HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, February 17, 2021

NEMC WASAIDIENI WAWEKEZAJI KUZINGATIA SHERIA YA MAZINGIRA – WAZIRI UMMY MWALIMU

 

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo leo Februari 16, 2021 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Waziri Ummy Mwalimu yuko katika ziara ya kikazi ya siku tatu (3) yenye lengo la kukagua shughuli za utunzaji na Uhifadhi wa Mazingira

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu akipata maelezo kutoka Mkurugenzi wa Mji Kibaha Bi. Jenipha Omolo wakati wa ziara ya kukagua dampo la Mji Kibaha, leo Februari 16, 2021. Waziri Ummy ameagiza kujengwa kwa dampo la kisasa ili kunusuru mazingira.

Eneo la Dampo la Mji Kibaha ambalo si miundombinu yake si Rafiki kwa mazingira, Waziri Ummy Mwalimu ametoa maelekezo ya kuhakikisha dampo hilo linazungushiwa uzio na kupandwa miti.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu akiteta jambo na Diwani wa Kata ya Kibaha wakati wa ziara ya kukagua dampo la Mji Kibaha, leo Februari 16, 2021. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhandisi Martin Ntemo.

*****************************************

Serikali imesema kamwe haitakuwa kikwazo kwa wawekezaji katika kutoa vibali vya Tathmini ya Athari kwa mazingira katika kuwezesha uwekezaji na maendeleo ya viwanda.

Kauli hii imetolewa hii leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano ana Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Pwani kwa lengo la kukagua shughuli za utunzaji na Uhifadhi wa Mazingira

Amesema azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kuwa inaweka mazingira Rafiki kwa wawekezaji na kutoa miongozi katika hifadhi ya mazingira na kuliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kutoa ushauri wa kitaalamu kuwezesha wawekezaji kuzingatia Sheria.

“NEMC simamieni Sheria ya Mazingira, Viwanda visiwe sehemu ya uchafuzi wa Mazingira ili Maendeleo ya Viwanda yaendane na Hifadhi ya Mazingira pia NEMC msifanye kazi ya upolisi kwa kufunga Viwanda na kutoza faini kubwa, kaeni na wenye Viwanda waelekezeni kuzingatia Sheria” Waziri Ummy alisisitiza.

Katika hatua nyingine Waziri Ummy amemuagiza Mkurugenzi wa Mji Kibaha kuhakikisha katika Mipango na Bajeti wanatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa dampo la kisasa pamoja na kutoa elimu kwa wananchi namna bora ya kutenganisha taka kuanzia ngazi ya kaya.

“Mkurugenzi, taka ni mali, si kila taka ziende dampo, wekeni utaratibu kwenye vizimba kwa kutenganisha taka za plastiki, taka za majumbani na taka zinazoweza kurejerezeka ili wenye viwanda vya plastiki na vile vya kutengeneza mbolea waweze kupata malighafi” Ummy alisisitiza.

Akimkaribisha katika Mkoa wa Pwani Mkuu wa Mkoa Mhandisi  Evarist Ndikilo amesema Mkoa wake unakabiliwa na changamoto kubwa ya ukataji miti kutokana na matumizi ya kuni na mkaa na kutoa rai kwa Wizara kuangalia uwezekano wa kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala ikiwemo gesi. 

Pia ameshauri kuwekwa kwa utaratibu kwa wachimbaji wa mchanga kuhakikisha kunakuwa na urejerezaji wa maeneo ya machimbo kwa kupanda miti ili kuepuka uharibifu wa Mazingira. 

Waziri Ummy amesisitiza kuwa Agenda ya Mazingira ni suala mtambuka na kutoa rai kwa uongozi wa Mkoa wa Pwani kutumia Sheria ndogo za Halmashauri kusimamia suala la upandaji miti kwa kuanzisha vitalu vya miche.

Katika siku ya kwanza ya Ziara ya Waziri Ummy Mwalimu Mkoa wa Pwani ametembelea Dampo la Mji Kibaha, Kiwanda cha Futan Mining kinachojihusisha na uchenjuaji wa madini ya Kopa na Kiwanda cha Prance International Ltd.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad