Wavuvi na Wakazi wa Kijiji cha Nyamikoma Wapewa Elimu ya Ufugaji wa Samaki kwa kutumia Vizimba - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, January 13, 2021

Wavuvi na Wakazi wa Kijiji cha Nyamikoma Wapewa Elimu ya Ufugaji wa Samaki kwa kutumia Vizimba

 

Mwakilishi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Silas William akitoa elimu ya ufugaji wa Samaki kwa kutumia Vizimba katika Mwalo wa Nyamikoma, Busega.

Elimu ya ufugaji Samaki kwa kutumia Vizimba imetolewa kwa Wavuvi na Wakazi wa kijiji cha Nyamikoma kilichopo kata ya Kabita wilayani Busega mnamo tarehe 11 Januari 2021. Elimu hiyo imetolewa huku ikiwa ni ombi la Wavuvi kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Mashauri Ndaki alipotembelea kijiji hicho na kufanya mkutano mnamo tarehe 30 Disemba 2020.

Katika kuhakikisha Serikali inaitikia kilio cha wavuvi na wakazi wa kijiji cha Nyamikoma, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeweza kutuma mwakilishi ili aweze kutoa elimu ya ufugaji wa Samaki kwa kutumia vizimba ili wavuvi waweze kupata uelewa wa kufuga Samaki kwa njia ya kisasa. Miongoni mwa mambo muhimu yaliyoelezwa na Afisa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Silas William ni pamoja na maeneo yanayofaa kwa kuweka vizimba, jinsi ya kutengeneza vizimba, aina ya vyakula vinavyotakiwa kulisha vifaranga vya Samaki, ukubwa wa vifaranga wanaotakiwa kufugwa na taratibu muhimu za kupata kibali cha ufugaji wa Samaki.

Aidha Bw. William amesema ufugaji huu una umuhimu mkubwa kwa uchumi wa mwananchi na kwa nchi kiujumla, huku akisisitiza ya kwamba ufugaji wa Samaki kwa kutumia vizimba katika ziwa Viktoria kwa sasa umelenga kwa ufugaji wa Samaki aina ya Sato pekee kwani ndio waliofanyiwa utafiti kitaalam wanaofaa kwa ufugaji.

Kwa upande mwingine Bw. William aliweza kueleza taratibu muhimu ambazo mfugaji atatakiwa kuzifata ili aweze kufanya ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba ikiwemo kuwa na taarifa ya utafiti wa eneo la kuweka kizimba, kibali cha utumiaji maji, mchoro pendekezwa wa kizimba, na mukhtasari wa serikali ya kijiji husika.

Wananchi wameonesha kuvutiwa na elimu waliyopewa lakini wameomba iwe endelevu ili iweze kuwajengea uwezo zaidi. Kwa upande mwingine wameiomba Serikali kuimarisha zaidi ulinzi ili watakapoanza ufugaji, ulinzi uwe miongoni mwa mambo muhimu kwani wanahofia wizi na muingiliano wa wanyama wengine kama Viboko ambao wamekuwa wakifanya uharibifu mara kwa mara.

Hata hivyo Bw. William amewatoa hofu wavuvi na wakazi wa Nyamikoma kwa kueleza kwamba suala la usalama ni moja ya masuala vipaumbele katika ufugaji huu na ndio maana Wizara ya Serikali inaelekeza kabla ya ufugaji kuanza ni lazima ufanyike utafiti wa kina ili kujua na kutathmini kama eneo linafaa kwaajili ya shughuli za ufugaji, pia kujua kama eneo linalokusudiwa kuwekwa vizimba halitakuwa na muingiliano wowote wa shughuli zozote na muingiliano wowote wa wanyama hatarishi ikiwemo Viboko.

Elimu ya ufugaji wa samaki inatolewa kwa wavuvi na wakazi wa Nyamikoma ikiwa ni mwitikio wa ombi kutoka kwa wananchi wa kijiji hicho kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi alipotembelea Mwalo wa Nyamikoma mwishoni mwa mwaka jana.

 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad