HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, February 26, 2021

TRA YAWATOA HOFU WAFANYABIASHARA MKOANI GEITA KUHUSU KODI YA ONGEZEKO LA THAMANI

 Na. Mwandishi wetu-Geita

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imewatoa hofu wafanyabiashara kuhusiana na suala la Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Kauli hiyo imetolewa mjini Katoro mkoani Geita na Afisa Msimamizi Kodi Mwandamizi wa TRA, Bw. Lutufyo Mtafya wakati akiongea na baadhi ya wafanyabiashara ambao walitaka kujua uhalisia kuhusu suala la VAT.

Mtafya amesema kwamba, TRA imebaini kuwa baadhi ya wafanyabiashara wamekua na hofu kwamba VAT hutozwa asilimia 18 kwenye mauzo wakati kiuhalisia kodi hiyo hutozwa kwenye ongezeko la thamani.

Bw. Mtafya amefafanua kwamba, mtu akifanya manunuzi analipia VAT ambayo ni asilimia 18, na anapouza bidhaa hizo hukusanya VAT hivyo, tofauti kati ya kiasi alicholipa wakati ananunua na kile anachokusanya wakati anauza ndicho humfanya alipe kodi ya ongezeko la thamani, kwa mantiki hiyo mlaji wa mwisho ndiye anayelipa kodi hiyo.

“Kitu ambacho baadhi ya wafanyabiashara walikua hawajui ni kwamba, katika ongezeko la thamani endapo mtu akinunua bidhaa kwa shilingi milioni moja na akiuza bidhaa hizo kwa shilingi milioni moja na laki moja basi ongezeko la thamani hapo ni shilingi laki moja, hivyo asilimia 18 itatozwa katika shilingi laki moja, kiasi hicho kidogo hulipwa na mlaji na sio mfanyabiashara”, alisema Mtafya.

Ameongeza kuwa, kwa mfanyabiashara yeyote aliyesajiliwa kwenye mfumo wa VAT anatengeneza hesabu, hivyo mapato ghafi ambayo yanapatikana kwenye biashara yake yanahesabika bila kuweka gharama za kodi ya ongezeko la thamani.

“Tunaondoa asilimia 18 aliyokusanya na ile tofauti inabaki kama mauzo yake kwa mwaka tofauti na wafanyabiashara wengine ambao hawajasajiliwa na VAT, kiasi chote cha mauzo ghafi huhesabika kama kiasi mapato ghafi kwenye biashara yake”, alisema Mtafya.

Kwa upande wao baadhi ya wafanyabiashara wa eneo la Katoro wameipongeza TRA kwa kuwapatia elimu ya kodi kwa kuwapitia katika sehemu zao za biashara na kuomba zoezi hilo liwe endelevu kwa ajili ya kuongeza makusanyo ya kodi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Bw. Hassan Mpunga ambaye ni mfanyabiashara wa duka la kuuza spea za pikipiki anaeleza kuwa wameipokea kwa mikono miwili kampeni ya elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango kwa kuwa wengi wao hawajawahi kupatiwa elimu hiyo kwa kufuatwa madukani.

“TRA wamefanya kitu kizuri kwa kutupatia elimu ya kodi kwasababu ukweli ni kwamba, sisi baadhi ya wafanyabiashara wa Katoro hatuna elimu ya kodi na wengi wetu tukiona maafisa wa TRA tu wanapita madukani kwetu tunakimbilia kufunga maduka tukidhani wanakuja kutukagua na kufunga maduka au kuchukua mali zetu kumbe tunakosa elimu kama hii”, alisema Hassan Mpunga.

Naye Bw. Nkwabi Sylvester anaeleza kuwa, moja ya kitu kikubwa alichojifunza katika kampeni hiyo ni kuhusu umuhimu wa kuwa na mashine ya kodi ya kielektroniki (EFD) na kutunza kumbukumbu za biashara yake ili aweze kukadiriwa kodi stahiki.

“Mimi nilichojifunza kikubwa katika zoezi hili wanalofanya watu wa TRA ni suala la kuwa na mashine ya EFD na kutunza kumbukumbu za biashara yangu, na mwanzo nilikua naona hasara kununua mashine kwasababu sikujua kuwa ile gharama ya kununua mashine kumbe baadaye inakuja kurudishiwa kupitia kodi yangu niliyokadiriwa kwa mwaka husika”, alisema Nkwabi.

Kampeni ya Elimu kwa Mlipakodi ya Mlango kwa Mlango mkoani Geita ni mwendelezo wa azma ya TRA ya kuhakikisha kuwa, wafanyabiashara nchini wanapatiwa elimu juu ya masuala mbalimbali ya kodi na kutatua kero zao mbalimbali. Aidha, Kampeni hiyo mkoani hapo ilianza tarehe 22 Februari na inatarajiwa kukamilika tarehe 3 Machi mwaka huu.
Afisa Msimamizi wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Godfrey Kumwembe (kulia) akitoa elimu ya kodi kwa mfanyabiashara wa duka la vifaa vya pikipiki katika eneo la Katoro mkoani Geita wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea mkoani humo.
Afisa Msimamizi Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), BI. Joyce Ng'oja(kulia) akimuelimisha mfanyabiashara wa duka la vifaa vya umeme kuhusu umuhimu wa kutoa risiti za EFD kwa wateja wake katika eneo la Katoro mkoani Geita wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea mkoani humo.
Afisa Msimamizi Kodi Mwandamizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Lutufyo Mtafya (kushoto) akitoa elimu ya kodi kwa mfanyabiashara wa duka la vitenge katika eneo la Katoro mkoani Geita wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea mkoani humo.
Afisa Msimamizi Kodi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bi. Rose Mahendeka (kulia) akimuelimisha mfanyabiashara wa duka la viatu kuhusu umuhimu wa kafanya makadirio ya biashara mapema katika eneo la Katoro mkoani Geita wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea mkoani humo.PICHA ZOTE NA TRA

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad