HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, January 14, 2021

BILIONEA LAIZER AJENGA SHULE NA KUIKABIDHI KWA SERIKALI

 



Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka kulia
akisalimiana na mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite Saniniu
Laizer kwenye uzinduzi wa shule iliyojengwa na Laizer.
Mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite bilionea, Saniniu Laizer
akizungumza baada ya kukabidhi kwa Serikali, shule ya msingi
aliyoijenga kwa gharama ya shilingi milioni 466.8 kwenye Kitongoji cha
Namelock Kijiji cha Naepo Kata ya Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani
Manyara.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Simanjiro Zuwena Omary Jiri akizungumza
baada ya mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite Saniniu Laizer
kukabidhi kwa Serikali shule ya msingi aliyoijengwa katika Kitongoji
cha Namelock Kijiji cha Naepo.

Mweyekiti wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara,
Adam Kobelo akipanda mti kwenye shule ya msingi Saniniu Laizer
iliyojengwa na mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite Bilionea
Saniniu Laizer.



Na Mwandishi wetu, Simanjiro

MFANYABIASHARA maarufu wa madini ya Tanzanite, Saniniu Laizer
ameikabidhi Serikali shule mpya ya msingi aliyoijenga kwa gharama ya
shilingi milioni 466.8 kwenye Kitongoji cha Namelock, Kijiji cha
Naepo, Kata ya Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.

Akisoma risala wakati wa kukabidhi shule hiyo mwanafamilia wa Laizer,
Simon Siria alisema shule hiyo itawanufaisha wanafunzi wa jamii ya
wakulima na wafugaji na ina madarasa saba.

Siria alisema shule hiyo ilianza kujengwa darasa moja na wananchi wa
kitongoji cha Namelock na kijiji cha Naepo mwaka 2017 ndipo bilionea
Laizer akaimaliza mwaka huu.

Alisema jamii iliona waanze kujenga shule kwani wakati wa mvua
wanafunzi huwa wanashindwa kuvuka korongo kwenda shule ya msingi Naepo iliyopo kilomita 1.5 kutoka katika eneo hilo.

"Shule hii itakuwa mkombozi kwa wanafunzi wa eneo hili kwani wengine
ni wadogo na iliwalazimu kutembea kilomita 2.5 kwenda shule ya msingi
Naisinyai na wengine kwenda Naepo," alisema Siria.

Bilionea Laizer akizungumza wakati akikabidhi shule hiyo kwa Serikali
alisema  imemgharimu jumla ya shilingi milioni 466.8 na hadi hivi sasa
kuna wanafunzi 30 wanaosoma hapo.

Bilionea Laizer alisema shule hiyo ina madarasa saba, matundu 10 ya
vyoo na nyumba mbili za walimu watakaoweza kuishi familia nne.

"Tunaomba serikali itupatie walimu na pia tunaomba shule hii iwe ya
mchepuo wa kiingereza ili wanafunzi watakaosoma hapo wawe bora kwenye
taaluma yao." alisema Bilionea Laizer.

Katibu Tawala wa wilaya ya Simanjiro, Zuwena Omary alisema Serikali
ipo pamoja na wachimbaji madini wenye kusaidia jamii kwa kuwekeza
kwenye miradi ya maendeleo.

"Kila mwanafunzi atakayesoma hapa na kufanikiwa kwenye maisha yake
hawezi kukusahau na pia utapata thawabu kutokana na tukio hili,"
alisema.

Alisema hivi sasa wanafunzi hao waliokuwa wanaotembea umbali mrefu
kufuata masomo katika shule za mbali watakuwa wanasoma karibu kwenye
shule hiyo ya msingi Saniniu Laizer.

Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka alisema
wachimbaji wengine wa madini ya Tanzanite wanapaswa kuiga mfano wa
bilionea Laizer kwa kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo ya jamii
ikiwemo shule.

Ole Sendeka alisema atamuunga mkono bilionea Laizer popote penye
kuhitaji mkono wa mbunge kwani amekuwa akisaidia jamii kupitia miradi
mbalimbali ya maendeleo ikiwemo shule na nyumba za ibada.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad