Na Shukrani Kawogo, Njombe.
Katibu tawala wa wilaya ya Ludewa
Zaina Mlawa amewataka madiwani wote kuhakikisha kuwa mpaka kufikia
January 30 watoto waliofaulu darasa la saba na kupangiwa shule
wanaripoti katika shule walizopangiwa na kuanza masomo.
Hayo
ameyasema katika hafla ya kuwaapisha madiwani iliyofanyika katika ukumbi
wa Halmashauri ya wilaya na kuongeza kuwa wasisubiri serikali itumie
nguvu katika kufanikisha hili.
Amesema mara nyingi idadi ya
wanafunzi waliofaulu na kupangiwa shule ni tofauti na idadi ya wanafunzi
wanaripoti katika shule hizo kitu ambacho kinashusha ukuaji wa sekta ya
elimu katika wilaya hiyo.
"Madiwa mkisimama vyema katika nafasi
zenu mnaweza kuleta maendeleo ya elimu katika kata zenu na wilaya kwa
ujumla, hivyo mhakikishe mnatekeleza hili kwa ushirikiano na wazazi",
Alisema Mlawa.
Aidha kwa upande wa mbunge wa jimbo hilo Joseph
Kamonga amewaomba madiwani hao kusimamia vyema vyanzo vya mapato pamoja
na kubuni vyanzo vingine ili kukuza uchumi wa wilaya hiyo.
Aliongeza
kuwa wanapaswa kukusanya mapato ili fedha hizo zitumike kutatua
matatizo mbalimbali ikiwemo kuboresha sekta ya elimu na afya.
"Ndugu
zangu tusipoweza kukusanya mapato hatutaweza kutatua changamoto za
wananchi, hivyo tunapaswa kufanya hivyo kwa nguvu zote na pale
patakapotokea changamoto za kisera au Sheria Mimi simu yangu iko wazi
muda wote msisite kunishirikisha", Alisema Kamonga.
Kwa upande wa
mmoja wa madiwani hao Willbard Mwinuka amesema kuwa wameyapokea yote
waliyoaswa na wakuu wa idara mbalimbali pamoja na mbunge na wataenda
kutekeleza kwa kila hali ili kuleta maendeleo katika wilaya hiyo.
Alisema
kwa upande wake amejipanga vyema katika kufanya kazi kwa bidii na
atahakikisha analeta Maendeleo katika kata yake na wilaya kwa ujumla.
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga (Aliyesimama) akiongea na Baraza la madiwani katika kikao cha kwanza baada ya kuapishwa. Kushoto ni Balozi Dk. Pindi Chana, kulia ni mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa Sunday Deogratius, mwenyekiti wa halmashauri Wise Mgina na Mkuu wa mkoa wa Njombe Marwa Rubirya.
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga (kushoto) akiteta Jambo na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa Sunday Deogratius.
Viongozi mbalimbali wakiwasili katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Ludewa kwa lengo la kuwaapisha madiwani na kuanza kikao cha kwanza Cha Baraza. Kulia ni mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga, mbunge viti maalum Balozi Dk. Pindi Chana, mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa Sunday Deogratius pamoja na Mkuu wa mkoa wa Njombe Marwa Rubirya.
Katibu tawala wa wilaya ya Ludewa Zaina Mlawa (Aliyesimama kulia) akiongea na madiwani hawapo pichani, katika halfa ya kuwaapisha madiwani iliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri wilayani humo. Anayefuata ni mkuu wa mkoa wa Njombe Marwa Rubirya, mwenyekiti wa halmashauri Wise Mgina Pamoja na mkurugenzi wa halmashauri Sunday Deogratius.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa Sunday Deogratius akiteta jambo na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Wise Mgina. Kushoto ni mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga na kulia ni katibu tawala wa wilaya hiyo Zaina Mlawa na mkuu wa mkoa wa Njombe Marwa Rubirya.
Balaza la madiwani wilaya ya Ludewa pamoja na wageni waalikwa wakiwa wamesimama baada ya kuapishwa na kuchagua mwenyekiti wa halmashauri.
Mwenyekiti wa halmashauri wilaya ya Ludewa Wise Mgina akiwapa mikono meza kuu baada ya kupata ushindi wa nafasi hiyo kwa kura 32 Kati ya 35 zilizopigwa.
No comments:
Post a Comment