HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, November 19, 2020

SERIKALI YAZINDUA KAMERA 306 ZA THAMANI YA BILIONI 1.2 MIRERANI

 


Karibu Mkuu wa Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila akizungumza kwenye uzinduzi wa kamera hizo.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro mhandisi Zephania Chaula akizungumza kwenye uzinduzi wa kamera hizo kwa kufanya kazi kwa uadilifu.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Missaile Mussa akiwaleza watendaji wa sekta mbalimbali wanaofanya kazi kwenye ukuta huo kushirikiana kwa upendo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila kushoto akimkabidhi kitufe cha kuashiria uzinduzi wa mfumo wa kamera ndani na nje ya ukuta unaozunguka machimbo ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.

Na Gift Thadey, Mirerani

SERIKALI imezindua mfumo wa usalama wa kamera 306 zenye thamani ya shilingi bilioni 1.2 kwenye ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara wenye lengo la kuhakikisha usalama na ulinzi wa rasilimali hiyo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila akizungumza jana mji mdogo wa Mirerani wakati wa uzinduzi wa kamera hizo amesema kutokana na udhibiti na ulipaji kodi kwa wachimbaji wa Tanzanite hivi sasa Serikali inaendelea kuingiza kipato kupitia sekta ya madini.

Profesa Msanjila amesema kamera hizo zimefungwa na kampuni ya kizalendo ya Starfix Enterprises ya jijini Dar es salaam kwa gharama ya shilingi bilioni 1.2.

Amesema wakati wa mchakato wa kutafuta mzabuni wa kutengeneza kamera hizo kuna baadhi ya kampuni zilipeleka maombi ya kuweka kamera hizo kwa gharama mbalimbali ikiwemo shilingi bilioni 80 na shilingi bilioni 30.

“Kampuni hii ya kizalendo inapaswa kupongezwa kwani wamefanya kazi hii kwa maslahi ya Taifa tofauti na makampuni mengineyo ambayo yalitaka kujineemesha,” amesema.

Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, mhandisi Zephania Chaula amesema kamera hizo zitarahisisha kazi ya kulinda madini hayo na itaondoa kero ya kubaini wahalifu kwenye migodi hiyo.

Mhandisi Chaula amesema kupitia kamera hizo kutakuwa na ushahidi usiotia shaka endapo mtu atakamatwa akifanya uhalifu ikiwemo kupitisha madini.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Missaile Mussa amewataka wadau wa madini ya Tanzanite wasikubali kuumbuliwa na kamera hizo kwa kufuata sheria katika eneo hilo.

Mussa amewataka watendaji wa sekta mbalimbali wanaofanya kazi kwenye ukuta huo unaozunguka machimbo hayo washirikiane kufanya kazi kwa upendo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt Faraja Mnyepe ameahidi kuhakikisha askari wanaendelea kutimiza wajibu wa kulinda rasilimali hiyo kupitia kamera hizo zinazofanya kazi katika mazingira ya giza, mwanga, jua, mvua, mchana na usiku.

Hata hivyo, mmoja kati ya wafanyabiashara wa madini ya Tanzanite Elisha Mollel pamoja na kupongeza hatua ya kufungwa kwa kamera hizo ameiomba serikali ifanyie kazi changamoto ya miundombinu ya barabara.

Mollel amesema miundombinu inayotumika kupanda na kushuka kuelekea kwenye migodi ni mibovu hivyo serikali iitengeneze kupitia kodi zinazolipwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad