Kwa
muda mrefu wakazi wa maeneo hayo hawakuwa na usafiri wa uhakika na hiyo
iliwalazimu kutumia boti ndogo na majahazi kwa ajili ya kusafirishia
mizigo na abiria na hivyo kuhatarisha maisha yao baharini endapo
ingetokea dharura ya ajali.
Kivuko hicho kipya kilichogharimu
shilingi Bilioni 5.3 mpaka kukamilika kwake na ambacho ujenzi wake
umegharamiwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani, kimejengwa na
kampuni ya kizalendo ya Songoro Marine Transport Boatyard ya jijini
Mwanza katika karakana yake ya kujengea na kukarabati vivuko iliyopo
Kigamboni jijini Dar es salaam na kina uwezo wa kubeba abiria 200 na
magari 10 ambazo ni sawa na tani 100.
Akizungumza katika hafla
fupi ya kupokea kivuko hicho iliyofanyika katika kisiwa cha Mafia na
kuhudhuriwa na viongozi kadha wa kadha wa mkoa huo, mgeni rasmi, Mkuu wa
Mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo aliipongeza Serikali ya
Awamu ya Tano kwa kuweza kutoa fedha zote hizo kwa ajli ya kuhudumia
wananchi wake na pia aliupongeza Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kwa
kuweza kusimamia ujenzi wa Kivuko hicho hadi kukamilika kwake.
‘’Kama
mlivyosikia katika hotuba zilizotangulia Wakala umekamilisha miradi ya
ujenzi wa vivuko vipya vya Kayenze – Bezi, Bugolora - Ukara na Chato –
Nkome na kufanya vivuko vipya vilivyonunuliwa katika mwaka wa fedha
2019/20 kuwa vinne kikiwepo hiki cha Kilindoni tunachokipokea leo kwa
pamoja vikiwa vimegharimu jumla ya Shilingi bilioni 15.3. Haya yote ni
matunda ya kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Serikali ya awamu ya tano
chini ya Jemedari wetu Mheshimiwa Dr. John Joseph Pombe Magufuli, rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’’
Alisema
Mheshimiwa Ndikilo ambapo aliongeza kuwa kwa kuwa Kivuko hicho ni
rasilimali muhimu ya Taifa na kinahitajiwa na wananchi wa Mafia na
Nyamisati, aliuagiza Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kusimamia kwa
karibu uendeshaji wake ili wananchi wafaidi matunda mazuri ya Serikali
yao kwa fursa ya maendeleo yao binafsi na nchi nzima kwa ujumla wake na
pia aliwasisitizia wananchi wa Mafia na Nyamisati kukitunza kivuko hicho
na kuwapa ushirikiano wa kutosha wahudumu wake kiweze kuwahudumia kwa
kipindi kirefu.
Naye mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi
Arch. Elius Mwakalinga, Mhandisi Elizabeth Manzi akizungumza katika
hafla hiyo, amesema ni dhamira ya Serikali kutaka kutoa huduma iliyo
bora yenye kukuza uchumi wa nchi ya Tanzania na Katika mwaka wa fedha
2019/20, Serikali ilitoa jumla ya Billioni 12,245,214,800.00 kwa ajili
ya miradi ya vivuko na maegesho ambayo inatekelezwa na Wakala wa Ufundi
na Umeme na Fedha hizo zinatokana na Mfuko Mkuu wa Serikali na Mfuko wa
Barabara.
Awali,
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y.
Maselle, akisoma taarifa fupi ya ujenzi wa kivuko hicho alisema, kazi ya
ujenzi huo imefanywa kulingana na viwango vinavyokubalika Kimataifa
(IMO Standards).
‘’Kivuko
hiki kimefanyiwa ukaguzi wa mwisho kabla ya kuanza kazi na Shirika la
Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) ambao walikuwa wakishiriki ukaguzi
wakati wa ujenzi ili kuthibitisha viwango vya usalama wa abiria, magari
na mizigo.’’ Alisema Mhandisi Maselle ambapo aliongeza kuwa baada ya
ukaguzi wa mwisho TASAC wamefanya usajili wa kivuko hiki kabla
hakijaanza kazi kwa jina la MV KILINDONI – HAPA KAZI TU.
‘’Ili
kuhakikisha usalama wa kivuko hiki kinapofanya kazi kimefungwa vifaa
stahiki vya kuongozea kama vile Radar, GPS, Echo Sounder, vifaa vya
mawasiliano (Communication equipment) na vifaa vya uokoaji vya kutosha
kwa watu wazima na watoto ambavyo ni makoti ya kujiokoa (life jackets)
na maboya (life rafts na life buoys).’’ Alimaliza Mtendaji Mkuu ambapo
alishukuru Serikali kwa kuendelea kuuamini Wakala katika kutekeleza
miradi hiyo na pia kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya miradi ya vivuko
kwa lengo la kuboresha huduma za usafirishaji katika maeneo mbalimbali
nchini na kuahidi kukitunza kivuko hicho kwa kukifanyia matengenezo kama
inavyotakiwa ili kiweze kudumu na kutoa huduma bora kwa wananchi kwa
wakati wote.
Kukamilika
kwa ujenzi wa kivuko cha MV. KILINDONI HAPA KAZI TU kunafanya idadi ya
vivuko kote nchini kufikia 33 hadi hivi sasa na hivyo kuifanya serikali
kuendelea kuboresha miundombinu ya usafiri kwa manufaa ya wananchi
wengi.
No comments:
Post a Comment