HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, February 25, 2021

Dkt. Ndungulile afurahishwa na huduma ya kufungua akaunti kidijitali kupitia SimBanking

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile (wa pili kushoto) akibonyesha sehemu ya mfano wa dole gumba wakati wa hafla ya uzunduzi wa maboresho ya huduma ya SimBanking ya Benki ya CRDB ambapo sasa hivi inawawezesha wateja wake kufungua akaunti wenyewe bure popote walipo, uliofanyika jana jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela.

Benki ya CRDB imeboresha huduma yake ya SimBanking ambapo sasa hivi inawawezesha wateja kufungua akaunti wenyewe bure popote walipo. Akizungumza katika hafla ya uzinduzi Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Faustine Ndugulile amezitaka benki nyingine hapa nchini kuiga mfano wa huduma bora za kiteknolojia zinazotolewa na Benki ya CRDB wakati huu wa kuelekea kwenye Tanzania ya TEHAMA. 

Dk. Ndugulile alisema lengo la Rais John Magufuli kuunda wizara maalum ya TEHAMA ni kuifikisha Tanzania kwenye ulimwengu wa teknolojia hivyo ipo kazi kubwa ya taasisi kuondokana na mazoea ya utoaji huduma kwa wananchi.

“Mheshimiwa Rais ametupa kazi kubwa ya kufanya kwenye wizara yetu maana tunatakiwa kuipeleka Tanzania kwenye ulimwengu wa TEHAMA. Niwapongeze Benki ya CRDB kwa ubunifu huu ambao unakwenda kuongeza ujumuishi wa Watanzania wengi katika sekta ya fedha “financial inclusion”. Hii itasaidia kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi kwa maana ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

“Nitoe rai kwa benki nyingine, kuiga sio dhambi... nao waige kwa Benki ya CRDB  yaani mteja anauwezo wa kufanya kila kitu kinachohusu akaunti yake na zaidi akiwa na simu yake ya mkononi.

“Benki ya CRDB wamenifariji zaidi baada ya kujua kwamba ubunifu wa huduma hii umefanywa na vijana wa kitanzania yaani ‘local services’ hili nalo ni jambo la kupongeza sana.

“...Hata serikali hivi sasa inawafuata wananchi kwa kuhakikisha masuala yote ya malipo ya serikali yanafanyika kwa simu za mkononi,” alisema Dk. Ndugulile ambaye pia ni Mbunge wa Kigamboni.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema lengo la taasisi hiyo kubwa ya fedha hapa Tanzania ni kumfikia mwananchi popote alipo kwa kutumia mifumo ya kidijitali.

“Tumejipanga vizuri kupitia kitengo chetu cha ubunifu wa kiteknolojia kinachoongozwa na vijana wazalendo kuhakikisha Benki ya CRDB inakuwa kinara wa teknolojia katika utoaji wa huduma zetu,” alisema Nsekela.

Nsekela alisema kupitia SimBanking mpya wateja sasa hivi wanafanya kila kitu kidijitali, kuanzia kufungua akaunti wenyewe kidijitali, kuomba mkopo kidijitali, kulipia bima kidijitali, kulipia ankara kidijitali na huduma nyengine lukuki. “… tumefanya maboresho makubwa sana ambayo yanampa uhuru mkubwa mteja wa kufanya miamala yote kupitia SimBanking na ndiomana sasa hivi tunasema Benki ni SimBanking,” aliongezea Nsekela.

Naye Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Khadija Said aliipongeza Benki ya CRDB kwa ubunifu bora wa huduma za kiteknolojia na kuwawezesha wateja wa benki hiyo kukata bima mbalimbali kwa kutumia simu ya mkononi. Naibu Kamishna aligusia pia kuhusu upatikanaji wa huduma ya stika za bima za magari kidijitali kupitia SimBanking pindi stika hizo zitakapozinduliwa rasmi mwezi Aprili.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad