HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 23 December 2020

Idara za Elimu katika Halmashauri zatakiwa “kujiongeza” ili kukabiliana na upungufu wa madarasa


Wakati wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wakijiandaa kuanza masomo yao yao mwezi Januari 2021, Idara za Elimu katika halmshauri za mkoa wa Rukwa zimetakiwa kuwa na mipango endelevu yenye kutekelezeka hasa ikizingatia maoteo ya wanafunzi wanaotazamiwa kuongezeka kutokana na uandikishaji wa wanafunzi na kuongezeka kwa ufaulu wao.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo ameyasema hayo alipotembelea songamebele ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari katika mtaa wa Utengule, kata ya Lwiche, Manispaa ya Sumbawanga ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu Mh. Kasim Majaliwa alipowaagiza Wakuu wa Mikoa kutoruhusu likizo kwa watumishi na watendaji serikalini kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliochaguliwa wanakwenda shule Pamoja na kupata meza na madawati.

Mh. Wangabo amesema kuwa kila mwaka wanafunzi wanaanza na kumaliza masomo yao na idara ya elimu inafahamu mahitaji ya vyumba vya madarasa na maotea ya ufaulu wanafunzi lakini wanashindwa kuweka mipango inayoendana na maotea hayo.

“Kwahiyo tangu sasa tunataka idara ya Elimu ijiongeze, tunataka itueleze maotea yanayoendana na hali halisi na tushirikishane wote kwa Pamoja ili tusifanye kazi kwa zima moto, sasa hivi tupo hapa kama vile tulikuwa hatujui kwamba wanafunzi wetu wapo darasa la sab ana watafaulu na hapa ufaulu wetu ni asilimia 80.28 waliofaulu kwenda kidato cha kwanza, sasa Je! Wangefaulu kwa asilimia 95 tungefanyaje?” Alihoji.

“Tuanze kujiongeza kwamba ufaulu kwa mwaka kesho unaweza ukafika asilimia 90, Je! Hawa watakuwa ni ongezeko la wanafunzi wangapi halafu tunakuja kuanza kufanya matayarisho, lakini watu wa elimu mmekaa tu, Halmshauri mmekaa tu, mpaka viongozi wa juu kabisa ndio wanakuja kutoa matamko maagizo, haipendezi wakati wataalamu wote wapo huku chini kikubwa tufanye kazi, yaliyopita si ndwele tugange yajayo,” Alisisitiza.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa manispaa ya Sumbawanga James Mtalitinya alimuhakikishia mkuu wa Mkoa huo kuwa hakuna mwanafunzi atakayebaki nyumbani hadi kufikia tarehe 28.2.2020 kwani nguvu iliyowekwa katika kumalizia ujenzi wa shule hiyo mpya utapelekea kuwapokea wanafunzi hao waliobaki kwaajili ya awamu ya pili ya kuripoti shule.

“Tumeona tuweke jitihada ya kumalizia shule ya Sekondari Utengule ambapo tunajenga madarasa saba kwaajili ya kuwachukua kwa minajili hiyo Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa tunategemea kuwachukua wanafunzi wote na tutabaki na ziada ya madarasa, lakini kwa kutambua pia tatizo hili la madarasa tumeweka mpango wa kujenga madarasa mawili kila shule ambazo tunategemea kufikia mwezi Juni 2021 ziwe zimefikia usawa wa linta ili mwezi Desemba tuweze kukamilisha,” Alisema.

Aidha, baadhi ya wananchi waliohudhuria songambele hiyo ya ujenzi wa madarasa saba ya shule hiyo mpya ya Utengule Niko Sanga amesema kuwa jambo kubwa lililowasukuma kuhamasika kushiriki katika ujenzi huo ni Pamoja na kuwapunguzia wazazi gharama za kuwalipia usafiri wanafunzi wanaofaulu katika Kata hiyo na kwenda kata ya jirani.

“Tumehamasika kwasababu shule ni ya kwetu maendeleo ni ya kwetu, Watoto watasoma hapa, tunaona ni kazi sana Watoto wanatoka Kizwite (kata ya jirani) anatembea kwa mguu kwasababu ya uchumi hatuna uwezo wa kumlipia nauli mtoto kila siku, tumehamasika kwasababu itakuwa karibu na Watoto wetu tunatamani sana iishe mapema ili Watoto wetu wasome maana Watoto wamefaulu wengi, waliochaguliwa ni wengi na vyumba ni vichache unakuta chumba kimoja kizwite kina wanafunzi Zaidi ya 300,” Alisema.

Wanafunzi 310 ambao wameochaguliwa na kukosa nafasi ya kuingia kidato cha kwanza katika Manispaa ya Sumbawanga kutokana na upungufu wa madarasa 7 wametoka katika kata ya Lwiche ambao wananchi wake wameamua kushirki songambele hiyo ili Watoto wao wasitembee umbali mrefu na pia kuwawezesha kuwa karibu na makazi yao.

Katika Songambele hiyo Mkuu wa Mkoa alitoa mifuko 30 ya Saruji kwaajili ya kuunga mkono juhudi za wananchi kuhakikisha madarasa hayo yanakamilika na wananfunzi wote waliochaguliwa wanaanza shule kabla ya tarehe 28.2.2020.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule (kulia) pamoja na Mkurugenzi wa manispaa ya Sumbawanga James Mtalitinya mifuko 30 ya Saruji ili kuunga mkono juhudi za ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari iliyopo mtaa wa utengule kata ya Lwiche Manispaa ya Sumbawanga.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo aliposhiriki katika Songambele ya ujenzi wa msingi wa darasa kwa Shule mpya ya Sekondari inayojengwa katika Mtaa wa Utengule Kata ya Lwiche Manispaa ya Sumbawanga.
Baadhi ya Wananchi na Viongozi wa Kiserikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule na Kamati za ulinzi na usalama za Mkoa wa Wilaya waliposhiriki katika Songambele ya Ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari katika Mtaa wa Utengule kata ya Lwiche  manispaa ya Sumbawanga.
Baadhi ya mafundi wakiendelea na ujenzi wa madarasa saba ya shule mpya inayojengwa katika Mtaa wa Utengule kata ya Lwiche ikiwa ni juhudi za kutekeleza sera ya kila Kata kuwa na Shule ya Sekondari.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad