HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, December 7, 2020

NMB yapongezwa kuchangia maendeleo Zanzibar

 


 Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na chama tawala wamevutiwa na jinsi Benki ya NMB ilivyojipanga kushiriki katika shughuli za maendeleo visiwani humo na mchango inaoutoa kujenga uchumi imara wa kisasa.

 

Wakiongea wakati wa hafla ya Usiku wa Taarab Zanzibar siku ya jumamosi, viongozi hao walipongeza nia Benki ya NMB kufanya kazi karibu na serikali huku wakiahidi ushirikiano wa kutosha na Benki hiyo.

 

NMB inashiriki kuijenga Zanzibar kupitia huduma zake mbalimbali na tayari imejipanga kushirikiana na Serikali ya Dkt Hussein Ali Mwinyi kutekeleza miradi mbalimbali.

 

Akiongea kabla ya burudani kuanza, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alisema Benki hiyo si tu kuwa ina nia ya kusaidia maendeleo ya Zanzibar lakini pia ina msuli wa kuchangia kifedha.

 

“Benki ya NMB ina uwezo mkubwa kushiriki katika miradi mikubwa ya kimkakati.Benki ina mezania ya zaidi ya trilioni 7 sasa, mtaji na ukwasi wa kutosha,” Bi. Zaipuna alifafanua na kuongeza kuwa NMB ni benki ambayo ina uwezo na iko tayari kushiriki katika miradi mikubwa ya kimkakati.

 

Bi Zaipuna aliongeza kuwa “Mheshimiwa rais, tumejipanga vyema kuwahudumia wananchi wa visiwani na kusaidia kutimiza maono ya serikali mpya”.

 

Usiku wa Taarab uliandaliwa rasmi kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa ushindi wake wa kishindo. Hafla hiyo iliandaliwa na CCM Mkoa wa Mjini Magharibi huku NMB ikishiriki kama mdhamini mkuu.

 

Mbali na Dkt Mwinyi, viongozi wengine wakuu waliokuwepo ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdullah, na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mhe. Zubeir Ali Maulid.

 

“Ushiriki wa karibu wa Benki ya NMB katika hafla hii ni kielelezo kingine tosha cha utayari wa kufanya kazi na Serikali hii na kushiriki katika maendeleo ya Zanzibar,” Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt Abdulla Juma Mabodi, aliwaambia waliodhuria.

 

“Tayari wana mchango mkubwa kwenye uchumi wetu. Sisi kama chama pamoja na serikali tunawapongeza kwa hilo na tunawashukuru sana NMB kuwa tayari kuchangia kwenye uchumi wa bluu,” aliongeza.

 

Naye Mkuu Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi – Unguja, Bw. Idrisa Kitwana Mustafa, aliwaambia wanahabari baada ya hafla hiyo kuwa mchango wa NMB katika kuleta mageuzi ya uchumi wa bluu utakuwa wa msingi sana.

 

Maendeleo ya uchumi wa bluu ni moja ya ajenda kubwa za Serikali ya Awamu ya Nane. Katika hotuba yake ya uzinduzi wa Baraza la 10 la Wawakilishi mwezi uliopita, Dkt Mwinyi aliahidi kuijenga Zanzibar mpya kwa kupitia uchumi wa kisasa wa bluu.

 

Kuhusu uchumi huo, Bi. Zaipuna alisema: “Benki ya NMB imejipanga kushirikiana na serikali kutimiza maono yake kwenye uchumi wa bluu na tayari tumeanza kwa vitendo. Wiki hii tumetoa elimu ya kuwajengea uwezo wavuvi, wakulima wa mwani na wavunaji wa chumvi.”

 

Programu hii inalenga kuwafikia wananchi 2,000 itakapofika mwezi Machi mwaka 2021.

 

“Tukishawajengea uwezo, lengo ni kuanza kuwapa mikopo ya riba nafuu ya Fanikiwa ambayo huanza kwa kiwango cha chini cha shilingi 500,000 mpaka shilingi milioni 5,” Bi Zaipuna alifafanua.

 

NMB pia ina shiriki katika maendeleo ya utalii wa Zanzibar.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna alipowasili kwenye viwanja vya ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar kuhudhuria Taarab ya kumpongeza iliofanyika jumamosi usiku. Benki ya NMB ilikuwa ndiyo mdhamini mkuu wa taarab hiyo. Katikati ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Zuberi Ali Maulid.

Burudani ya Taarab ikiendelea.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad