Charles James, Michuzi TV
WAZIRI
wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile
amemuagiza Posta Masta Mkuu nchini Hassan Mwang'ombe kuhakikisha
anaimarisha kitengo chake cha ubunifu, utafiti na masoko ili kukuza
mapato ya Shirika hilo na kuongeza ufanisi kazini.
Dk Ndugulile
ameyasema hayo leo jijini Dodoma alipokua akifungua Baraza la 27 la
Wafanyakazi wa Shirika la Posta nchini ambapo amewataka kuzingatia
weledi na uzalendo kazini na yeyote ambaye ataenda kinyume na miongozo
ya kazi basi hatosita kumchukulia hatua kali za kinidhamu.
Amesema
anafurahi kuona Baraza hilo linaenda kujadili na kuweka mikakati ya
pamoja ya namna gani wanaweza kusonga mbele huku akiwataka wawasilishe
wizarani maazimio yote ambayo watayaazimia ili serikali iangalie namna
ya kuyafanyia kazi.
Waziri Ndugulile amewataka watumishi wa
Shirika hilo kongwe la Mawasiliano nchini kuacha kufanya kazi kwa mazoea
huku akiwataka kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia ili kuwa wa
kisasa zaidi.
" Nimeshapokea malalamiko yanayowahusu, Wizara hii
ni mpya lakini taasisi zake za kisekta siyo mpya, niwatake muwe na
mawazo mapya na fikra mpya ili tuweze kusonga mbele, tuongeze ubunifu,
utafiti na masoko mapya tutumie rasilimali za Posta kufikia wananchi ni
lazima tuingie kwenye ushindani tusibaki kung'ang'ania Telegram tu.
Mimi
kama Waziri siwezi kukubali kufanya kazi za Mameneja wa Mikoa, ambaye
atalala kwenye kituo chake cha kazi mimi nitambutua tu, hatutaki
ufanyaji kazi wa mazoea tena, tumeaminiwa ni lazima tuitunze imani
hiyo," Amesema Dk Ndugulile.
Kwa upande wake Posta Masta Mkuu,
Hassan Mwang'ombe amesema kupitia mkutano huo wa Baraza hilo la
Wafanyakazi watajadili mambo ya Msingi yenye tija kwenye Shirika lao na
Taifa kwa ujumla.
" Kikao hiki ni muhimu sana kwetu, kitaleta
uelewa wa pamoja na kitapunguza pia migogoro kazini, pia tumepanga
kujadili maslahi ya wafanyakazi wetu na kuongeza nidhamu serikalini,"
Amesema Mwang'ombe.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile akizungumza na watumishi wa wizara hiyo na wale wa Shirika la Posta nchini leo jijini Dodoma alipokua akifungua Baraza la 27 la Wafanyakazi wa Shirika hilo.
Baadhi ya wafanyakazi wa Shirika la Posta wakimsikiliza Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile leo jijini Dodoma alipokua akifungua Baraza la 27 la Wafanyakazi wa Shirika hilo.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile akiteta jambo na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Zainab Chaula wakati wa ufunguzi wa Baraza la 27 la Wafanyakazi wa Shirika hilo leo jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment