HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, February 13, 2021

TAMWA ZANZIBAR YATAKIWA KUTATHIMINI MCHANGO WA WANAWAKE VIONGOZI




Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mhe. Salama Mbarouk Khatib (wapili kutoka kulia), mratibu wa TAMWA ZNZ ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said, (wakwanza kutoka kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na wanaume mawakala wa mabadiliko mara baada ya kumalizika kwa kikao.  



TAMWA, ZANZIBAR

MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Salama Mbarouk Khatib, amekishauri Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kujikita katika ufanyaji wa tafiti zenye lengo kutathimini mchango wa viongozi wa wanawake waliowahi kushika nafasi za uongozi katika ngazi mbalimbali Zanzibar ili zitumike kama mfano kwa wanawake wengine kuhamasika kujiingiza katika nafasi sizo.

Akizungumza wakati wa kikao chake na Wanaume mawakala wa mabadiliko chenye lengo la kujadili na kuwakumbusha viongozi kuhusu umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika nafasi ya uongozi chini ya TAMWA Zanzibar, mkuu huyo wa Mkoa alisema iwapo tafiti zitafanyika zitasaidia kuionesha jamii kuhusu uwezo walionao wanawake katika uongozi.

Alisema kuwa ipo mifano mbalimbali ya wanawake waliowahi kushika nafasi za uongozi na kuzitumikia kwa mafanikio makubwa na kudai kuwa kama TAMWA Zanzibar itafanya tafiti hizo kwa kina itarejesha hamasa kwa wanawake wengine kuiga mifano hiyo.

“Nikuombeni sana TAMWA ikiwezekana tufanye utafiti, na mimi ofisi yangu ipo tayari kabisa kuungana nanyi kufanikisha hilo ili tutathimini na tutambue mchango wa wanawake waliowahi kushika nafasi za uongozi katika ngazi mbalimbali hapa Zanzibar. Tukifanyiwa tafiti hizi tunaweza kuoneshwa kwamba katika ngazi ya maamuzi ya uwaziri basi waziri fulani alifanya vizuri zaidi,” alisema.

Alifafanua kuwa kufanya hivyo kutasaidia kuwanadi wanawake wengine waonekane kwamba wana uwezo wa kufanya kazi, uwezo wa kutoa maamuzi na uwezo wa kusimamia majukumu yao wanayopewa.

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa serikali imedhamiria kuzingatia usawa wa ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi kuanzia ngazi ya shehia hadi Taifa ili kuwaandaa na kuwajenga kuwa viongozi bora kuanzia ngazi za chini.

Alisema, “Ni kweli kwamba bado kunahitajika juhudi za kuendelea kuwajenga wanawake kuhusu dhana ya uongozi na maadili yake, ndio maana hata Serikali ya awamu ya Nane chini ya Rais, Mhe. Dk. Hussein Mwinyi imeanza kwa kuweka kipaumbele kwa wanawake katika nafasi mbalimbali, mfano mimi mwenyewe ni mwanamke na nashukuru Mhe. Rais ameniamini na kunipa nafasi hii na hii ni kuonesha ni namna gani serikali inatambua na kuthamini ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi.”

 

Hata hivyo Bi. Salama amebainisha kuwa changamoto inayochelewesha ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi ni kuwepo kwa misimamo ya kidini jambo linalotokana na  kukinzana kwa tafsiri juu ya mwanamke na uongozi na kuwataka wanaume mawakala wa mabadiliko kuendelea kutoa elimu kwa viongozi wa dini zote ili kuhakikisha kunakuwa na ufahamu sawa wa wanawake katika uongozi.

“Mimi mwenyewe nafahamu zana nzima ya kuwa na ukombozi wa wanawake katika nafasi mbalimbali. Wanawake wanataka wajitokeze lakini mifumo bado inawapelekea wasiende kugombea nafasi hizo kutokana na kutofautiana kwa tafsiri ya maandiko juu ya wanawake na uongozi hivyo nikuombeni tuendelee kutoa elimu kwa viongozi wa dini mbalimbali ili kuona jamii inatambua umuhimu wa wanawake kushiriki kwenye uongozi,” alisema.

Mwenyekiti wa wanaume mawakala wa mabadiliko, Suleiman Massoud Said alipongeza utendaji kazi wa mkuu huyo wa mkoa na kusema kuwa kwa kipindi chote ameendelea kuwa ni kiongozi mwanamke wa kuigwa kutokana na uchapa kazi wake.

Alisema, “sisi tunakupongeza sana kwa utendaji kazi wako kwani umeendelea kuwa ni mfano wa kuigwa kwa wanawake wenye ndoto za kuwa viongozi kutokana na juhudi na uimara wako katika utendaji kazi na hii inaashiria ni kwa namna gani wanawake wanao uwezo mkubwa wa kuongoza kama wakipewa fursa.”

Aliongeza kuwa mawakala hao wa mabadiliko wataendelea kufanya kazi kwa ukaribu na ofisi ya mkoa huo ili kuona kwamba jamii inabadili fikra na kumchukulia mwanamke kama mtu mwenye uwezo wa kupewa nafasi ya maamuzi kama wanaume.

Mapema mratibu wa TAMWA Zanzibar ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said, alisema TAMWA ZNZ itaendelea kufanya juhudi za kuelimisha jamii kuhusu dhana ya uongozi kwa wanawake lengo ilikiwa ni kuongeza idadi ya wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi na siasa.

Kikao hicho cha Mkuu wa Mkoa na wanaume mawakala wa mabadiliko ambao wamewezeshwa na TAMWA Zanzibar ni mwendelezo wa juhudi za Chama hicho kutetea na kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi na Siasa.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad