Serikali Kufuta Kodi za Kemikali Viwanda vya Ngozi - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, February 12, 2021

Serikali Kufuta Kodi za Kemikali Viwanda vya Ngozi

Na Immaculate Makilika - MAELEZO 
 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli  amesema kuwa Serikali itashughulikia na kufuta  kodi inayotozwa katika kemikali zinazotumikakuondoa manyoya kwenye ngozi wakati wa uchakataji wa ngozi. 
 
Rais Magufuli ameyasema hayo leo mkoani Morogoro, wakati akifungua kiwanda cha ngozi cha Ace Leather Tanzania Limited kilichopo Kihonda  mkoani  Morogoro. 
 
“Kemikali zinazotumika kuondoa manyoya ili ngozi iwe kwenye ubora hii tutashughulikia kama Serikali, Wizara ya Viwanda mkafanyie kazi ili hizi kemikali zinazokuja kwenye viwanda vya ngozi tu tuzifutie kodi ili waweze kuchakata ngozi zetu. Kuna ng’ombe zaidi ya milioni 34,  mbuzi zaidi ya milioni 21 ngozi zote hizi,  hata samaki  Sangara wa Mwanza wana ngozi na zinatumika kutengenezea viatu”, alisema Rais Magufuli.
 
 Kuhusu malighafi za ngozi kuuzwa nje ya nchi, Rais Magufuli alisema kuwa ukiwa na kiwanda hautauza malighafi nje, ukifanya hivyo maana yake umesafirisha ajira na fedha kwa watakaoenda kuchakata nje ya nchi. 
 
“Suala la vibali kwa wanaosafirisha ngozi ghafi nje ya nchi  hilo linaweza kufanyiwa kazi na Wizara ya Mifugo,  mnawatoza asilimia 80, watozeni asilimia 100 ili waache kusafirisha ngozi ghafi nje ya nchi hiyo inaweza ikawa njia ya kuzuia watu wasipeleke ngozi ghafi nje kwa kuwa viwanda vipo na uwezo wa kuchakata ngozi upo”, alisisitiza Rais Magufuli. 
 
Aidha, Rais Magufuli alimpongeza, Rostam Aziz,  Mwekezaji wa kiwanda cha Ace Leather Tanzania Limited kwa kuanzisha kiwanda hicho ambacho  kitazalisha ajira 1,000 na kumtaka kuzingatia maslahi ya wafanyakazi pamoja na vifaa. 
 
Sambamba na hilo, Rais Magufuli ameitaka benki ya CRDB kuhakikisha  kiwanda cha Canvas  kinaanza  kufanya kazi. Vilevile Rais Magufuli aliitaka Wizara ya Fedha kuhakikisha kiwanda cha Moproco kinafanya kazi. 
 
“Nazungumza hapa mawaziri mpo, msiangaike kuleta waraka kwenye Baraza la Mawaziri  watafute mwekezaji  nije niitwe siku moja kufungua kiwanda cha Moproco kinachotengeneza mafuta ili kitengeneze ajira kwa watu wa Morogoro na watanzania. 
 
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliitaka Wizara ya Viwanda  kuvichukua viwanda ambavyo viko kwa wawekezaji na havijaendelezwa. 
 
Kwa upande wake, Rostam Azizi  alisema kuwa kiwanda hicho ni kikubwa  na chenye vifaa vya kisasa zaidi  barani Afrika ambacho kina uwezo wa kuchakata ngozi hadi hatua ya mwisho kwa kiwango  cha mwisho cha asilimia 65 ya ngozi zote za ngombe zinazozalishwa nchini na  ngozi za mbuzi na kondoo zinazozalishwa nchini kwa asilimia 100  na kitazalisha ajira 1,000. 
 
“Mheshimiwa Rais sera zako ndizo zilizotusukuma kuwekeza takriban bilioni 50 katika kufufua kiwanda hiki, umekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha na kusisitiza wawekezaji hasa wa ndani wawekeze ili uchumi wetu uweze kuboreka”, alisema Rostam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad