miradi hiyo kumemaliza kero ya muda mrefu ya upatikanaji
wa maji safi na salama kwa wananchi wa vijiji hivyo ambao kabla ya
ujenzi wa miradi hiyo, walilazimika kutumia maji ya visima vya asili
vilivyochimbwa kienyeji na wengine kwenda mtoni kuchota maji ambayo
hayakuwa safi na salama.
Meneja ufundi wa Souwasa Jafari Yahaya alisema, Serikali imetoa jumla
ya shilingi milioni 772 ili kujenga miradi yote mwili iliyohusisha
ujenzi wa matenki, miundombinu mbalimbali na vituo vya kuchotea maji
vilivyojengwa katika makazi ya watu na kwenye taasisi za umma.
Akizungumzia mradi wa Kipapa Jafari alisema, serikali kupitia wizara ya
maji imetoa shilingi milioni 569 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu
na kuboresha huduma ya maji ambapo kati ya hizo, tayari imetoa
milioni 444 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo.
Alisema, kazi zilizopangwa na zilizofanyika ni ujenzi wa chanzo,ujenzi
wa tenki la kusambazaji maji,usambazaji wa bomba za kusafirishia na
kusambaza maji na kujenga vituo 23 vya kuchotea maji.
Kwa mujibu wake,kazi zimekamilika kwa asilimia 98 na wananchi wanapata
huduma ya maji safi na salama, isipokuwa ujenzi wa uzio ambao
hajakamilika na unaendelea kujengwa.
Aidha katika mradi wa Muhilo Jafari alisema, Serikali imetoa shilingi
milioni 203 na kazi zilizofanyika ni ujenzi wa tenki wa lita 50,000 na
shughuli nyingine ambapo wakazi 1,247 wamenufaika na mradi huo.
Aliongeza kuwa, serikali imetoa fedha hizo kwa ajili ya kuboresha
huduma ya maji kwa wananchi wa maeneo hayo ili watumie muda mwingi
kufanya shughuli za maendeleo, badala ya kupoteza muda wao kwenda
kutafuta maji mbali na makazi yao.
Alisema, miradi yote ipo chini ya wakala wa maji safi na usafi wa
mazingira vijijini(Ruwasa) mkoa wa Ruvuma na Souwasa ilipewa kazi ya
kujenga kama fundi.
Jafari alisema, miradi yote imekamilika kwa asilimia 98 na sasa
wananchi wanapata huduma ya maji katika maeneo yao pamoja na taasisi za
serikali kama shule na zahanati na kuishukuru Ruwasa kwa kwa kuwaamini
na kuwapa kazi ya Ujenzi wa miradi hiyo.
Manfred Nchimbi(56) mkazi wa Kipapa alisema, awali walilazimika kuamka
saa 9 usiku na kutembea umbali wa km 3 kwenda kutafuta maji, lakini
sasa kero hiyo imemalizika na kuishukuru serikali kupitia wizara ya
maji kutekeleza mradi huo ambao umemaliza kabisa mateso ya muda mrefu.
Alisema, kabla ya kujengwa kwa mradi huo na wakala wa usambazaji maji
safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) chini ya fundi Mamlaka ya
maji safi na usafi wa mazingira Songea(Souwasa) walitumia maji kutoka
katika vyanzo visivyo rasmi lakini havikutosheleza mahitaji yao.
Kanisia Komba mkazi wa kijiji cha Mhilo,mbali na kuishukuru serikali
kwa kupeleka huduma ya maji katika kijiji hicho alisema, maji hayo
yamerudisha na kuboresha mahusiano na kuimarika ndoa zao.
Alisema, baadhi ya ndoa zimevunjika kwa sababu ya akina mama kuchelewa
kurudi nyumbani kutoka kutafuta maji, hivyo wanaume kudhani walikuwa
kwenye michepuko(nyumba ndogo) jambo ambalo lilichangia ndoa nyingi
kuvunjika na kusambaratika kwa familia.
Monday, March 8, 2021

Home
Unlabelled
ML 700 ZAMALIZA KERO YA MAJI KIPAPA NA MHILO
ML 700 ZAMALIZA KERO YA MAJI KIPAPA NA MHILO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment