Mkuu wa Wilaya ya Kishapu - Nyabaganga Taraba(aliyevaa kitenge)
akipokea moja ya vitanda kutoka kwa Meneja wa NMB Magharibi Kanda ya wa
NMB - Sospeter Magesse. Benki ya NMB ilikabidhi pia vitanda vitatu vya
kujifungulia na vinne vya kawaida na magodoro yake, pamoja na mashuka 25
kwa ajili ya hospitali ya Jakaya Kikwete.
***********************************
Mwandishi Wetu
Kishapu.
Benki ya NMB kupitia tawi lake la Kishapu imetoa msaada wa vitanda saba
vikiwemo vitatu vya kujifungulia na mashuka 25 kwa hospitali ya Jakaya
Kikwete ya halmashauri hiyo.
Msaada huo wenye thamani ya zaidi
ya Sh.milioni 5 unaotarajiwa kuoboresha huduma kwa wajawazito wilayani
humo ulikabidhiwa na Meneja wa NMB Kanda ya Magharibi, Sospeter Magesse.
Akikabidhi msaada huo ambao ni muendelezo wa misaada
inayotolewa na benki hiyo kuboresha sekta ya afya na elimu sehemu
mbalimbali nchini, Magesse alisema huo ni utekelezaji wa sera ya benki
ya kurejesha sehemu ya faida kwa jamii.
Alisema benki hiyo
imetenga bajeti ya Sh1 bilioni kwa mwaka kwa ajili ya kusaidia
utekelezaji wa miradi ya maendeleo na misaada wakati wa majanga ya
asili.
“Pamoja na sekta ya elimu na afya, NMB pia hushirikiana
na Serikali na wadau wengine kusaidia jamii wakati wa majanga ya asili.
Haya ni maeneo matatu tunayoyapa kipaumbele katika miradi yetu ya
kusaidia jamii,” alisema Magesse
Akifafanua kwanini NMB
imejikita katika miradi ya afya na elimu, meneja huyo ni kwa sababu
sekta hizo ni maeneo muhimu kwa maendeleo na ujenzi wa Taifa.
“Ili
kuendelea na kufanikiwa kiuchumi, Taifa linahitaji watu wenye afya
njema na elimu bora; hii ndiyo maana NMB inasaidia maendeleo katika
sekta za elimu na afya,” alisema Magesse
Mganga mkuu wa
Halmashauri ya Kishapu, Dk. Shani Mudamu alisema kupatikana kwa vitanda
vitatu vya kujifungulia kutaiwezesha hospitali hiyo kuwahudumia
wajawazito sita kwa wakati mmoja.
“Awali tulikuwa na uwezo wa
kuwahudumia wajawazito wanne pekee kwa wakati mmoja. Sasa tutaweza
kuhudumia sita huku kitanda kimoja kikiwekwa akiba kwa ajili ya
dharura,” alisema Dk. Mudamu
Akipokea msaada huo, Mkuu wa Wilaya
ya Kishapu, Nyabaganga Taraba aliushurku uongozi wa NMB kwa kuendelea
kuchangia miradi ya maendeleo wilayani humo.
“Mwanzoni tulipokea
Sh5 milioni kusaidia kupaua vyumba vya madarasa na majengo ya zahanati;
tukapokea Sh5 milioni nyingine ilichochea wazo la ujenzi kujenga shule
ya sekondari ya wasichana Kishapu; na leo tumepokea vitanda na mashuka
vyenye thamani ya Sh5 milioni. Tunaomba ushirikiano huu uendelee,”
alisema Taraba
Kuhusu huduma za kibenki, Taraba aliwataka wakazi
wa wilaya ya Kishapu kuchangamkia mikopo ya kuendeleza sekta sekta ya
kilimo inayotolewa na benki hiyo kuongeza tija katika shughuli zao.
“Wafugaji
wakope kunenepesha yao. Wakulima wakope trekta; tutumie benki hii
kuongeza tija katika sekta ya kilimo na mifugo ambayo ndiyo njia kuu ya
kiuchumi kwa Kishapu,” alishauri mkuu huyo wa wilaya
Mmoja wa
wajawazito waliokuwa wakisubiri huduma hospitalini hapo, Mariam Masanja
aliishukuru Serikali na wadau wa maendeleo ikiwemo benki ya NMB kwa
kuboresha huduma hospitalini hapo.
Friday, February 19, 2021

NMB yaongeza faraja kwa wajawazito Kishapu
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment