MKUU wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella ameaagiza watendaji wote wanaohusika na usajili wa Vizazi na Vifo kuweka mikakati itakayowezesha wananchi katika maeneno yao kusajiliwa ili kuwaondolea usumbufu wa kutokuwa na nyaraka mara wanapohitaji huduma nyingine.
Hayo yamesemwa hii leo Jijini Mwanza kupitia hotuba ya Mkuu wa Mkoa huo iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe.Dkt. Philis Nyimbi wakati wa kufungua mafunzo kwa Makatibu Tawala wa Wilaya na Maafisa Tarafa wa Mkoa huo yaliyoandaliwa na Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) yatakayosaidia kutekeleza majukumu yao ya usajili wa Kizazi,Vifo, ndoa na talaka kikamilifu.
Ameeleza kwamba umuhimu wa nyaraka mbalimbali zinazotolewa na RITA unaendelea kuongezeka hivyo lazima kuwe na mkakati wa kuwaelimisha wananchi kujisajili na kuwe na mikakati mahsusi itakayowezesha wananchi wengi zaidi kupata huduma kwa wakati.
Mhe. Mongella amewapongeza RITA kwa hatua ambazo wanaendelea kuchukua katika kuboresha mfumo wa usajili kupitia Mkakati wa Kitaifa wa Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu na Takwimu ambao unaendelea kutekelezwa kupitia Progam Mbalimbali. Ameongeza kwamba Mpango wa Usajili wa Watoto wa Umri Chini ya Miaka Mitano umeleta matokeo chanya kwa kuwawezesha watoto kupata cheti cha kuzaliwa karibu na maeneo wanayoishi ambapo na takwimu zake zimepatikana na kutumika katika kupanga mipango ya maendeleo.
Mhe. Mongella amewapongeza RITA kwa kuandaa mafunzo haya kwani inawezekana baadhi ya watendaji katika ofisi za Wilaya ni wageni katika nafasi hizo hivyo mafunzo haya yataongeza ufanisi. Amewataka washiriki kuzingatia mafunzo wanayopata na kuwataka kutunza Miongozo wanayopewa ili iwasaidie watendaji wengine siku za usoni.
Akizungumzia huduma za Mirathi na Wosia, Mhe. Mongella amewaonya baadhi ya wananchi hasa ndugu na jamaa wa karibu wa marehemu ambao wamekuwa na tabia za mnyanyasaji na uporaji wa mali za marehemu mara baada ya mazishi na hivyo kusababisha uvunyifu wa amani, upotevu wa mali na kuwanyima haki warithi halali kwa kigezo kwamba wao ni wasimamizi wa mirathi.
"Nawasihi viongozi wenzangu tutoe elimu kwa wananchi wetu kuanzia sasa wajenge utamaduni wa kuandika wosia mapema na waondokane na dhana mbaya kwamba ni uchuro,dhana hii siyo sahihi kama kufa tutakufa tu na kuacha matatizo makubwa ya ndugu kugombania mali".Alisema Mhe. Mongella.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Msaada wa haki za kisheria kutoka RITA Bi. Lina Msanga amesema kuwa sheria imetamka wazi kwamba kila tukio la kizazi, kifo, ndoa na talaka yanapotokea lazima yasajiliwe na kuhifadhiwa katika daftari la Msajili Mkuu wa matukio hayo ambaye ni Kabidhi Wasii Mkuu.
" Usajili ni takwa la kisheria lakini kuna sehemu kama watumishi wa umma hatutekelezi ipasavyo majukumu yetu na ndiyo maana leo hii tupo hapa kuwapatia mafunzo Maalum kuhusu sheria na miongozo mbalimbali itakayowasaidia kutekeleza majukumu yenu".Alisema Bi. Msanga.
Vilevile Katibu Tawala wa Wilaya ya Kwimba Ndugu Nyakia Chirukile amesema kuwa baadhi ya viongozi wa dini na kimila wamekuwa wakifungisha ndoa bila ya kufuata utaratibu na sheria hivyo kutosajili na kusababisha migogoro na hata vifo kwa wanandoa.
" katika wilaya yangu kuna binti ameozeshwa kimila na umri wake ulikuwa mdogo sana na hivyo kupata matatizo ya uzazi kwa kupungukiwa damu, tulimsaidia damu kwa bahati mbaya ndugu zake wakamtoroshwa kwa kuogopa vyombo vya sheria".Alisema Chirukile.
Kwa upande wake Afisa Tarafa ya Katunguru Bw. Batalangile Kaswahili amesema kuwa kukosekana kwa uadirifu na uwajibikaji kwa watumishi waliopewa dhamana ya kuwahudumia wananchi ndiyo chanzo kinachosababisha kukosekana kwa uratibu mzuri wa kuyasajili matukio mbalimbali yanapotokea.
" kwa mfano mimi katika Tarafa yangu nimepewa pikipiki nashindwaje kufuatilia utendaji kazi wa maafisa watendaji wa kata na vijiji ili wanipe hizo taarifa? huu ni usembe wetu sisi watumishi wa umma".Alisema Bw. Kaswahili.
RITA inaendelea kutoa mafunzo kwa Makatibu Tawala, maafisa Tarafa, maafisa watendaji kata na Watumishi wa vituo vya tiba vinavyotoa huduma ya mama na mtoto katika Mikoa yote ya Tanzania bara lengo likiwa ni kuwajengea uwezo katika uwajibikaji na kuongeza kasi ya usajili wa matukio hayo.
No comments:
Post a Comment